Na. Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Abdallah Ulega amewataka wananchi wanaofanya shughuli zao katika Ukanda wa
Bahari ya Hindi kuchangamkia fursa ya ufugaji viumbe maji wakiwemo kaa na
jongoo bahari ambao wamekuwa na soko kubwa nje ya nchi.
Akizungumza mwishoni mwa wiki
(24.04.2021) katika Kijiji cha Tawalani kilichopo kata ya Manza iliyopo Wilaya
ya Mkinga, Mkoani Tanga, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja mkoani
humo, Mhe. Ulega amesema Ukanda wa Bahari ya Hindi bado haujatumiwa vyema
katika kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, hivyo wananchi
kujikita zaidi katika uvuvi na kutojishughulisha na ufugaji wa viumbe maji
ambao wamekuwa wakitakiwa nchi mbalimbali.
Mhe. Ulega amebainisha kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amekuwa akizungumzia
sana Sekta ya Uvuvi kuwekeza kwenye uchumi wa bluu, hivyo wananchi hususan
wanaofanya shughuli za uvuvi wanatakiwa kuongeza wigo wa shughuli za kiuchumi
katika Ukanda wa Bahari ya Hindi zikiwemo za ufugaji wa viumbe maji hususan kaa
na jongoo bahari pamoja na kilimo cha zao la mwani.
“Shughuli za uchumi ziwe nyingi sana,
rais anataka twende na uchumi wa bluu, anataka tufanye kazi twende baharini
tufanye kazi lakini huku pwani tutengeneze vizimba kwa ajili ya shughuli
mbalimbali mfano kunenepesha kaa na majongoo bahari na tufunge Kamba kwa ajili
ya kulima mwani.” Amesema Mhe. Ulega
Ameongeza kuwa ni wakati sasa kwa
wananchi wa ukanda huo kuondoa umasikini kwa kuendeleza shughuli za uvuvi,
ufugaji wa viumbe maji pamoja na kilimo cha mwani ili waweze kuongeza mapato na
kuwa na wigo mpana zaidi wa kuongeza kipato kwa mwaka.
Akisoma taarifa ya Kikundi Shirikishi
cha Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) mwishoni mwa wiki (24.04.2021) katika
Kijiji cha Tawalani, katibu wa kikundi hicho Bw. Salehe Ally Sua amesema katika
kipindi cha miezi kumi wamepata tani 52 za mwani na kuziuza kwa Shilingi
Milioni 52 ambapo kwa sasa wamefanikiwa kupata soko la uhakika ambalo wanauza
Shilingi 1,250 kwa kilogramu moja.
Aidha, amesema kupitia kilimo hicho
kipato cha mtu mmoja mmoja kimeweza kuongezeka na kujikomboa kiuchumi hali
ambayo imewasaidia kujipatia maendeleo na kumudu mahitaji mbalimbali ya
kijamii.
Licha ya mafanikio hayo Bw. Sua amesema
wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya mabadiliko ya hali ya hewa
ambayo imekuwa ikiharibu zao hilo na kupanda na kushuka kwa bei ya zao mwani
katika masoko mbalimbali hali ambayo inawafanya wakulima kushindwa kuweka
mipango stahiki ya kilimo hicho pamoja na ukosefu wa vifaa kwa ajili ya kilimo
hicho.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri Ulega
amesema wizara itatoa Shilingi Milioni Nne kwa ajili ya kununua kamba za kilimo
cha mwani na kuelekeza fedha au kamba zenye thamani ya hiyo pesa ziwasilishwe
haraka katika kikundi hicho.
Amesema fedha hizo ziwe chachu kwa
ajili ya kukuza kilimo hicho na kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi itazidi kutoa
misaada mbalimbali kwa vikundi vinavyojishughilisha na kilimo cha zao la mwani
kwa kutoa vifaa zikiwemo kamba ili kuongeza uzalishaji wa zao la mwani hali ambayo
pia inaweza kuchochea uwepo wa viwanda vya kuzalisha bidhaa zitokanazo na
mwani.
Akiwa katika ziara hiyo ya kikazi ya
siku moja Mkoani Tanga, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega
ametoa msaada wa injini mbili za boti kwa ajili vikundi vya uvuvi vya Upendo
Beach Group na Songambele.
Injini hizo zenye thamani ya shilingi
Milioni 30 ambapo kila moja ina thamani ya Shilingi Milioni 15, Naibu Waziri
Ulega amewataka wavuvi hao kutotumia vifaa hivyo kwa kujiingiza katika uvuvi
haramu bali watumie kwa ajili ya uvuvi unaofuata sheria na kanuni na kwamba
serikali bado inaendelea kuweka mazingira mazuri ya uvuvi kwa kuondoa tozo
ambazo zimekuwa kero kwao.
Wakizungumza baada ya kukabidhiwa
injini hizo, viongozi wa vikundi hivyo wamesema wamefurahishwa na msaada huo
ambao utakuwa na tija kwao katika kuongeza kiwango cha uvuvi na kutumia muda
mfupi baharini na kuwataka wavuvi wengine kujiunga katika ushirika ili waweze
kupata misaada mbalimbali kutoka kwa wadau ikiwemo Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kutoka kulia) akiwa ameshikana mkono na Mwenyekiti wa kikundi cha Upendo Beach Bw. Mzee Makole, wakati Naibu Waziri Ulega akikabidhi msaada wa injini ya boti yenye thamani ya Shilingi Milioni 15 kwa ajili ya kukiimarisha kikundi hicho kwenye shughuli za uvuvi. Naibu Waziri Ulega amekabidhi msaada huo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi akiwa nje ya jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga wakati alipofika ziara ya kikazi ya siku moja mkoani humo. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martine Shigella na kwanza kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini Mhe. Ummy Mwalimu. (24.04.2021)
Katibu
wa Kikundi Shirikishi cha Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika Kijiji cha
Tawalani, kilichopo Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga Bw. Salehe Ally Sua
akifafanua jambo juu ya zao la mwani kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Abdallah Ulega, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martine Shigella na Katibu Tawala wa
mkoa huo Bi. Judica Omari, wakati Naibu Waziri Ulega alipofika katika kijiji
hicho kuhamasisha kilimo cha zao la mwani na kutoa ahadi ya wizara ya kutoa
msaada wa Shilingi Milioni Nne kwa ajili ya kununulia kamba maalumu ya kupandia
zao hilo ambazo ameagiza zifike katika kikundi hicho ndani ya muda mfupi.
(24.04.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni