Na. Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Abdallah Ulega amewataka wananchi wa Kijiji cha Horohoro Kijijini Kata ya Duga
katika Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, kutoruhusu mifugo ipitishwe kinyemela
mpakani kwenda nchi jirani badala yake wawafichue wanaofanya hivyo ili
kuwadhibiti kwani serikali inakosa mapato.
Mhe. Ulega aliyasema hayo mwishoni mwa
wiki (24.04.2021) wakati alipofanya ziara ya kikazi wilayani humo kwa
kutembelea eneo lenye ekari 23 ambapo kutajengwa mnada wa mifugo kijijini hapo
na kusema kuwa mnada huo utakuwa chachu ya kuinua maendeleo ya wananchi na
taifa kwa ujumla.
Alisema lazima wananchi wilayani hapo
kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri wa kudhibiti mifugo kupitishwa kinyemela
kwenda nje ya nchi ili kuiwezesha serikali kukusanya mapato hatua ambayo
itakuwa ni chachu kubwa kwao kuwezesha maendeleo.
“Niwaambie tu kwamba lazima hivi sasa
tujipange kwa ujio wa fursa za mnada huu kwani baada ya miaka miwili eneo hili
litakuwa na picha tofauti na ilivyokuwa hapo awali na litafungua ukurasa mpya
wa maendelea kwenye eneo lenu na tumekubaliana wizarani jambo hilo litaanza
mwezi wa tano, wazee wa duga mtupe ushirikiano kwa vijana wetu ambao watakuja
kufanya kazi hapa.“ Alisema Mhe. Ulega
“RC Shigella utakuwa umeacha alama kwa
hili na nyinyi wananchi RC ametoa rai mnada huo usigeuke kuwa ni dude ambalo
litakuwa limekaa halina shughuli za kufanya watu wanapitisha mifugo njia za
panya na nyie mnawaona na hamtoi taarifa kuzuia jambo hilo.” Alifafanua Mhe.
Ulega
Naibu Waziri huyo alisema mnada huo
ukianza kufanya kazi, eneo hilo litakuwa na shughuli mbalimbali ambazo
zitawasaidia kuwaingizia vipato mbalimbali vya kimaendeleo hali ambayo
itasaidia kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
“Lakini niwaambie kwamba mkiacha watu
wanapitisha mifugo kwa njia ya panya hakuna nchi inachokipata na wananchi
hamuwezi kupata chochote hapo ni sehemu nzuri ya kuhakikisha mnapaombea na
kupiga dua, sala tuweze kuinua uchumi wetu watu wa Mkinga.” Alisema
Aidha alisema mnada huo utaanza mwezi
Mei mwaka huu, huku akiwataka wakazi wa eneo la Kata ya Duga kuwapa ushirikiano
watumishi ambao watapelekwa kwa ajili ya kufanya kazi hiyo ya kuhakikisha
wanakusanya ushuru wa serikali.
Aliwataka pia wafugaji wa eneo hilo
kuhakikisha wanafuga kisasa ili waweze kuwa na ng’ombe wenye tija zaidi
kutokana na kwamba watanzania wapo kwenye mazingira mazuri ya kufuga kisasa
tofauti na nchi nyingine.
“Mhe. Rais wetu Samia Suluhu Hassan
anataka kuona ng’ombe wenye kilo 500 diwani wa Kata ya Duga na wengine tunataka
tukimbie mchakamchaka tufikie lengo la Rais anataka kuona tunauza nyama inatupa
tija, mfugaji anabadilika anapata kipato na nchi inapata mapato ya kutosha.”
Alisema.
Naibu Waziri huyo alisema kuwa Mkuu wa
Mkoa wa Tanga Mhe. Martine Shigella alibainisha kuwa mkoa unataka kufanya mambo
mbalimbali ya maendeleo lakini hayo yote hayawezi kufanikiwa ikiwa baadhi ya
watu wanapitisha ng’ombe kwenda nje ya nchi kinyemela kwa kutumia njia zisizo
rasmi.
Alifafanua kuwa ili kuongeza mapato ya
serikali kupitia mifugo, katika mwaka ujao wa fedha 2021/2022 Wizara ya Mifugo
na Uvuvi imepanga kutumia Shilingi Bilioni 4 na Milioni 400 kwa ajili ya
kujenga minada mbalimbali nchini ukiwemo wa Kijiji cha Horohoro Kijijini kata
ya Duga katika Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga.
Alisema ujenzi huo unatokana na takwa
la kisheria la magonjwa ya wanyama namba 17 ya mwaka 2003 ambayo inataka
kufanyika hayo huku akieleza kuwa wizara ina mipango mingi ya kuhakikisha
wanawasaidia wafugaji kuhusu sehemu za malisho.
Awali akizungumza katika eneo hilo la
mnada Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martine Shigella alisema moja ya tatizo kubwa
lililopo eneo la mpakani ni kutokuwa na mnada wa uhakika kwa ajili ya
wafanyabiashara na wafugaji wa mifugo, ndiyo maana serikali ya Mkoa wa Tanga na
Wizara ya Mifugo na Uvuvi zinataka kusiwe na ufugaji wa kuhamahama.
Mhe. Shigella alisema hotuba ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa bungeni hivi
karibuni, ameeleza nia yake ya kutaka
kuona wafugaji matajiri na siyo wa kuhamahama na ili kuweza kujenga mazingira
wezeshi ya eneo la kuuzia mifugo kwani bila kufanya hivyo, wafanyabiashara wamekuwa wakienda kuwalangua wafugaji kwenye
mazizi yao na hivyo kujikuta hawanufaiki
ipasavyo.
“Kuna soko kubwa nchini Kenya ambapo
baadhi ya wafugaji na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu walikuwa wanasafirisha
mifugo kwenda Kenya na baadhi ya watumishi wa serikali wasiokuwa waaminifu ndio
walikuwa wanaongoza mchakato huo wa kusafirisha mifugo bila kupitia kwenye
taratibu mahsusi zilizopo.” Alisema Mhe. Shigella
Hata hivyo alisema anaishukuru wizara
kwa kuliona hilo na kuunda kamati na
kuweza kubaini uwepo wa changamoto
walizokuwa wanalalamikia wafanyabiashara na wananchi wa Kijiji cha Horohoro
Kijijini kwani kubwa walilokuwa nalo ni mifugo kupitishwa kwenye njia isiyokuwa
rasmi, kutokana na kutokuwa na eneo maalumu ambalo mifugo kabla haijasafirishwa
inatakiwa ipumzishwe mahali ambapo itakaguliwa magonjwa na kukusanywa kwa tozo
kabla ya kusafirishwa kwenda nchi jirani.
Kwa upande wake Afisa Biashara wa
Minada kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Basil Mataba alisema wizara ina
jumla ya minada ya upili 14 na minada 11 ya mpakani ambapo mnada wa Kijiji cha
Horohoro Kijijini mara utakapoanza kufanya kazi utakuwa wa 12.
Bw. Mataba alisema wanategemea Mwezi
Mei mwaka huu mnada wa Kijiji cha Horohoro Kijijini utaanza kufanya kazi hivyo
kuondoa adha ambazo walikuwa wakizipata wafanyabiashara na wafugaji kutorosha
mifugo kwenda nje ya nchi ili kuuza mifugo yao.
Alibainisha hadi sasa eneo hilo la mnada tayari shughuli mbalimbali zinaendelea ikiwemo ya kufyeka nyasi na tayari kibanda cha kukusanyia ushuru kimeshasimikwa wakati wakiendelea na ujenzi wa eneo hilo huku akieleza kwamba wizara itaendelea na hatua za ununuzi wa vifaa kwa ajili ya uzio wa awali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni