Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel ameiagiza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), kufanya tafiti zitakazo lisaidia taifa kupiga hatua kupitia sekta ya mifugo.
Prof. Ole Gabriel, aliyasema hayo
wakati wa kikao cha baraza la wafanyakazi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo
Tanzania (TALIRI), kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya jiji Mkoani Dodoma Aprili 23, 2021.
Akizungumza na Wajumbe wa baraza hilo Prof. Ole Gabriel alisema kuwa, hakuna Taasisi nyingine ambayo Wizara hiyo inaweza kuitegemea katika suala la utafiti zaidi ya TALIRI, hivyo ni lazima ifanye tafiti zitakazo boresha sekta ya mifugo nchini na kuchangia pato la taifa.
“Tusibakie kujisifu tuu kuwa Tanzania
ni nchi ya pili barani Afrika kwa idadi kubwa ya mifugo lazima tujisifie kwa
namna tutavyoweza kutumia sekta hii kukuza uchumi wa taifa” alisema Prof. Ole
Gabriel
Alisema kuwa tafiti ndizo zinaweza
kulisadia taifa kutoka hapa lilipo na kupiga hatua kufikia nchi ambazo
zimefanikiwa katika sekta ya mifugo.
“Kama Rais alivyokuwa akitoa hotuba
yake bungeni alisema ng'ombe wetu akichinjwa nyama yake haiwezi kuzidi kilo 150
hii yote ni kutokana na kutokuwa na
utafiti wa mbegu bora ambazo zitaweza kutoa kiasi cha kutosha cha nyama”
alisema Prof. Ole Gabriel
Aidha alisema kuwa, TALIRI inatakiwa
kufanya tafiti ya mbegu bora za ngombe ili kuwa na uhakika wa nyama ya kutosha
pamoja na maziwa.
“Lazima sekta hii ya mifugo tui ‘link’
na Tanzania ya viwanda hivyo basi tunatakiwa kuhakikisha kuwa ng'ombe wetu
wanatoa nyama ya kutosha na iliyo bora, maziwa mengi, ngozi, pembe pamoja na
kwato” alisema Prof. Ole Gabriel
Kadhalika alisema kuwa kama sekta ya
mifugo itashindwa kuwa na bidhaa zitokanazo na mazao ya mifugo bora, hata
malighafi kwa ajili ya viwanda hazita kidhi viwango.
Aliongeza kuwa ni wakati sasa kwa
Taasisi hiyo kukaa mguu sawa silaha begani ili kuzalisha mifugo bora na kukuza
sekta ya mifugo.
Vile vile, aliiagiza TALIRI kuhakikisha
wanakuwa wabunifu katika kuangalia changamoto mpya zinazohusu wafugaji ili kuzifanyia kazi mara moja.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa baraza hilo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
TALIRI Dk. Jonas Kizima, alisema kuwa kikao hicho ni cha pili kwa baraza hilo
na moja ya kazi yake ni kupitia bajeti yake.
“Pamoja na kupitia bajeti pia
mweshimiwa Katibu Mkuu tutakuwa na maazimio ambayo tutayaandika na kukuletea
wewe ikiwa ni sehemu ya utekelezaji alisema Kizima.
Kwa upande wao Wajumbe wa baraza la
wafanyakazi TALIRI wamemshukuru Katibu Mkuu (Mifugo) kwa kuweza kufika na
kushiriki nao na kuahidi kuwa wamepokea
maelekezo yake na watahakikisha wanayafanyia kazi na kuyasimamia vizuri Ili
kuongeza tija na ufanisi katika kazi zao za kitafiti.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akiongea na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) (hawapo pichani) wakati wa kikao cha baraza la wanyakazi hao kulichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. (23.04.2021)
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) na Mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi, Dkt. Jonas Kizima (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa Taasisi hiyo na watumishi kutoka WMUV mara baada ya kikao cha Baraza la Wafanyakazi kulichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. (23.04.2021)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akisalimiana na watumishi wa Wizara pamoja na watumishi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) wakati alipowasili kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kufungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa TALIRI. (23.04.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni