Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa mlipuko wa magonjwa ya Nguruwe hayajitokezi mara kwa mara nchini.
Haya yamesemwa na Naibu Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega leo (23.04.2021) wakati akijibu swali Bungeni
lililoulizwa na Mbunge wa Jiombo la Ndanda, Cecil Mwambe.
Ulega amesema serikali kupitia Wizara
ya Mifugo na Uvuvi imeweka mikakati kuhakikisha inadhibiti mlipuko wa magonjwa
ya nguruwe. Mikakati hiyo ni pamoja na Kuhimiza wafugaji kuacha kufuga nguruwe
kwa njia huria, Kuzuia wageni kuingia kwenye mabanda ya nguruwe, Kuhimiza
wafugaji kupulizia dawa za kuua virusi na kupe kwenye mabanda na kuweka dawa ya
kuchovya kwenye milango ya mabanda, Kuweka katazo la kusafirisha nguruwe na
mazao yake kutoka sehemu zenye ugonjwa.
Vilevile Kuhimiza wafugaji kutokuruhusu
wachinjaji au wafanyabiashara kuingia katika mabanda na kuchagua nguruwe wa
kununua, Wafugaji kuepuka kulisha nguruwe mabaki ya vyakula kutoka kwenye
hoteli na migahawa, Kuacha kuchanganya nguruwe wageni na wenyeji kwenye banda
moja na Wafugaji kutoa taarifa za ugonjwa au vifo vya nguruwe pindi
vinapojitokeza kwa Mtaalamu wa Mifugo aliye karibu.
Mkakati wa Serikali kupitia Wizara ni
kuendelea kutoa elimu ya udhibiti kwa wadau wote katika mnyororo wa thamani,
wakiwemo wafanyabiashara na wasafirishaji wa nguruwe pamoja na watoa huduma za
Afya ya Mifugo. Kazi hii itaendelea kufanyaka kwa kuzingatia uhalisia katika
kila eneo kwa wafugaji wakubwa na wadogo.
Aidha, Ulega amesema suala la motisha
kwa wafugaji wa nguruwe serikali itakwenda kuliangalia kuona namna ya
utekelezaji wake ili ukuaji wa tasnia ya nguruwe uende sambamba na ukuaji wa
mifugo mingine.
Pia amesema kuwa serikali imejipanga
vyema kuhakikisha inajenga majosho katika vijiji lengo ni kuhakikisha maeneo
ambayo kuna wafugaji kuna kuwa na josho. Mkakati wa serikali ni kuendelea na
zoezi la uogeshaji kwani katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mafanikio
makubwa ya udhibiti wa magonjwa yaenezwayo na kupe.
Hivi karibuni kulijitokeza mlipuko wa
ugonjwa wa Homa ya Nguruwe katika mikoa kadhaa nchini na kusababisha hasara kwa
wafugaji. Ugonjwa huu unaosababishwa na virusi, hauna chanjo wala tiba. Njia
pekee za kudhibiti ugonjwa wa Homa ya Nguruwe ni kuzingatia kanuni bora za
ufugaji wa nguruwe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni