Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka wafugaji kusimamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wafugaji na kuhakikisha wanayatunza.
Ndaki ameyasema hayo jana (21.04.2021)
wakati akifungua mkutano wa kumi na moja (11) wa siku ya Nyanda za Malisho
Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Edema katika mkoani Morogoro.
Wafugaji wametakiwa kuhakikisha wanayasimamia
na wanayatunza maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za ufugaji na
kuyaendeleza kwa kupanda malisho na kuweka miundombinu ya maji kwa ajili ya
kunyweshea mifugo yao.
“Ni lazima maeneo yaliyotengwa kwa
ajili ya shughuli za ufugaji tunayalinda na kuyaendeleza kwa kupanda malisho na
kuweka miundombinu ya maji na siyo kuyaacha yabaki kama mapori kwani watumiaji
wengine wa ardhi wanaweza kuanza kuyatumia na baadae migogoro inaanza,” alisema
Ndaki.
Ndaki pia amewataka wafugaji
kuhakikisha wanaendelea kuomba ardhi kwa ajili ya shughuli za ufugaji katika
vijiji na kumilikishwa kwa kupata hati za kimila ili waweze kuwa na maeneo kwa
ajili ya mifugo yao lakini pia waweze kupanda malisho.
Akizungumza katika mkutano huo Waziri
Ndaki amesema viongozi ni lazima wabadili fikra pale wanapoona mifugo imeingia
katika maeneo yao, badala ya kulalamika inatakiwa watafute suluhisho kwani
uwepo wa mifugo ni fursa kiuchumi katika maeneo yao.
Vilevile amewataka wataalam kuendelea
kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu umuhimu wa kumiliki ardhi na upandaji wa
malisho kwa ajili ya mifugo yao.
Ndaki amekishukuru Chama cha Nyanda za
Malisho Tanzania kwa kazi nzuri wanayoifanyana na amewahakikishia kuwa Wizara
ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kuwapa ushirikiano kwani malisho kwa mifugo ni
jambo la muhimu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata
Sanare amesema kuwa mkoa wake kwa asilimia kubwa una wafugaji na wakulima
lakini tatizo kubwa lililopo ni watu kupata ardhi bila kufuata utaratibu, hata
kwenye maeneo ambayo tayari yalishapimwa na kutengwa kwa ajili ya shughuli za
kilimo, mifugo na watumiaji wengine wa ardhi.
Sanare amesema kwa sasa wanaendelea kuwadhibiti
watu ambao wanavamia ardhi bila kufuata utaratibu ikiwa ni pamoja na
kuwachukulia hatua viongozi kwenye vijiji na wataalam ambao wametoa hati za
kimila bila kufuata utaratibu au kwa kutojiridhisha.
Akisoma taarifa kwa niaba ya Katibu
Mkuu anayesimamia Sekta ya Mifugo, Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Maeneo ya
Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Dkt. Asimwe Rwiguza amesema wizara
imekuwa ikishirikiana na Chama cha Nyanda za Malisho na wataalam katika utekelezaji
wa majukumu mbalimbali ya uendelezaji nyanda za malisho hapa nchini.
Dkt. Rwiguza amesema wameshirikiana na
chama hicho katika maandalizi ya Mwongozo wa Upatikanaji, Usimamizi na
Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho ambapo mwongozo huo upo katika hatua za mwisho
ili uweze kuwasilishwa kwa wadau kwa ajili ya kupata maoni yao.
Wizara kwa kushirikiana na wadau
ikiwemo Chama cha Nyanda za Malisho imeendelea kutatua migogoro mbalimbali ya
ardhi inayowahusu wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. Vilevile Dkt. Rwiguza
amewasihi wafugaji kuhakikisha wanayatumia Mabaraza ya Ardhi ya Kata pale
wanapokuwa na migogoro ya ardhi.
Mwenyekiti wa Chama cha Nyanda za
Malisho Tanzania, Dkt. Ismail Selemani amemshukuru Waziri kwa kukubali mwaliko
wao na kushiriki katika kikao hicho. Lakini pia amesema kuwa Wizara ya Mifugo
na Uvuvi kila mwaka imekuwa ikiendele kutatua changamoto mbalimbali zinazohusiana
na Nyanda za Malisho.
Dkt. Selemani amesema kupitia wizara wanashuhudia kasi ya uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata mifugo na mazao yake hali ambayo itasaidia kukuza uchumi wa wafugaji na kuongeza mchango wa mifugo katika pato la taifa.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akisaini kitabu cha wageni ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wakati alipofika mkoani hapo kwa ajili ya kufungua mkutano wa kumi na moja (11) wa siku ya Nyanda za Malisho Tanzania utakaofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Edema. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Ole Sanare. (21.04.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni