Serikali kwa kushirikiana na wadau imepanga kudhibiti Uvuvi haramu kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu lililopo Mkoani Kilimanjaro.
Haya yamesemwa na Katibu Mkuu
anayesimamia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah leo (28.04.2021) baada ya
kumalizika kwa kikao cha ujirani mwema kilichojadili kuhusu ulinzi na usimamizi
wa rasilimali za Uvuvi kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu. Kikao hicho kiliwajumuisha
Viongozi na Wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wilaya za Mwanga,
Moshi na Simanjiro kilichofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Kindoroko wilayani
Mwanga.
Dkt. Tamatamah amesema kupitia kikao
hicho wamejadili kwa kina kuhusu tatizo la Uvuvi haramu unaofanyika kwenye
Bwawa la Nyumba ya Mungu na kutoka na maazimio ambayo Wizara na Halmashauri zilizoshiriki
pamoja na wadau watakwenda kuyasimamia utekelezaji wake lengo likiwa ni
kudhibiti shughuli za uvuvi haramu katika bwawa hilo. Moja ya maazimio hayo ni
pamoja na udhibiti wa uuzwaji wa samaki wadogo kwenye masoko yanayosimamiwa na
halmashauri.
“Samaki wadogo wanavuliwa pasipo halali
na huwa wanauzwa kwenye masoko ambayo yapo chini ya halmashauri, hivyo
tumekubaliana wote kuwa baada ya siku saba halmashauri zihakikishe samaki hao
hawauzwi tena katika masoko na hii itasaidia kuwafanya wavuvi kupunguza au
kuacha kuvua samaki hao kwa kuanza kukosa wanunuzi,” alisema Dkt. Tamatamah.
Dkt. Tamatamah amesema sera ya uvuvi ya
mwaka 2015 imekasimu majukumu ya usimamizi wa rasilimali za uvuvi kwa serikali
kuu kwa maana ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya TAMISEMI kupitia
Halmashauri na majukumu mengine yamekasimiwa kwa wavuvi na wadau wengine.
Vilevile amesema kuwa Wizara
inayojukumu la kutunga sera, sheria na kanuni lakini TAMISEMI kupitia
halmashauri zinaowajibu wa kuzisimamia na kuhakikisha kwamba utekelezaji wake
unafuatwa. Lakini kwa upande wa wavuvi wanaowajibu wa kushiriki katika ulinzi
shirikishi wa rasilimali za uvuvi kwa kuwa wao ndio wanufaika wa kwanza.
Mkutano huo umewahusisha wadau wa pande
zote kwa maana ya wizara, halmashauri na wadau ili kuwa na mkakati wa pamoja
badala ya kila mmoja kuwa na mkakati wake kuhusu udhibiti wa uvuvi haramu na
kuhakikisha rasilimali za uvuvi kwenye bwawa la Nyumba ya Mungu zinalindwa na
kusimamiwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mhe.
Thomas Apson amesema moja ya changamoto iliyojitokeza katika udhibiti wa uvuvi
haramu ni kwamba kila wilaya ilikuwa ikifanya doria kwa wakati wake hivyo
wavuvi wakiona doria inafanyika katika wilaya moja wanakimbilia kwenye wilaya
nyingine. Lakini kutokana na makubaliano ya kikao, sasa utawekwa utaratibu
mzuri wa doria zinazofanyika ili kutotoa tena nafasi kwa wavuvi kufanya uvuvi
haramu.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mhe.
Zephania Chaula amesema moja ya changamoto iliyopo ni ya uingizwaji wa zana
haramu za uvuvi kupitia mipakani. Hivyo ameziomba mamlaka zinazohusika
kuhakikisha zana hizo hazipitishwi kwani hiyo ni moja ya njia ya kudhibiti
uvuvi haramu hapa nchini.
Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara
ya Mifugo na Uvuvi, Emmanuel Bulayi amesema kwamba wizara inaendelea
kuwahamasisha wavuvi kujiunga kwenye vyama vya ushirika ili waweze kuunganishwa
na taasisi za fedha kama Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ambazo zipo tayari
kuwakopesha na hivyo wataweza kununua zana sahihi na zenye ubora kwa ajili ya
kufanyia shughuli za uvuvi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni