Nav bar

Jumanne, 21 Februari 2023

BIL 6.2 ZA MABWAWA KUNUFAISHA WAFUGAJI

Na. Edward Kondela


Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha kila sekta nchini ambapo imepanga kujenga mabwawa ya kunyweshea mifugo maji kote nchini.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumza (17.02.2023) wakati alipofanya ziara ya kikazi kukagua maendeleo ya ujenzi wa bwawa la maji la Kwekinkwembe lililopo katika Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga, amesema Rais Dkt. Samia katika bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2022/23 ameridhia kuipatia wizara Shilingi Bilioni 6.2 kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa hayo.


Naibu Waziri Ulega amefafanua kuwa kila sekta nchini imeguswa ikiwemo ya mifugo na kwamba hakuna iliyeachwa nyuma hivyo wafugaji watanufaika kwa kupata maji ya uhakika mara baada ya mradi wa ujenzi wa mabwawa ya kunyweshea mifugo maji kukamilika.


“Rais Mhe. Dkt. Samia hakuna aliyemuacha pembeni ndiyo maana amegusa wakulima mbegu za ruzuku, amegusa wafugaji mabwawa na majosho, hivyo hakuna aliyeachwa nyuma.” Amesema Mhe. Ulega.


Aidha amemtaka mkandarasi anayefanya shughuli za ujenzi wa bwawa hilo kuhakikisha anatoa taarifa ya kila hatua ya ujenzi na kuacha nakala wilayani hadi ngazi ya kijiji kunapojengwa bwawa hilo ili taarifa ziwe wazi na kumtaka kukamilisha ujenzi kwa wakati.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Mhe. Abel Busalama amewataka wananchi wa Kijiji cha Kwekinkwembe kuhakikisha bwawa hilo linalojengwa kwa thamani ya Shilingi Milioni 504 mara litakapokamilika walisimamie vyema ili liwe na tija kwao.


Amesema uongozi wa kijiji utapaswa kuweka utaratibu mzuri wa namna ya kulitumia na kuliongezea thamani kwa kuyafanyia pia maji hayo shughuli mbalimbali.


Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji nchini (CCWT) Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga Bw. Merieki Long’oni amesema ni faraja kubwa kwao kwa namna serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali kuwasogezea huduma ya maji karibu kwa ajili ya mifugo yao kwa kuwa maji ni shida katika baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amehitimisha ziara ya kikazi ya siku tatu katika Mkoa wa Tanga ambapo amekagua na kushuhudia maendeleo ya miradi mbalimbali ya sekta za mifugo na uvuvi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), (katikati) akikagua maendeleo ya ujenzi wa bwawa la kunyweshea mifugo maji la Kwekinkwembe lililopo katika Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga huku akimtaka mkandarasi kukamilisha ujenzi kwa wakati na kuwashirikisha viongozi wa eneo hilo. (17.02.2023)

Muonekano wa juu wa maendeleo ya ujenzi wa bwawa la kunyweshea mifugo maji la Kwekinkwembe lililopo katika Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga ambapo ni moja mabwawa yanayojengwa maeneo mbalimbali nchini yatakayogharimu Shilingi Bilioni 6.2. (17.02.2023)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni