Na Mbaraka Kambona, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Utunzaji wa Rasilimali za Uvuvi (EMEDO) chini ya Ufadhili wa Shirika la Royal National Lifeboat Institution(RNLI) linalojishughulisha na usalama kwenye maji na uokozi wanatekeleza mradi wa kuzuia wavuvi kuzama majini na kuhakikisha wanakuwa salama wakati wote wa shughuli zao katika Ziwa Victoria.
Mradi huo wa miaka 3 kuanzia 2022/2025 umelenga kuwaelimisha wavuvi hatua mbambali za kuchukua za kujizuia kuzama majini kabla ya kuingia kazini, lakini pia mradi utajikita katika kutoa mafunzo mbalimbali kwa jamii na wavuvi, BMU na watalamu wengine wa serikali wanaofanya kazi na wavuvi.
Pia, Mradi utashirikiana kwa karibu na taasisi za serikali zinazohusika moja kwa moja kwenye suala la usalama kwenye maji .
Lengo kuu la mradi huo ni kuhakikisha kuwa wadau wote wa sekta ya uvuvi kwa pamoja wanashirikiana kuchukua hatua mbalimbali za kuzuia matukio ya kuzama kwa wavuvi na wanakuwa salama wakiwa katika shughuli zao za kila siku.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Programu wa shirika la RNLI nchini Tanzania, Rachel Roland, mwaka 2019 walifanya utafiti kuhusu usalama wa jamii za wavuvi wanaoishi kandokando ya ziwa viktoria na walibaini kuwa asilimia 84 ya vifo vya wavuvi vinatokea wakiwa katika shughuli zao za kila siku za uvuvi katika ziwa.
Hivyo, mwaka 2022 RNLI na EMEDO walizindua mradi unaoitwa “Lake Victoria Drowning Prevention Project” kwa lengo la kufuatilia visa hatarishi vinavyochangia kusababisha kuzama kwa wavuvi katika ziwa hilo na kuchukua hatua za kupunguza vifo huku kauli mbiu ikiwa ni "Kuzama Kunazuilika, Chukua Tahadhari".
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu(Sekta ya Uvuvi), Bw. Stephen Lukanga alisema kuwa mradi huo ni muhimu kwa ustawi wa maisha ya jamii za wavuvi hivyo utekelezaji wake unahitaji ushirikiano wa karibu baina ya serikali na wadau katika kila hatua ili kuwe na uelewa wa pamoja wakati wote.
RNLI ni shirika la kimataifa lililoanzishwa mwaka 1824 kwa ajili ya kusaidia kuokoa maisha ya jamii zinazoishi kandokando ya bahari na ziwa nchini Uingereza na Ireland, lakini kwa sasa wamepanua wigo na kufanya kazi katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu (Sekta ya Uvuvi), Bw. Stephen Lukanga akisisitiza jambo wakati wa kikao cha kuwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Mradi wa Lake Victoria Drowning Prevention Project katika kikao kilichowahusisha Wataalam kutoka Sekta ya Uvuvi na Wataalam kutoka Shirika la EMEDO na Shirika la RNLi kilichofanyika Mtumba, jijini Dodoma Februari 15, 2023.
Mkuu wa Programu wa Shirika la RNLI nchini Tanzania, Rachel Roland akitoa maelezo mafupi kuhusu shughughuli za shirika hilo muda mfupi kabla ya kuwasilisha taarifa yao ya Utekelezaji wa Mradi wa Lake Victoria Drowning Prevention Project katika kikao kilichowahusisha wao na Wataalam kutoka Sekta ya Uvuvi kilichofanyika Mtumba, jijini Dodoma Februari 15, 2023.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu(Sekta ya Uvuvi), Bw. Stephen Lukanga(wa pili kutoka kushoto mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao cha kuwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Mradi wa Lake Victoria Drowning Prevention Project kilichofanyika Mtumba jijini Dodoma Februari 15, 2023. Wa kwanza kushoto mstari wa mbele ni Mkuu wa Programu wa Shirika la RNLI nchini Tanzania, Rachel Roland na kulia ni Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Utunzaji wa Rasilimali za Uvuvi (EMEDO), Madam Editrudith.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni