Nav bar

Jumanne, 21 Februari 2023

ULEGA: MSOMERA YAZIDI KUNG’ARA MIRADI YA WAFUGAJI YAPAA

Na. Edward Kondela


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amesema anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo serikali inahakikisha kila sekta inafikiwa katika maendeleo wakiwemo wafugaji na wavuvi.


Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo (16.12.2023) wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Kijiji cha Msomera kilichopo Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali inayowahusu wafugaji, yakiwemo mabwawa ya maji, minada ya mifugo, majosho na malambo ili kusogeza huduma karibu kwa wakazi wa kijiji hicho.


Amesema mbali na wafugaji ambao serikali imekuwa ikiwafikia kwa kuwapatia huduma mbalimbali za miundombinu kwa ajili ya shughuli za mifugo, wavuvi na wafugaji wa samaki pia wanafikiwa.


“Hakuna lililosimama yote yanasonga mbele makandarasi waendelee kushirikisha vyema wenyeji ambao wanajua mazingira ya hapa na wenyeji kushirikiana na makandarasi na wenyewe kuwashirikisha viongozi kila hatua.” Amesema Mhe. Ulega


Ameongeza kuwa anaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa imetenga fedha Shilingi kwa mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji kwa wafugaji, ikiwemo minada takriban Shilingi Bilioni 5.9 kwa ajili ya kujenga minada mipya na kukarabati ya zamani na Shilingi Bilioni 5.9 kwa ajili ya kutengeneza majosho.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Albert Msando akitoa taarifa ya wilaya kwenye kikao cha Kijiji cha Msomera ambacho Naibu Waziri Ulega alikuwa mgeni rasmi, amesema hadi sasa serikali imeshajenga majosho saba kwa ajili ya kuoshea mifugo, miradi kwa ajili ya malisho ya mifugo ambapo maandalizi yamekamilika yakiwemo ya upatikanaji wa mbegu.


Mhe. Msando ameongeza kuwa idadi ya mifugo iliyopo katika kijiji hicho ni mingi kuliko idadi ya wakazi wake ambapo inafikia zaidi ya 86,234 ikiwemo ng’ombe 28,049 mbuzi 32,743 kondoo 24,795 na punda 647.


Nao baadhi ya wanakijiji cha Msomera katika kikao hicho walipata fursa ya kutoa maoni na maswali kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) ambapo moja ya maoni yao ni kuwepo kwa vikundi vinavyojumuisha wanakijiji hao ili wapatiwe mashamba darasa na ng’ombe wa maziwa ili wafuge kisasa, ambapo Naibu waziri Ulega ameielekeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) kufika katika kijiji hicho na kutoa elimu juu ya mikopo kwa wafugaji hao ili waweze kufuga kwa tija na kibiashara kwa kuwa wana makazi ya kudumu.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) yuko Mkoani Tanga kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kujionea namna maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya sekta za mifugo na uvuvi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akiendesha trekta mara baada ya kufika katika moja ya mashamba darasa ya malisho ya mifugo kwenye Kijiji cha Msomera Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, katika ziara yake ya siku moja kwenye wilaya hiyo.  (16.02.2023)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni