WATAFITI na wanasayansi kutoka nchini 18 duniani, wamekutana jijini Arusha kutafuta ufumbuzi wa kutokomeza ugonjwa wa Ndorobo unaoenezwa na Mbung’o ambao umekuwa tishio kwa wanyama na binadamu kwa nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.
Akiongea
kwenye mkutano huo jana Jijini Arusha Mkurugenzi wa huduma za Mifugo kutoka
Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga alisema watafiti hao watakuja na
jibu la pamoja la namna ya kutokomeza ugonjwa huo unaotishia soko la Nyama kimataifa.
Amesisitiza
kuwa uwepo wa ugonjwa wa Ndorobo, Afrika inapata hasara ya takribani dola za
kimarekani bilioni 1.2 kutokana na gharama za matibabu na mifugo kukataliwa
kuchinjwa .
Amesema
Tanzania imefanikiwa kudhibiti ugonjwa huo kwa kiasi kikubwa ambapo hadi sasa
upo chini ya asilimia 1.5, lakini jitihada zaidi zinahitajika ili kuutokomeza
kutokana na mbung’o wengi kuwepo maeneo yaliyo jirani na misitu na hifadhi za
wanyama pori na hivyo kusababisha mifugo mingi kukondeana na hatimaye kufa
kutokana na vimelea wanavyoambukizwa na Mbung’o.
“Ng’ombe
anapougua ugonjwa huo hukondeana kwa muda mrefu, afya yake huwa mbovu na hivyo
hushindwa kuzalisha na nyama yake huwa mbovu haifai kuliwa na binadamu ndio
maana watafiti wamekutana ili kubadilishana uzoefu ili kupata njia bora ya
kutokomeza ugonjwa huo” amesema
Prof.
Nonga amesema kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya jitihada kubwa ya
kupambana na ugonjwa huo kupitia majosho ya uogeshaji mifugo zaidi ya 3000
yaliyopo nchi nzima ili kuua wadudu kupe na mbung’o.
“Serikali
imekuwa ikinunua dawa za kuogesha mifugo na kuzitoa kwa wafugaji ili wakaogeshe
mifugo yao na kutokomeza magonjwa yaenezwayo na Mbung’o, Kupe na Mbu
anayesambaza ugonjwa wa homa ya bonde la ufa” amesema Prof Nonga.
Aidha
amesema hapa nchini kuna viwanda vya nyama zaidi ya 10 vinavyohitaji kuzalisha
nyama iliyobora ili kuuza nje ya nchi, lakini vimeshindwa kukidhi mahitaji ya
soko kutokana na changamoto ya nyama kunakosababishwa na ugonjwa wa mbung’o.
Ameongeza
kuwa, pamoja na mambo mengine mkutano huo utakuja na majibu juu ya ufugaji bora
wenye tija utakaokuwa na manufaa kwa mfugaji kuweza kutajirika na mifugo yake. Alitoa
wito kwa wafugaji kuwatumia wataalamu wa mifugo pindi wanapoona uwepo wa dalili
za magonjwa hayo.
Naye
Dkt. Furaha Mramba ambaye ni mtafiti kiongozi kupitia mradi wa kudhibiti
ugonjwa wa Ndorobo kwa njia ya kutumia dawa Tanzania, amesema kuwa wamefanikiwa
kugundua aina saba za Ndorobo wenye uwezo wa kusambaza ugonjwa kwa mifugo na
binadamu.
Dkt.
Mramba ambaye pia ni Mkurugenzi wa kampuni ya kuzalisha chanjo za wanyama
Tanzania, amesema maeneo ya uhifadhi wa wanyama pori ndio yenye Ndorobo wengi
na hivyo aliwashauri wafugaji kuhakikisha wanafuata ushauri wanaopewa na
wataalam wa mifugo ikiwa ni pamoja na uogeshaji mifugo ili pale wanapolisha
maeneo jirani na hifadhi za Wanyama pori mifugo isiweze kuathiriwa na magonjwa
hayo.
Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo, Prof. Hezron Nonga akifungua mkutano uliowakutanisha watafiti wa mifugo Africa kujadili namna ya kudhibiti ugonjwa wa Ndorobo kwa kutumia dawa ambao umefanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha. (14.02.2022)
Mtafiti kiongozi wa Mradi wa kudhibiti ugonjwa wa ndorobo kwa njia ya dawa Tanzania, Dkt. Furaha Mramba akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mkutano uliowakutanisha watafiti wa mifugo Africa kujadili namna ya kudhibiti ugonjwa wa Ndorobo kwa kutumia dawa ambao umefanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha. (14.02.2022)
Baadhi ya washiriki wa mkutano uliowakutanisha watafiti wa mifugon Africa kujadili namna ya kudhibiti ugonjwa wa Ndorobo kwa kutumia dawa wakifuatilia mada zilizokuwa zinawasilishwa. Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha. (14.02.2022)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni