Nav bar

Jumanne, 21 Februari 2023

SERIKALI KUTUMIA BILIONI 1.8 KWA AJILI YA MASHAMBA DARASA YA UFUGAJI SAMAKI

Serikali  ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt.Rais, Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewezesha Halmashauri kumi na nne (14) kwa kutoa fedha kiasi cha Tsh 1.8 Bilioni kwa ajili ya kujenga miradi ya mashamba darasa ya Ufugaji Samaki.


Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe maji, kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Eng.George Kwandu (16.02.2023) alipoenda kukagua moja ya miradi hiyo uliopo Kijiji cha Tubugwe,kata ya Chamkoroma, Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma.


Eng. Kwandu amesema mradi huo wa  kijiji cha Tubugwe umegharimu kiasi cha Tsh 128 milioni, kwa lengo la kuwasaidia vijana na wanawake nchini ambapo itaobgeza ajira kwa vijana, kuongeza kipato na kuongeza usalama wa chakula.


Aidha, Eng kwandu  amesema mradi huo unatakiwa kutekelezwa katika kipindi cha miezi mitatu, ambapo kutakuwa na Ujenzi wa mabwawa manne ambayo kwa kila moja ina mita za mraba 600, mfeleji wa kupitishia maji, ofisi na jengo la kufundishia ufugaji samaki.


 "Tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha mradi huu, na kwa niaba ya katibu Mkuu Uvuvi niwaombe wanufaika muulinde mradi huu", amesema Eng. Kwandu.


Pia, ameongezea kwa kusema mradi huo unasimamiwa na Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, ambapo matarajio ya wizara mradi utakapo kamilika utawezesha wakulima Mia moja (100) kila wilaya.


Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Tubugwe Kibaoni, Bw. Noel Makubi, amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan  kwa kuona vyema kuleta mabwawa ya shamba darasa katika kijiji hicho ambapo wanakijiji watapata fursa kama ajira na kujiongezea kipato.


Pia, Makubi amemshukuru Mkurugenzi wa Uvuvi kwa kushirikiana nao vizuri kwakufika eneo la mradi huo na kufuatilia Miundombinu ya kuleta maji na kuhakikisha mradi unaenda sawa.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Dkt. Omary Nkulo(wa pili kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe maji Eng.GeorgeKwandu(wa pili kulia), wakati alipoenda kutembelea ofisini kwake na kumuelezea lengo la ujio huo ambapo ni kukagua mradi wa ujenzi wa mabwawa ya kufugia samaki kwa ajili ya Shamba darasa la ufugaji bora wa samaki katika kijiji cha Tubugwe kilichopo kata ya Chamkoroma, Wilayani hapo. Leo (16.02.2023.) na kushoto ni Afisa Uvuvi Mwandamizi Bw. John Mapunda.

Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe maji, Eng. George Kwandu (wapili kulia) akikagua cements ambazo zitatumika kujenga mradi wa mabwawa ya kufugia samaki kwa ajili ya Shamba darasa la ufugaji bora wa samaki, wakati alipoenda kutembelea mradi huo uliopo kijiji cha  Tubugwe, kata ya Chamkoroma, Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, (kushoto) ni  Afisa Uvuvi mwandamizi Bw. John Mapunda.16.02.2023.

Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe maji, Eng. George Kwandu (wapili kulia) akichukua vipimo vya mfeleji ambao utatumika kuchukulia maji na kupeleka kwenye mradi wa mabwawa ya kufugia samaki kwa ajili ya Shamba darasa la ufugaji bora wa samaki katika kijiji cha Tubugwe kilichopo kata ya Chamkoroma, Wilaya ya Kongwa. (16.02.2023)

Afisa Uvuvi mwandamizi Bw. John Mapunda (watatu kushoto) akielezea namna ya bwawa bora la kufugia samaki linavyopaswa kuwa na kuwaelezea mafundi wa ujenzi, sehemu ya kutolea maji inatakiwa iwe na kimo gani kitaalamu, wakati walipoenda kutembelea mradi wa ujenzi wa mabwawa ya kufugia samaki ambapo mradi huo utagharimu kiasi cha Tsh 128 milioni, katika kijiji cha Tubugwe kilichopo, Wilaya ya Kongwa. (16.02.2023).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni