Nav bar

Jumatatu, 29 Juni 2020

HALMASHAURI ZASHAURIWA KUIGA MACHINJIO YA ILALA.



Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Elisante Ole Gabriel amezishauri Halmashauri zote nchini ambazo zinafanya shughuli za ufugaji  kuiga mfano wa Machinjio ya kisasa ya Ilala ili nao waone haja ya kuwa na  machinjio ya kisasa yatakayosaidia kuboresha biashara ya machinjio na kuongeza pato la halmashauri zao.

Profesa Ole Gabriel alitoa rai hiyo ofisini kwake jijini Dodoma Juni 26, 2020 alipokutana na Timu ya Wataalamu kutoka Manispaa ya Ilala waliokuja kutembelea Machinjio ya Dodoma ili kujifunza namna ambavyo machinjio hayo yanavyoendeshwa.

Akiongea na Wataalamu hao, Prof. Ole Gabriel alisema itapendeza kama kila halmashauri ikawa na machinjio ya kisasa kwani yatasaidia kuongeza mapato ya halmashauri hizo na kuachana na kukimbizana kila siku na waendeshaji wa machinjio yaliyopo sasa ambayo hayana viwango ambavyo vinatakiwa.

“Niwaombe Makatibu Tawala wa Mikoa waliangalie hili, waone uwezekano wa kujenga machinjio ya kisasa yatakayosaidia kuboresha mazingira ya biashara yatakayochagiza kuongezeka kwa mapato ya Halmashauri,”alisema

Aliongeza kuwa sio lazima Halmashauri zijenge Machinjio wao wenyewe, wanaweza kuingia ubia na sekta binafsi na wakajenga machinjio ya kisasa wakawa wanauza nyama katika soko la ndani na nje ya nchi, kodi ya Serikali ikawa inalipwa na wateja wakaendelea kupata huduma nzuri.

Prof. Ole Gabriel aliendelea kusema kuwa biashara ya nyama sio ndogo huku akifafanua kuwa kwa sasa wastani wa kilo milioni 2.6 za nyama zinaliwa nchini kila siku na hivyo aliwahimiza maafisa biashara kuelimisha jamii kuhusu zao la nyama ili watu wale nyama kwa wingi.

“Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) mahitaji ya kidunia kwa mtu mmoja anatakiwa kula kilo 50 kwa mwaka, lakini sisi Watanzania bado wastani wetu wa kula nyama kwa mtu bado upo chini sana, kwa sasa tumefikia kilo 15 kwa mwaka, bado kiasi ni kidogo sana,” alieleza

“Maafisa biashara tumieni taaluma zenu kuelimisha umma kuhusu zao la nyama ili watu wale nyama, watu wakila nyama kwa wingi itachagiza biashara ya machinjio na ndipo hasa uwekezaji pia utakwenda vizuri,” alisisitiza

Aidha, aliipongeza Halmashauri ya Bahi kwa jitihada wanazoendelea nazo za kujenga machinjio ya kisasa jambo ambalo litaboresha biashara ya machinjio na kuongeza pato la Halmashauri hiyo.

Akielezea kuhusu machinjio ya Dodoma, Prof. Ole Gabriel alisema kabla machinjio hayo hayajachukuliwa na Serikali ng’ombe waliokuwa wanachinjwa kwa siku ni kati ya 40 mpaka 50 lakini toka machinjio hiyo irudishwe serikalini namba ya ng’ombe wanaochinjwa imepanda kufikia 150.

Aliendelea kueleza kuwa mikakati waliyonayo kuhusu machinjio hayo ni kuendelea kuiboresha kufikia kuwa Machinjio ya Mfano kwa Afrika Mashariki, Ukanda wa Nchi za SADC na hata ikiwezekana Afrika.

Aidha, Prof. Ole Gabriel alisema kuwa anaamini ziara hiyo ni katika  kutambua jitihada za Wizara na hivyo aliwahakikishia wataalamu hayo kuwa Wizara ipo tayari kushirikiana na Manispaa ya Ilala kuhakikisha mipango yao inafanikiwa na machinjio hiyo iweze kufanya kazi zake kama walivyokusudia.

Naye Afisa Masoko wa Manispaa ya Ilala, ambaye pia ndiye alikuwa kiongozi wa timu hiyo ya Wataalamu, Ando Mwankuga alisema machinjio ya Ilala ni mradi wa kimkakati katika kuboresha mazingira ya biashara ya machinjio ambayo itawawezesha kuwa na nyama za viwango zitakazouzika  hata  nje ya nchi.

“Lengo la mradi ni kuongeza mapato ya Manispaa, tunaamini mradi ukikamilika na kuanza kazi tutapunguza utegemezi kwa Serikali,” alisema

Alisema machinjio hiyo ambayo ni kubwa na ya kisasa inategemewa kuanza kufanya kazi Disemba, 2020 na watakuwa wanachinja   ng’ombe 1500 na mbuzi 1000 kila siku.



Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akisisitiza jambo wakati akiongea na timu ya wataalam kutoka manispaa ya Ilala (hawapo pichani) waliokuja kumtembelea ofisini kwake jijini Dodoma Juni 26,2020. Kulia ni Afisa Mipango wa Manispaa ya Ilala, Ando Mwankuga, kushoto niKaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji Mifugo na Masoko wa Wizara ya mifugo na Uvuvi Bw. Abdallah Temba. 



Afisa Mipango wa Manispaa ya Ilala, Ando Mwankuga akieleza lengo la Ziara yao kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) walipomtembelea ofisini kwake mapema Juni 26,2020. 



Baadhi ya wajumbe kutoka Manispaa ya Ilala wakiwa katika kikao wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo pichani) walipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma. Juni 26,2020. 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni