Nav bar

Ijumaa, 26 Juni 2020

MADAKTARI WA MIFUGO WATAKIWA KUHUISHA TAARIFA ZAO.



Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania, Dkt.Bedan Masuruli amewataka Madaktari wa Mifugo nchini kuhuisha majina yao kwenye daftari la usajili wa madaktari wa mifugo  kabla ya  Julai 1, 2020.

Wakati akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma Juni 26, 2020, Dkt. Masuruli amesema ni muhimu wataalam kuhuisha majina yao ili baraza liweze kufahamu wako wapi, wanafanya nini na wanatoa huduma gani.

"Nasisitiza madaktari wote wa mifugo ambao hawajahuisha taarifa zao kwenye daftari la usajili wa madaktari wafanye hivyo kuanzia leo hadi kufikia Juni 30, 2020 kwani kuanzia Julai mosi tunaanza kusimamia Sheria" amesema Dkt. Masuruli.

Hata hivyo Dkt. Masuruli amesema wanafanya haya yote ili kuboresha huduma kwa wafugaji wote nchini na watatoa vitambulisho kwa wataalam wote ili wafugaji waweze kuwatambua.

 Amesema kuwa wamejipanga kusambaza wataalamu wa mifugo kwenye ngazi za msingi ili kuwa karibu na wananchi na kuwashauri namna ya kuipatia kinga mifugo hiyo na kuleta tija katika ufugaji wao.

Aliongeza kuwa ili kufikia adhima hiyo ni lazima wataalamu wote wa ngazi ya msingi kusajiliwa, kujiandikisha na kujiorodhesha katika daftari ili kusaidia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kujua ubora wa wataalamu walionao katika maeneo yote na kusaidia wananchi  kuongeza tija katika  sekta ya ufugaji.


Tumeongeza muda ili wataalum waweze kuhuisha majina yao kwenye daftari la usajili wa madaktari kabla ya Julai 1 wawe tayari wamejisajili, na kwa ambaye hata fanya hivyo sheria za usajili zitachukua mkondo wake,alisisitiza

“Baada ya kuhuisha taarifa zao,  wataalamu watapatiwa vitambulisho maalum ili kusaidia wafugaji na wananchi kutambua kuwa ni mtaalamu aliyekidhi viwango hivyo, mwananchi anaweza kupatiwa huduma kwa kupata ushauri, kinga na namna ya kuboresha ufugaji ili kufikia mafaniko makubwa, aliongeza

Dkt.Masuruli amesema kuwa Wataalamu hao  watatakiwa kuwasilisha Wizarani taarifa za magonjwa ya mifugo inayosumbua katika maeneo yao ili kusaidia serikali kuandaa mpango kazi wa kutatua changamoto zilizoshindikana kutatuliwa na wataalaum hao.

Aidha, amesisitiza kuwa lengo kuu la kusogeza huduma hizo kwa wananchi ni kutaka kuhakikisha wanapatiwa huduma bora zinazokidhi viwango na itasaidia kubaini magonjwa yanayojitokeza katika mifungo ya wananchi wanao wahudumia na kuwasaidia kwa ukaribu.

“Natoa wito kwa vituo vyote vya afya ya wanyama kuanzia Julai Mosi, 2020 kuweka mpango wa muda wa miezi mitatu kupata hadubini katika vituo hivyo ili kusaidia kujua magonjwa katika mifugo ya wananchi wao wanao wahudumia, alifafanua.

Dkt.Masuruli ameongeza kuwa   ili wananchi waweze kunufaika na ufugaji wanahitaji wataalamu wa mifugo kuwa karibu na wafugaji ili kuwasaidia kuwapatia huduma bora itakayokidhi viwango na kuleta tija kwa asilimia kubwa na kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.



Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania, Dkt. Bedan Masuruli akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) lengo ni kuwataka madaktari wa mifugo kuhuisha majina yao kwenye daftari la usajili kabla ya Julai mosi 2020 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni