Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Magufuli
ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa jitihada kubwa ilizozichukua katika
kipindi cha miaka mitano ya Uongozi wake ambazo zimesaidia kuboresha na kukuza
uchumi wa nchi.
Akizungumza wakati akitoa hotuba yake ya kulifunga Bunge la kumi
na moja (11) la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Juni 16, 2020 jijini Dodoma,
Rais Magufuli alisema kuwa katika kipindi hiki cha miaka mitano ya uongozi wake
Wizara ya mifugo imechukua hatua kadhaa ambazo zimesaidia nchi kufikia
mafanikio makubwa.
Rais Magufuli akitaja baadhi ya maeneo ambayo Wizara
imeyashughulikia na kupata mafanikio, alisema kuwa katika kipindi hicho
serikali iliongeza eneo la ufugaji kutoka hekta milioni 1.4 mwaka 2005 hadi
kufikia hekta milioni 5 mwaka 2020. Jambo ambalo amelitaja kuwa limechangia kwa
kiasi kikubwa kupunguza migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, Serikali kupitia Wizara imejenga
mabwawa mapya ya kuogeshea ng’ombe 104, imesambaza chanjo na dawa za Mifugo
nchi nzima, huku idadi ya ng’ombe waliohimilishwa imeongezeka kutoka laki moja
na elfu tano (105,000) mwaka 2015 hadi kufikia laki tano kumi na nne elfu na
mia saba (514,700).
Aliongeza kuwa serikali imeimarisha ulinzi na usimamizi wa
rasilimali za uvuvi, kwa kuanzisha kanda kuu tatu (3) za Ziwa Victoria,
Tanganyika na Pwani ikiwa ni pamoja na kudhibiti zana haramu za uvuvi.
“Nakumbuka kuna wakati nilimuona Mhe. Mpina alikuwa anatembea na
rula kwenye Migahawa kupima urefu wa Samaki, hiyo ilikuwa ni katika hatua za
kuhakikisha tunapata mafanikio haya ambayo tumeyapata”, alisema Rais Magufuli.
Aliendelea kusema kuwa Wizara imehamasisha na kufanikiwa
kuongeza idadi ya Wafugaji wa Samaki kutoka laki moja themanini elfu na mia
nane arobaini na tatu (180,843) mwaka 2015 hadi kufikia laki mbili sitini elfu
mia nne sabini na nne (260,474) mwaka 2020.
“Katika kipindi hiki tumeongeza idadi ya Mabwawa kutoka 220,545
hadi kufikia 260,445 na kuongeza vizimba vya samaki kutoka 109 hadi 431, na
uzalishaji wa Vifaranga vya Samaki vimeongezeka kutoka milioni nane na tisini
elfu (8,090,000) hadi Vifaranga milioni kumi na nne laki tano thelathini na
moja elfu mia nne themanini na saba (14,531,487)”, aliongeza Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa sambamba na mafanikio hayo
serikali imeongezea mtaji kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kiasi cha
Shilingi Bilioni Mia Mbili na nane kupitia Mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya
Afrika. Pia serikali imeipatia TADB Dola za Kimarekani Milioni 25 sawa na
Shilingi Bilioni 57.8 ili kuendesha Mfuko wa dhamana.
“Hii ina maana kuwa kwa miaka mitano iliyopita Serikali imeipa
TADB Shilingi Bilioni 324.8 kuiwezesha Benki hiyo kutoa mikopo ya moja kwa moja
kwa wakulima, wafugaji na wavuvi yenye thamani ya kiasi cha shilingi bilioni
166.9 kwa Riba nafuu”, aliongeza Rais Magufuli
Kutokana na hatua hizo, Rais Magufuli alisema kuwa mafanikio
makubwa yamepatikana ambapo Sangara kwenye ziwa Victoria wameongezeka kutoka
tani 417,936 mwaka 2016 hadi kufikia tani 816,964 mwaka 2020.
“Kufuatia hatua hizo, urefu wa Sangara umeongezeka kutoka
wastani wa sentimeta 16 hadi kufikia sentimeta 25.2 jambo ambalo limefanya
samaki wetu kuanza kuhitajika kwa kiasi kikubwa katika soko la Ulaya na nyinyi
ni mashahidi Waheshimiwa Wabunge ndege zimeanza kuja Mwanza na kubeba Samaki
wetu kwa ajili ya kupeleka nje ya nchi”, alisisitiza Rais Magufuli.
“Kwa kuzingatia hilo mauzo ya samaki nje ya nchi
yameongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 379 mwaka 2015 hadi bilioni 692
mwaka 2019”, alieleza Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli alisisitiza kuwa mafanikio hayo sio mambo
madogo ni hatua muhimu katika kukuza uchumi wa nchi ambao kwa sasa upo katika
hatua nzuri ya kufikia uchumi wa kati ifikipo mwaka 2025.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Magufuli Akizungumza
wakati akitoa hotuba yake ya kulifunga Bunge la kumi na moja (11) la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Juni 16, 2020 jijini Dodoma.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni