Baraza
la Veterinari nchini Tanzania limewataka watu wote ambao hawana sifa za
Udaktari wa Mifugo kuacha mara moja kuhudumia na kutibu Mifugo huku likionya
kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa watakao kwenda kinyume na Sheria.
Onyo
hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Veterinari, Profesa Rudovick Kazwala
katika Mkutano wa 45 wa Baraza hilo ulilofanyika jijini Dodoma Mei 4, 2020.
Akiongea
na Vyombo vya Habari mara baada ya Mkutano huo, Profesa Kazwala alisema kuwa
kutokana na fani hiyo ya Udaktari wa Mifugo kuingiliwa na watu wasiokuwa na
sifa Baraza limeamua kuandaa vitambulisho na beji vitakavyowatambulisha
Madaktari hao pindi wanapokwenda kutoa huduma kwa wafugaji.
“Wale
wote wanaojiingiza katika fani hii bila kuwa na vyeti vya kitaaluma wajue kuwa
kuna sheria namba 16 ya Veterinari ya mwaka 2003 ambayo inakataza mtu ambaye
hajasomea taaluma ya Udaktari wa mifugo kufanya kazi ya kuhudumia na kutibu
mifugo, atakayekutwa na kosa hilo sheria itachukua mkondo wake” alisema Profesa Kazwala
Alisisitiza
kuwa kuanzia sasa wafugaji wanapaswa kujua kuwa wataalamu wa mifugo watakuwa na
vitambulisho vitakavyokuwa vinatolewa na Baraza hilo na kuwataka kuwakataa watu
watakaokuwa wanakwenda kutaka kutibu mifugo yao bila kitambulisho.
“Huko
nyuma hatukuwa na vitambulisho, kukosekana kwa vitambulisho kulipelekea watu
wasio na sifa kujiingiza katika kazi ya tiba ya mifugo na kuchafua sifa za fani
yetu”,alisema Profesa alifafanua
Kufuatia
changamoto hiyo, Profesa Kazwala alisema mkutano huo umekubaliana na kupitisha
maamuzi kuwa wataalamu wa mifugo wawe na vitambulisho ambavyo vitasaidia kuzuia na kuwaondoa watu wasio na sifa ya
udaktari wa mifugo.
Aliongeza
kuwa watahakikisha wakaguzi wa mifugo wanapita kila mara kwa wafugaji kukagua
mifugo yao na kufuatilia kama kuna watu kama hao ambao wanaendelea kuvunja
sheria.
Profesa
Kazwala ametoa wito kwa wafugaji na wananchi kwa ujumla kushirikiana na Baraza
hilo kuwakataa watu hao wasio na vitambulisho huku akiwasisitiza hata hao
madaktari watakaokuwa na vitambulisho wanapokwenda kutibu mifugo yao kuweka
kumbukumbu zao vizuri ikiwemo namba ya usajili ya mtaalamu huyo ili kama
likitokea tatizo lolote litakalo sababishwa na mtaalamu huyo iwe rahisi
kumtambua.
Aidha,
Profesa Kazwala amewaeleza wananchi kuwa huduma za mifugo zinaendelea
kuboreshwa nchini na kuanzia sasa vituo vyote vinavyotoa matibabu ya wanyama
lazima viwe na vifaa vya kuchunguza mifugo kwa
maana ya Darubini ili kutoa vipimo sahihi vya Sampuli zitakazokuwa
zinachukuliwa kutoka kwa mifugo.
Mwenyekiti
wa Baraza la Veterinari Tanzania, Prof. Rudovick Kazwala akiongea na waandishi
wa habari muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wa 45 wa Baraza la Veterinari
Tanzania uliofanyika jijini Dodoma. (04/06/2020)
Mkurugenzi
wa Huduma za Mifugo, Prof. Hezron Nonga akifafanua jambo mbele ya vyombo vya
habari katika mkutano wa 45 wa Baraza la Veterinari Tanzania uliofanyika jijini
Dodoma. (04/06/2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni