Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi amesema Serikali imedhamiria kuboresha Sekta ya Uvuvi kwa kuwawezesha wavuvi wadogo wakiwemo wanawake ili waweze kunufaika na rasilimali za uvuvi zilizopo nchini.
Aliyasema hayo wakati wa
hafla ya mashindano ya mbio za kuendesha mitumbwi kwa wavuvi wanawake kutoka
mikoa ya Kanda ya ziwa iliyofanyika jijini Mwanza Machi 6, 2022.
“ Tumedhamiria kuwainua
wavuvi wadogo na ndio maana tumeandaa mwongozo wa hiari na mpango mkakati kwa
ajili ya kuendeleza uvuvi, rasilimali na mazao yake hapa nchini,” alisema
Bulayi
Alisema lengo la Serikali
la kuandaa Mwongozo huo kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Kilimo na
Chakula Duniani (FAO) ni kukuza mchango wa sekta ya uvuvi mdogo kwa maslahi
mapana ya wananchi kiuchumi, kijamii na kimazingira.
Aliongeza kwa kusema kuwa
mwongozo huo ambao umekubaliwa na Jumuiya ya Kimataifa, unaamsha misingi ya kusimamia na kuendeleza uvuvi
mdogo kwa sababu asilimia 85 ya shughuli za uvuvi hapa nchini zinafanywa na
wananchi wenye kipato cha chini.
Alifafanua kwamba Serikali
inataka kuwainua wavuvi wadogo kwa kuwawezesha mikopo na kuwapatia
mafunzo ili waweze kufanya uvuvi wenye tija kupitia vikundi vyao vya
uvuvi na ushirika.
Kwa upande wake mwakilishi
wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), Bw. Charles Tulahi aliishukuru
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) kwa kuwapa fursa
ya kushiriki kwenye maandalizi ya mwongozo wa hiari wa kitaifa wa kutambua na
kuendeleza rasilimali za Uvuvi na kwamba
hatua hiyo itasaidia katika kuboresha lishe na
ajira kwa jamii.
"Ni Imani yetu kuwa
mpango kabambe huo wa Uvuvi utaleta mabadiliko makubwa katika Sekta ya Uvuvi
Nchini hasa kwa wavuvi wadogo wanawake ", alisema
"Tumeshirikiana na
Serikali ya Tanzania kuhakikisha mazingira ya mvuvi mdogo wa Tanzania yanakuwa
bora zaidi kwa ajili ya kupata kipato lakini pia ustawi wa maisha yao"
aliongeza
Alifafanua kuwa Shirika la
Chakula na Kilimo Duniani (FAO) limeipatia Tanzania kiasi cha shilingi milioni
450 zilizotumika kuandaa mwongozo na shughuli za utawala katika kipindi cha
miaka mitatu iliyopita.
Naye, Mkurugenzi wa Shirika
lisilo la kiserikali la EMEDO, Bi. Editrudith Lukanga alisema mchango wa
mwanamke katika uvuvi ni mkubwa lakini bado mchango huo haujatambuliwa
kikamilifu.
Aidha, aliishukuru Serikali
kwa kuandaa Mwongozo huo ambao utawasaidia wanawake wavuvi kutambuliwa kwenye
shughuli zao za uvuvi kwa kufanya uvuvi wenye tija utakaowaongezea kipato,
ajira na lishe.
Washiriki wanawake wakiwa kwenye zoezi la kushindana kuendesha
mitumbwi ziwa victoria Jijini Mwanza. Machi 06, 2022. lengo likiwa ni
pamoja na kuamasisha wanawake kushiriki katika zoezi la Uvuvi.
Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi,
Bw. Emmanuel Bulayi (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa
mashindano ya wanawake ya kuendesha mitumbwi na maafisa kutoka Shirika la
Chakula na Kilimo Duniani (FAO), EMEDO na maafisa kutoka Wizara ya Mifugo na
Uvuvi mara baada ya mashindano hayo yaliyofanyika ziwa victoria kamanga
Jijini Mwanza. Machi 06, 2022.
Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw.
Emmanuel Bulayi (wa pili kutoka kushoto) akikabidhi zawadi ya fedha kiasi cha
shilingi laki saba kwa washindi wa kwanza wa mashindano ya kupiga kasia kwa
wanawake mara baada ya mashindano hayo yaliyofanyika ziwa Victoria
kamanga Mkoani mwanza Machi 06, 2022.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni