Nav bar

Alhamisi, 10 Machi 2022

ULINZI WA RASILIMALI ZA UVUVI KUSTAWISHA UCHUMI WA BULUU - ULEGA

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewataka wataalam, wavuvi na wafugaji wa viumbe maji kulinda rasilimali za uvuvi ili kustawisha uchumi wa buluu.

Naibu Waziri Ulega ametoa kauli hiyo (07.03.2022) wakati alipokuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa mwaka wa kimataifa wa uvuvi mdogo na ukuzaji viumbe maji – IYAFA 2022 uliofanyika kwenye uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza.

Amesema upo umuhimu wa kuanzisha chombo cha ulinzi wa rasiliamli za uvuvi chenye wataalam wa uvuvi na ulinzi ili kuhakikisha rasilimali hizo zinalindwa.

Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan imeweka malengo ya kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinalindwa ili kustawisha uchumi wa buluu utakaosaidia kukuza pato la wavuvi, wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi na taifa kwa ujumla.

Serikali kwa muda mrefu imekuwa ikisikia changamoto nyingi zinazowakabili wavuvi na rasilimali za uvuvi na kwamba sasa ni wakati muafaka wa kukabiliana na changamoto hizo.Hivyo aliwataka watumishi wa Wizara kwa  kushirikiana na  Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) ili waone ni namna gani wanaweza kusaidia sekta ya uvuvi kwa baadhi ya maeneo hususani changamoto zinazowakabili wavuvi wadogo nchini.

Naibu Waziri Ulega aliwataka wataalam wa Sekta ya Uvuvi kushirikiana na wawakilishi wa FAO kuandaa mradi kwa ajili ya matumizi bora ya Ziwa Victoria utakaosaidia katika kuepusha migogoro na wavuvi na utakaolinda rasilimali za uvuvi. Lakini pia wataalam waandae mradi utakaosaidia katika kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi kwa kuwa bado ipo changamoto ya upotevu wa mazao hayo.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa FAO hapa nchini, Charles Tulahi alisema Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limetangaza mwaka 2022 kuwa ni mwaka wa uvuvi mdogo na ufugaji viumbe maji kutokana na mchango mkubwa ambao sekta za uvuvi na ufugaji wa viumbe maji zinatoa katika kuimarisha lishe, kutokomeza umaskini na katika kuongeza ajira.

FAO imepewa jukumu la kuongoza maadhimisha ya mwaka huu wa uvuvi mdogo na ufugaji wa viumbe maji kwa kushirikiana na serikali mbalimbali duniani, mashirika pamoja na vyombo muhimu kwa wavuvi. Tulahi ameipongeza Tanzania kwa kuwa na Mpango kazi wa Kitaifa wa utekelezaji wa miongozo ya uvuvi nchini.

Kabla ya kuzindua maadhimisho hayo, Naibu Waziri Ulega alitembelea mwalo wa Kirumba ambapo aliwaeleza wavuvi kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan imepanga kuhakikisha tozo zote kichefuchefu zinaondolewa ili wavuvi na wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi waweze kufanya shughuli zao kwa uhuru na tija zaidi.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akiongea na wavuvi wadogo (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa mwaka wa kimataifa wa uvuvi mdogo na ukuzaji viumbe maji 2022 kwenye uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza, Machi 07, 2022. Mhe. Ulega amesema uvuvi ni kazi kama zilivyo kazi nyingine hivyo amewataka wataalam kufanya kazi zaidi ili kuiheshimisha kazi hiyo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Mwakilishi Msaidizi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Bw. Charles Tulaki (kulia) mara baada ya uzinduzi wa mwaka wa kimataifa wa uvuvi mdogo na ukuzaji viumbe maji 2022 uliofanyika kwenye uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza, Machi 07, 2022. Katikati ni Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi.

Mwakilishi wa wafugaji viumbe maji, Mhe. Said Sadiki akiongea na hadhara ya wavuvi walioshiriki kwenye uzinduzi wa mwaka wa kimataifa wa uvuvi mdogo na ukuzaji viumbe maji 2022 ambapo amesema kuwa ufugaji wa samaki una faida kubwa endapo wafugaji hao watafuata maelekezo wanayopewa na wataalam, Machi 07,2022

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (wa tatu kutoka kushoto) akipata maelezo kutoka kwa mvuvi, Bi. Elizabeth Mpuya (wa tatu kutoka kulia) wakati alipokuwa anatembelea mabanda ya baadhi ya wavuvi kwenye uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza, Machi 07, 2022. Wa pili kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi.

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (wa nne kutoka kushoto waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki mara baada ya kuzindua maadhimisho ya mwaka wa kimataifa wa uvuvi mdogo na ukuzaji viumbe maji 2022 kwenye uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza, Machi 07, 2022.

 Hakuna maoni:

Chapisha Maoni