Na Mbaraka Kambona, Lindi
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewataka Wataalam na Watendaji wa Serikali katika
Mikoa ya Lindi na Mtwara kuwahamasisha Wananchi kutumia fursa zilizopo katika
Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi hususan ufugaji wa Majongoo Bahari, Kaa na Ukulima wa Mwani ili
waweze kukuza kipato chao.
Naibu Waziri Ulega alitoa
agizo hilo katika kikao kazi cha mkakati wa Kampeni ya Kuhamasisha Shughuli za
Ukuzaji Viumbe Maji Bahari kwa Wataalam wa Mikoa ya Lindi na Mtwara
kilichofanyika Mkoani Lindi Februari 28, 2022.
"Uchumi wa buluu ni
moja ya vipaumbele vya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake ya Awamu
ya Sita, lakini namna gani tumetumia fursa hizo kulingana na uhitaji wa soko
ili kuwainua watu katika uchumi wao na Taifa letu ndio kazi yetu sisi wataalam
tuliopo hapa", alisema Mhe. Ulega
Alisema kuwa wataalam hao
kuanzia Maafisa Ardhi, Maafisa Maendeleo na Ushirika, Maafisa Uvuvi na Maafisa
Biashara wakishirikiana vyema watakuwa na mchango mkubwa katika kuwainua watu
kiuchumi kupitia Rasilimali Bahari.
Aliongeza kwa kusema kuwa
uchumi wa buluu una fursa kubwa ya biashara, hivyo ni lazima maafisa hao waweze
kuwasaidia wananchi kuwaonesha fursa zinazopatikana humo ili waweze kuzalisha
kwa wingi na kupelekea katika masoko makubwa na kukuza kipato chao.
Aidha, aliongeza kwa
kuwataka wataalam hao kujipanga vyema na kwenda kuwajengea uwezo na
kuwahamasisha Wananchi kutumia fursa hizo huku akifafanua kuwa wananchi
wachache wakielewa fursa hizo kutashawishi watu wengi zaidi kuingia katika
shughuli hizo.
"Ninaamini sisi
Wataalam tukiwa na utayari wa kuwasaidia hawa wananchi kutumia fursa hizi
vizuri basi tutaweza kuwaondoa katika hali ya uduni na wakawa na kipato cha
uhakika", alisisitiza
Kuhusu mikakati ya Serikali
kukuza Sekta ya Uvuvi ukanda wa kusini, Mhe. Ulega alisema katika Wilaya ya
Kilwa Masoko panajengwa bandari kubwa ya Uvuvi itakayotoa fursa nyingi za
kujiongezea kipato wananchi lakini fursa
hizo zote ili ziweze kuwa na tija ni muhimu timu ya wataalam hao ikapanga na
kuwa na dhamira ya dhati ya kusaidia wananchi kunufaika na fursa hizo.
"Kwa kuanzia ni lazima
muunde vikundi vya ushirika ambavyo vitakuwa na watu walio tayari ili Serikali
itakapoleta pesa za kuwasaidia ikute vikundi hivyo vipo tayari",
alifafanua
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiongea na Wataalam na Watendaji wa Serikali wa
Mkoa wa Lindi na Mtwara wakati akifungua kikao kazi cha mkakati wa Kampeni ya
Kuhamasisha Shughuli za Ukuzaji Viumbe Maji Bahari kwa Wataalam wa Mikoa ya
Lindi na Mtwara kilichofanyika Mkoani Lindi Februari 28, 2022.
Mkuu wa Wilaya ya Lindi,
Mhe. Shaibu Ndemanga akitoa taarifa ya Mkoa kwa Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kutoka kushoto) katika kikao kazi cha mkakati wa Kampeni ya
Kuhamasisha Shughuli za Ukuzaji Viumbe Maji Bahari kwa Wataalam wa Mikoa ya
Lindi na Mtwara kilichofanyika Mkoani Lindi Februari 28, 2022. Katika kikao
kazi hicho Mhe. Ndemanga alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab
Telack.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni