Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega ameziagiza Halmashauri za Wilaya hususan zilizopo katika Ukanda wa
Pwani ya Bahari ya Hindi kutoa asilimia 10 zinazotengwa na Serikali kwa ajili
ya kuwezesha vijana na kuwapa vikundi vya ushirika vya Wafugaji jongoo bahari,
kaa na Wakulima wa Mwani ili waweze kuongeza nguvu na kuendeleza shughuli zao
za uzalishaji.
Ulega alitoa maelekezo hayo
alipokuwa akiongea kwa nyakati tofauti na kikundi cha ufugaji jongoo bahari na
kikundi cha wakulima wa mwani alipowatembelea kukagua shughuli wanazofanya
Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani Februari 25, 2022.
Wakati akiongea na
wanavikundi hao, Naibu Waziri Ulega alitumia nafasi hiyo kufikisha ujumbe kwa
Wakurugenzi wa Halmashauri kupitia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Bagamoyo, Bw. Shauri Selenda kuwa asilimia 10 zinazotengwa na Serikali kwa
ajili ya kuwezesha vijana wapewe
wanavikundi hao wanaofuga jongoo bahari, kaa na kilimo cha Mwani ili waweze
kufanya uzalishaji mkubwa na wenye tija.
“Tunataka hii Pwani yetu
yote kuanzia Moa kule Tanga Mpaka Msimbati itumike kwa ajili ya shughuli za
uzalishaji, vijana na kina mama wawezeshwe kufanya shughuli hizi ili kuvutia
watu wengine kufanya shughuli hizi na kuzalisha kwa tija zaidi”, alisisitiza
Mhe. Ulega
Alisema lengo la kuwezesha
vikundi hivyo ni kutaka wakue ili watoke katika uzalishaji mdogo na kuwa Kampuni
na kuzalisha kwa wingi kitendo ambacho kitawaongezea kipato wao na taifa kwa
ujumla.
“Haya mambo mnayofanya ya
uzalishaji yameandikwa katika ilani ya Chama cha Mapinduzi, na hizo pesa
tunazosema zitolewe ni utekelezaji wake chini ya maono ya Rais Samia Suluhu
Hassan”, alifafanua
Aidha, Mhe. Ulega aliutaka
uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kutembelea vikundi
hivyo ili kujua changamoto zao na kuwaelekeza namna ya kufanya ili waweze
kukopeshwa na benki hiyo.
“Lakini natoa maelekezo pia
kwa watu wa benki ya kilimo, mtembelee hivi vikundi mpange vizuri na
muwaongezee nguvu ili wapate mavuno ya uhakika, wewe Afisa Biashara kutoka
Benki ya TADB, nakupa wiki moja urudi hapa ukutane na hawa wanavikundi, uweke
nao mikakati na uwaelekeze namna ya kufanya ili waweze kupata hiyo
mikopo”,alisema
Pamoja na hayo, aliwahimiza
vijana kuendelea kuchangamkia fursa hizo za ufugaji wa majongoo bahari na
ukulima wa mwani kwa sababu soko biashara hiyo ina manufaa makubwa na soko pana
ambalo sio rahisi kulikidhi.
Katika hatua nyingine, Mhe.
Ulega pia kuvipongeza vyombo vya habari kwa kazi nzuri wanayofanya ya kutangaza
vyema fursa mbalimbali zinazopatikana katika uchumi wa buluu na hivyo
aliendelea kuwaomba kuendelea na kazi hiyo ya kutangaza fursa hizo zinazopatikana
nchini ili ziweze kuvutia wawekezaji wengi zaidi.
Lengo la ziara yake Mkoani
Pwani ni kutathmini na kufanya kikao kazi cha kuweka Mikakati na kampeni ya
kuhamasisha kutumia ipasavyo fursa za uchumi wa buluu huku akisisitiza kuwa baada ya miezi 3 atarejea tena katika
maeneo hayo ili kufanya ufuatiliaji wa maelekezo hayo.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiongea na Wanakikundi wa Kilimo cha Mwani
kilichopo Kijiji cha Mlingotini, Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani Februari 25, 2022.
Mhe. Ulega alitembelea kikundi hicho ikiwa Ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya
siku mbili Mkoani Pwani ambayo lengo lake ni kutathmini na kufanya kikao kazi
cha kuweka Mikakati na kampeni ya kuhamasisha kutumia ipasavyo fursa za uchumi
wa buluu.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akiwa amemshika Jongoo Bahari
alipotembelea Kikundi cha kuzalisha Majongoo Bahari cha Kaole kilichopo
Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani Februari 25, 2022. Mhe. Ulega alimuelekeza
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kukiwezesha Kikundi hicho ili kiweze
kuzalisha kwa tija.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni