Nav bar

Jumatano, 2 Machi 2022

RAIS SAMIA KUWAINUA WANANCHI KUPITIA UCHUMI WA BULUU-ULEGA


Na Mbaraka Kambona, Lindi

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amejipanga kuwainua wananchi kupitia fursa zinazopatikana katika Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi ili waweze kukuza kipato chao na kuchangia katika pato la taifa.

Ulega alitoa kauli hiyo Machi 1, 2022 alipotembelea vikundi vya ukulima wa mwani, ufugaji samaki na Kambakochi kwa lengo la kuhamasisha wananchi kuchangamkia fursa za ukuzaji viumbe maji zilizopo katika Mkoa wa Lindi.

“Nia ya Rais wetu, Mama Samia ni kuhakikisha mnakuwa na kipato kizuri wakati wote, mzunguko wenu wa kipato uimarike kupitia fursa hizi zinazopatikana katika uchumi wa buluu, uchumi wenu ukiimarika umasikini utapungua lakini vilevile mtaweza sasa kuchangia mapato katika Halmashauri zetu na taifa kwa ujumla”,alisema Mhe. Ulega

Alisema nia ya serikali ni kutaka kuwawezesha wananchi kujiunga katika vikundi ili waweze kukopesheka kirahisi huku akimuelekeza Mtendaji Mkuu, Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Dkt. Semvua Mzighani kuhakikisha wanawasaidia vikundi vya ukuzaji viumbe maji  kwa kuwapa utaalam wa namna ya kuzalisha kwa tija  na kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao yao.

Aidha, katika ziara yake hiyo pia alizielekeza Halmashauri na Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB) kuhakikisha wanawapa maarifa ya kibiashara na kuwawezesha mitaji ili wananchi hao waweze kujikwamua kimaisha kupitia shughuli zao hizo.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack alimshukuru Mhe. Rais Samia kwa kufungua fursa za uchumi wa buluu na kusema kuwa Mkoa wa Lindi wapo tayari kuzitumia fursa hizo ili wananchi waweze kunufaika.

“Mhe. Naibu Waziri ninachotaka kukuthibitishia ni kwamba uchumi wa buluu tumeshauanza hapa mkoani Lindi na tuko tayari kwenda mbele tunachohitaji ni kuungwa mkono tu”, alisisitiza Mhe. Telack


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akitoa maelekezo kwa Mtendaji Mkuu, Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Dkt. Semvua Mzighani (kushoto)  alipotembelea vikundi vya ukulima wa mwani, ufugaji samaki na Kambakochi kwa lengo la kuhamasisha wananchi kuchangamkia fursa za ukuzaji viumbe maji zilizopo katika Mkoa wa Lindi Machi 1, 2022. 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega(katikati) akimueleza jambo Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack (kushoto) kuhusu ufugaji wa Samaki katika mabwawa walipotembelea kikundi cha ASM kinachoshughulika na ufugaji wa samaki katika mabwawa kwa kutumia maji ya hahari kilichopo Mkoani Lindi Machi 1, 2022. 

 


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akimueleza jambo Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack (wa pili kutoka kulia) kuhusu ufugaji wa Samaki katika mabwawa kwa kutumia maji ya bahari walipotembelea kikundi cha ufugaji Samaki cha ASM kilichopo mkoani Lindi Machi 1, 2022. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni