Na Saja Kigumbe
Serikali imeweka wazi kuwa
mradi wa ujenzi wa bandari ya uvuvi unatarajia kuanza muda wowote kuanzia sasa
baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu.
Bandari hiyo ambayo
inatarajiwa kujengwa Wilayani Kilwa Masoko, Mkoani Lindi inatarajiwa kuwa
chachu ya kuimarika kwa uchumi wa buluu nchini.
Hayo yalibainishwa Machi
16, 2022 Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Mafunzo ya uvuvi, Dkt. Erastus Mosha
wakati wa mkutano wa wadau uliolenga kupitia rasimu ya taarifa ya upembuzi
yakinifu wa mradi huo wa kimkakati.
Alisema bandari hiyo
itaiwezesha nchi kupata mapato kupitia
meli za uvuvi na bidhaa zinazotokana na uvuvi zitauzwa hapa ndani na nje ya nchi.
Dkt. Mosha alisema Serikali
tayari imetenga fedha za kufanikisha ujenzi huo ambao unatarajiwa kufanyika
katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa.
“Tanzania hatujawahi kuwa
na bandari ya uvuvi na hili limesababisha tumeshindwa kunufaika vya kutosha
kupitia rasilimali za uvuvi kwa maana kwamba meli kubwa zinazovua kwenye ukanda
wa uchumi wa bahari kushindwa kuja kwetu kutoa mizigo yao.
“Kutokana na mazingira hayo tumeishia kupata tozo ya
leseni ya hizo meli pekee, tukiacha mizigo yote wanayopata na shughuli zote
zinazohusu uvuvi na bandari zinaenda kufanyika katika nchi nyingine tungekuwa
na bandari, meli zingeweza kuja kwetu,” alisema Dkt. Mosha.
Kwa upande wake Kaimu
Mkurugenzi Idara ya Uvuvi Bi. Merisia Mparazo alisema utekelezaji wa mradi huo
utaiwezesha nchi kuvuna rasilimali zilizopo kwenye ukanda wa uchumi wa bahari
hususani kwenye kina kirefu.
Alisema uwepo wa bandari
hiyo utapanua wigo wa kiuchumu katika mkoa wa Lindi ambapo licha ya shughuli za
bandari utawezesha kuanzishwa kwa viwanda vya kuchakata samaki watakaovuliwa,
biashara ya mafuta ya meli na utengenezaji wa vyombo hivyo vya uvivu.
“Kama kuna bandari ya uvuvi
lazima zitakuwepo shughuli nyingine zinazoendana na hiyo, mfano zile meli
zitahitaji mafuta au marekebisho madogo madogo tunategemea huduma za aina hii
zitapatikana pale.
"Kana kwamba hiyo
haitoshi kama samaki hao wakubwa watakuja kwenye bandari yetu lazima uchakataji
utafanyika hapa nchini hivyo kutakuwa na viwanda vya kuchakata minofu ya
samaki, bado biashara ya vyakula na hoteli itachukua nafasi hivyo vyote
vitazidi kuuchangamsha mkoa mzima wa Lindi,” alisema Merisia.
Kwa upande wake mwakilishi
wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi, Bw.
Ramadhani Hatibu amesema Mkoa huo umepokea vizuri mradi huo kutokana na kuwa na
tija kwa taifa na jamii kwa ujumla.
Amesema kutokana na mradi
huo kutasaidia kuvua samaki wenye ujazo mkubwa ambao utasaidia pato la Taifa.
Naye Mdau wa uvuvi Bw.
Khalfan Shabani amesema ujenzi wa bandari hiyo ya Uvuvi utaleta maendeleo
makubwa katika Sekta ya Uvuvi.
Aidha ameiyomba Serikali
kuwakaribisha wawekezaji kwa ajili ya ujenzi wa karakana ya meli baada ya
ujenzi wa bandari kukamilika.
Mkurugenzi Msaidizi Utafiti
na Mafunzo ya uvuvi Sekta ya Uvuvi Dkt. Erastus Mosha (katikati) akiwa kwenye
picha ya pamoja na wadau wa Sekta hiyo mara baada ya kikao kifupi
kilichofanyika kwenye ukumbi wa millennium tower Jijini Dar es salaam lengo
likiwa ni pamoja na kujadili taarifa ya upembuzi yakinifu ya ujenzi wa bandari
ya Uvuvi Machi 16, 2022.
Mkurugenzi Msaidizi wa
uendelezaji wa Uendelezaji wa Rasilimali za Uvuvi (Uvuvi), Bi. Merisia Parazo
(kulia) akifungua kikao na kueleza lengo la kikao hicho kilichofanyika kwenye
ukumbi wa millennium tower Jijini Dar es salaam, Machi 16, 2022
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni