Na. Edward Kondela
Wakala ya Maabara ya
Veterinari Tanzania (TVLA) imesema katika mwaka ujao wa fedha 2022/2023
inatarajia kuongeza wigo wa kufanya vipimo vya ubora wa vyakula vya mifugo ili
kubaini aina za sumu kuvu ambazo zinaweza kusababisha madhara ya kiafya kwa
binadamu na mifugo.
Mtendaji Mkuu wa TVLA Dkt.
Stella Bitanyi amebainisha hayo ofisini kwake jijini Dar es Salaam, wakati wa
zoezi la kuhakiki ubora wa vyakula vya mifugo vinavyozalishwa hapa nchini
lililofanyika mwishoni mwa wiki, zoezi ambalo limefanywa katika wilaya za
Temeke na Ubungo na wataalamu kutoka TVLA.
Dkt. Bitanyi amesema wakala
hiyo inatarajia pia kupima mabaki ya ‘antibiotic’ na dawa nyingine za mifugo
ndani ya vyakula vya mifugo ili kuhakikisha ubora wa vyakula vya mifugo kwa
kutokuwa na mabaki ya dawa ambazo zinaweza kusababisha usugu wa dawa kwa mifugo
pamoja na binadamu atakayetumia mazao yanayotokana na mifugo hiyo.
Katika hatua nyingine
mtendaji mkuu huyo wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), ametoa
wito kwa wazalishaji wa vyakula vya mifugo nchini pamoja na wafugaji
kuhakikisha wanafikisha sampuli za vyakula katika maabara hiyo ili kupima ubora
wa chakula ambacho kinastahili kutumiwa na mifugo pamoja na malighafi ambazo
zitatumiwa katika kutengeneza vyakula hivyo.
Amebainisha kuwa matumizi
ya vyakula sahihi vya mifugo ambavyo vina virutubisho vinavyostahili,
vitamuwezesha mfugaji kufuga kwa tija kwa kuwa mifugo itakuwa katika muda
unaotakiwa kitaalamu na kufikia kiwango cha uzito unaotakiwa sokoni.
Akizungumza wakati wa zoezi
la kukagua ubora wa vyakula vya mifugo katika Wilaya za Temeke na Ubungo, Afisa
Mtafiti wa Mifugo kutoka TVLA Dkt. Evaline Mfuru amesema uwiano sawa wa
virutubisho vinavyotakiwa kwenye vyakula vya mifugo kwa kiasi kikubwa hupunguza
gharama za uzalishaji pamoja na kudhibiti magonjwa ya mifugo.
Nao baadhi ya wafugaji na
wazalishaji wa vyakula vya mifugo wamesema zoezi la uhakiki wa ubora wa vyakula
vya mifugo litakuwa na tija kwa kuhakikisha vinapatikana vyakula bora, ambavyo
vitaleta tija kwa mfugaji pamoja na kuondoa sokoni vyakula vya mifugo ambavyo
havikidhi vigezo.
Wakala ya Maabara ya
Veterinari Tanzania (TVLA) ambayo iko chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi
imekuwa ikifanya uchunguzi wa ubora wa vyakula vya mifugo ili vyakula hivyo
viwe katika viwango vinavyotakiwa kwa ajili ya matumizi ya mifugo na kuleta
tija kwa mfugaji.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya
Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi, akizungumza ofisi
kwake jijini Dar es Salaam, juu ya mipango ya TVLA katika mwaka ujao wa fedha
2022/2023 kuongeza wigo wa kufanya vipimo vya ubora wa vyakula vya mifugo ili
kubaini aina za sumu kuvu ambazo zinaweza kusababisha madhara ya usugu wa dawa
kwa binadamu na mifugo. (14.02.2022)
Kutoka kushoto ni Mkaguzi
wa Vyakula vya Mifugo kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Bi. Theodora
Baziwe, akifuatiwa na Fundi Sanifu Maabara kutoka Wakala ya Maabara ya
Veterinari Tanzania (TVLA) Bw. Henry Mlundachuma, wakizungumza na mfugaji Bw.
Erasto Mbise, walipomtembelea nyumbani kwake katika Wilaya ya Temeke Mkoani Dar
es Salaam ili kujiona shughuli za ufugaji na vyakula vya mifugo anavyotumia
ikiwa ni sehemu ya kuhakiki ubora wa vyakula vya mifugo zoezi lililofanywa
katika wilaya za Temeke na Ubungo na wataalamu kutoka TVLA. (14.02.2022)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni