Na Mbaraka Kambona, Pwani
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewahimiza Viongozi wa Mikoa iliyopo Pwani ya
Bahari ya Hindi hususan Pwani na Dar es Salaam kuhamasisha wananchi wao
kujiunga katika vikundi vya ushirika ili wawezeshwe na serikali kunufaika na
fursa zinazopatikana katika uchumi wa buluu ikiwemo ufugaji wa kaa, majongoo
bahari na kilimo cha mwani.
Ulega alitoa rai hiyo
katika kikao kazi cha mkakati wa kampeni ya kuhamasisha shughuli za ukuzaji
viumbe maji bahari kwa viongozi na wataalam wa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam
kilichofanyika Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani Februari 24, 2022.
Alisema ili wananchi waweze
kunufaika na fursa hizo, suala la kuwa na ushirika ni muhimu sana huku
akihimiza kila halmashauri kuhamasisha wananchi kujiunga katika vikundi na
kuunda ushirika katika maeneo yao.
“Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hotuba yake aliyoitoa
Januari 7, 2022 katika kilele cha Matembezi ya Miaka 58 ya Mapinduzi ya
Zanzibar alisisitiza shughuli za ukuzaji viumbe maji hususani ufugaji wa kaa
kuwa ni moja ya fursa za ajira kwa vijana”,alisema Mhe. Ulega
Alifafanua kwa kusema kuwa
Ibara ya 43 (h) ya Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inahimiza
kuanzishwa vikundi vya ushirika vya wavuvi na wafugaji viumbe maji huku
akiongeza kuwa kukuza na kuimarisha
uchumi wa buluu ni moja ya kipaumbele cha serikali ya awamu ya sita, hivyo ni
muhimu kuwaanda wananchi na fursa pana iliyopo katika tasnia ya ukuzaji viumbe
maji ili serikali inapoanza kuwawezesha wawe wako tayari.
Aidha, alisema Serikali
inatambua changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia ya Ukuzaji Viumbe Maji
katika kuzitumia fursa hizo zikiwemo mitaji midogo ya uwekezaji, upatikanaji wa
pembejeo mbalimbali na masoko ya baadhi ya mazao yatokanayo na ukuzaji viumbe
maji, katika kukabiliana na changamoto hizo,alisema, mwaka 2019, Wizara ya
Mifugo na Uvuvi ilianzisha Dawati la Sekta Binafsi ili liwe kiunganishi au
daraja kati ya Wizara, wawekezaji, masoko na taasisi za kifedha kama njia
mojawapo ya ufumbuzi wa tatizo la mitaji, masoko na vitendea kazi kwa wavuvi,
wakuzaji viumbe maji.
Lengo la ziara yake ni
kutathmini na kufanya kikao kazi cha kuweka Mikakati na kampeni ya kuhamasisha
kutumia ipasavyo fursa za uchumi wa buluu
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiongea na Viongozi na Wataalam wa Mikoa ya Pwani
na Dar es Salaam katika Kikao Kazi cha Mikakati na Kampeni ya Kuhamasisha
Shughuli za Ukuzaji Viumbe Maji Bahari kilichofanyika Wilayani Bagamoyo, Mkoani
Pwani Februari 24, 2022. Mhe. Ulega aliwahimiza Viongozi hao kuwahamasisha
Wananchi wao kuchangamkia fursa zilizopo katika uchumi wa buluu ikiwemo ufugaji wa Kaa, Majongoo Bahari, Kambakochi
na ukulima wa Mwani.
Sehemu ya Viongozi na
Wataalam wa Mikoa ya Pwani na Dar es Salaam walioshiriki katika Kikao Kazi cha
Mikakati na Kampeni ya Kuhamasisha Shughuli za Ukuzaji Viumbe Maji Bahari
kilichofanyika Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani Februari 24, 2022. Mhe. Ulega
aliwahimiza Viongozi hao kuwahamasisha Wananchi wao kuchangamkia fursa zilizopo
katika uchumi wa buluu ikiwemo ufugaji
wa Kaa, Majongoo Bahari, Kambakochi na ukulima wa Mwani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni