Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda amesisitiza watalaam wa Mifugo kufanya
kazi zao kwa Weledi ili kusaidia Sekta ya Mifugo kusonga mbele.
Hayo ameyasema leo 23 feb
2022 alipokuwa akifungua kikao cha Watalaam wa Mifugo na Uvuvi kanda za nyanda
za juu kusini na kusini Magharibi, mkoni Katavi.
"Watalaam fanyeni kazi
zenu kwa Weledi ili wafugaji hawa wafaidike na huduma zenu, kila mtalaam awe na
Register, ili mwisho wa siku aulizwe amehudumia wafugaji wangapi katika
halmashauri yake, kata au kijiji.Lakini kama hiyo haitoshi kwa mwaka fedha
2023/2024 tutakuwa na mkataba wa utendaji kazi ili kupima utendaji kazi wa
watalaam wetu" Alisema Nzunda.
Aidha, Nzunda amesema
kuwa Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kuwa
na Mifugo mingi, asilimia 1.4 ya ng'ombe wote wako Tanzania na nchi yetu ni ya pili barani Africa kwa uwingi wa Mifugo
ikitanguliwa na Ethiopia, lakini bado tija hiyo ya kuwa na mifugo mingi kiasi
hicho haionekani.
"Pamoja na kuwa
Tanzania tuna ng'ombe 33 Milioni lakini bado inachangia kiasi kidogo sana
katika pato la taifa, ni asilimia 7.1tu, tunazidiwa na Botswana yenye mifugo
Milioni mbili lakini inachangia pato la taifa
zaidi ya asilimia 20."Alisema Nzunda.
Katibu Mkuu Mifugo amesema
kuwa, sasa ni wakati mwafaka wa kufanya
mageuzi katika Sekta ya Mifugo kwa kila Mkoa wenye Mifugo/Halmashauri na kata
kuandaa Mpango mkakati wa Sekta ya mifugo ili kuutekeleza Mpango huo ili Sekta
iweze kusonga mbele na kuleta matokeo chanya na yenye tija kwa Taifa.
Pia, Bw. Nzunda amesisitiza
kuwa suala la Uogeshaji Mifugo, Uchanjaji, Utambuzi na ufuatiliaji, ulimaji wa
malisho sio suala la hiari tena,ni lazima kama tunataka mabadiliko katika
Sekta, wafugaji wabadilike na waanze kufuga kwa tija.
Katika hatua nyingine
katibu Mkuu mifugo ameweka jiwe la Msingi katika Ujenzi wa kiwanda cha
usindikaji Maziwa cha MSS-Nsimbo Mkoani Katavi.
Mmiliki wa kiwanda hicho
cha MSS-Nsimbo Bw. Marick Salum amesema kuwa kiwanda hicho kikikamilika
kitakuwa na uwezo wa kusindika Maziwa lita elfu mbili kwa saa. Pia amemwambia
katibu Mkuu Mifugo kuwa mkoa wa Katavi una ng'ombe zaidi ya elfu moja hivyo
upatikanaji wa Maziwa sio tatizo, pia uanzishwaji wa kiwanda hicho ni muhimu
kwa sababu wafugaji watapata soko la kuuzia maziwa yao.
Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda akihutubia Watalaam wa Sekta ya Mifugo
na Uvuvi(Hawapo pichani) wa kanda ya nyanda za juu kusini na kusini Magharibi
leo tarehe 23/02/2022 Mkoani Katavi.Lengo la kikao hicho ni kubadilishana
uzoefu katika utendaji kazi.Kulia ni Dkt.Samora Mshang'a,Daktari wa Mifugo
kutoka mkoa wa Mbeya,kushoto ni Dkt.Anneth Kitambi, Mkurugnzi Msaidizi huduma
za ukaguzi-Ustawi wa wanyama na utambuzi wa Mifugo.
Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda (Kushoto) akiweka jiwe la Msingi
katika Ujenzi wa Kiwanda cha kusindika Maziwa cha MSS-Nsimbo Mkoani Katavi leo
tarehe 23/02/2022.Kulia ni Bw.Marick Salum,Mmiliki wa Kiwanda cha MSS-Nsimbo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni