Na. Edward Kondela
Serikali imewataka wakulima na wafugaji wanaofanya shughuli zao kwenye maeneo wasiyoruhusiwa, kuondoka mara moja na kuwataka wafuate sheria, taratibu na kanuni za nchi ambapo wakulima na wafugaji wanatakiwa kuwa kwenye maeneo waliyotengewa kisheria bila kuingiliana.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amebainisha hayo (24.01.2021) akiwa katika Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara kutatua mgogoro wa matumizi ya ardhi uliojitokeza hivi karibuni kati ya wakulima na wafugaji katika ukanda wa malisho ya mifugo wa vijiji vya Amei, Loolera, Lesoit na Lembapuri, mgogoro ambao umesababisha kifo cha mkulima Bw. Emelian Malima miaka 45 anayedaiwa kuuwawa na wafugaji (20.01.2021) katika eneo la ukanda wa malisho ya mifugo.
Akizungumza na baadhi ya wakulima na wafugaji wanaofanya shughuli zao katika vijiji hivyo, Waziri Ndaki amesema serikali imekuwa ikitenga matumizi bora ya ardhi maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Wilaya ya Kiteto na kwamba maeneo ya wakulima yametengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo pekee na maeneo ya wafugaji yametengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo na wote wanalindwa na sheria.
“Wilaya ya Kiteto ilishatenga maeneo ya wakulima na wafugaji na maeneo hayo ya wafugaji wanakaa wafugaji na mifugo yao na maeneo ya wakulima wanakaa wakulima na kulima mazao yao, hakuna mtu anayeruhusiwa kuingilia eneo la wenzake sisi wakulima haturuhusiwi kuingilia maeneo ya wafugaji na wafugaji haturuhusiwi kuingilia maeneo ya wakulima.” Amesema Waziri Ndaki
Katika ziara hiyo ya kikazi ya siku moja Wilayani Kiteto ambayo Waziri Wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amefuatana na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Manyara ikiongozwa na mkuu wa mkoa huo Mhe. Joseph Mkirikiti, Waziri Ndaki amewataka wakulima walioingilia eneo la malisho ya mifugo katika vijiji vya Amei, Loolera, Lesoit na Lembapuri vilivyopo kata za Loolera na Lengatei na kufanya shughuli za kilimo watoke eneo hilo kwa kuwa wanachangia migogoro inayotokana na wakulima hao kuingilia eneo la malisho.
Kuhusu kifo cha mkulima Bw. Emelian Malima miaka 45 anayedaiwa kuuwawa na wafugaji katika eneo hilo la malisho, Waziri Ndaki ametaka tukio hilo liwe la kwanza na mwisho na kumhakikisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kuwa Wilaya ya Kiteto iko salama na itaendelea kuwa salama.
“Hicho kifo tulichokisikia ni cha kwanza na mwisho hatutamtetea mtu na ndiyo maana watuhumiwa wa tukio hilo wamekamatwa na mahakama itatenda haki pia ninamhakikishia Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa aliyenielekeza kuja hapa kuwa Wilaya ya Kiteto iko salama.” Amesema Mhe. Ndaki
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Joseph Mkirikiti amewataka wakulima kuheshimu amri ya mahakama kwa kuacha kulima kwenye ukanda wa malisho katika Wilaya ya Kiteto, kwa kuwa wamekuwa wakirudi na kukutwa na hatia huku wakiiomba mahakama kuwaruhusu waondoke baada ya kuvuna jambo ambalo limekuwa likijirudia mara kwa mara.
Aidha, amesema uongozi wa kijiji ndiyo wenye mamlaka kupitia mkutano mkuu kugawa maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali yakiwemo ya kilimo na kubainisha amekuwa akipewa taarifa na baadhi ya wakulima kuwa wamegaiwa maeneo na wenyeviti wa vijiji ambao wamekuwa hawafuati utaratibu ambapo Mhe. Mkirikiti amewataka watu wote ambao wamepewa maeneo ya kilimo kinyume na utaratibu kufika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kiteto ili kujua hatma yao na kutaka viongozi waliohusika kuchukuliwa hatua za kisheria.
Pia, amepiga marufuku baadhi ya watu ambao wamekuwa wakifanya shughuli za uwakala wa ardhi katika Wilaya ya Kiteto na kuwauzia watu wanaotoka nje ya wilaya hiyo maeneo ya malisho ya mifugo kwa kuwadanganya kuwa ni maeneo ya kilimo.
Baadhi ya wananchi waliopatiwa nafasi kuzungumza katika mkutano huo wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki, Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Joseph Mkirikiti na wananchi wanaofanya shughuli zao katika ukanda wa malisho Wilayani Kiteto, wamesema mgogoro uliojitokeza kati ya wakulima na wafugaji unatokana na ukinzani wa baadhi ya vijiji kuingiliana na kila kijiji kuainisha matumizi tofauti ya ardhi ya kijiji.
Katika kuhakikisha wanaendeleza shughuli za kilimo Katika Wilaya ya Kiteto, uongozi wa Mkoa wa Manyara na wilaya hiyo umeainisha nia yao ya kuwatafutia maeneo ya kilimo na kuacha kufanya shughuli za kilimo katika ukanda wa malisho ya mifugo kwenye vijiji vya Amei, Loolera, Lesoit na Lembapuri vilivyopo Kata za Loolera na Lengatei.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (aliyenyoosha mkono) akiwa katika eneo ambalo inadaiwa wafugaji walimuua Bw. Emelian Malima miaka 45 ambaye alikuwa akifanya shughuli za kilimo katika ukanda wa malisho ya mifugo katika Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, ambapo Waziri Ndaki amechukizwa na kitendo hicho cha wananchi kujichukulia sheria mkononi na kutaka iwe mwanzo na mwisho. (24.01.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni