Na Mbaraka Kambona,
Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul ameitaka Wakala ya Elimu na Mafunzo ya
Uvuvi (FETA) kuongeza kasi ya kuzalisha Wataalam watakaokuwa na uwezo wa
kuendesha Meli za uvuvi wa bahari kuu zitakazonunuliwa na Serikali ili kuongeza
ajira na kukuza uchumi wa nchi kupitia uchumi wa bluu.
Gekul
alitoa kauli hiyo alipofanya ziara katika ofisi za Wakala hiyo zilizopo
Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani mwishoni mwa wiki.
Alisema
kuwa mpango wa serikali katika miaka hii mitano chini ya uongozi wa Rais, Dkt.
John Pombe Magufuli ni kununua meli nane zitakazotumika kwenye shughuli za
uvuvi wa bahari kuu, hivyo ni muhimu kuongeza kasi ya kutoa wataalam ambao wataweza
kuziendesha meli hizo pindi zitakapofika.
Aliongeza
kuwa mwishoni mwa mwaka huu meli ya kwanza itakuja, huku akisema kuwa
haitapendeza kama vyombo hivyo vitakuja halafu pasiwepo na vijana watakaohusika
na kuviendesha.
“Nchi
inawategemea mtoe wataalam watakaosaidia kuendesha meli hizo zitakazoletwa kwa
ajili ya uvuvi wa bahari kuu, tunaomba mkatuzalishie wataalam ambao hatutapata
upungufu wa wataalam wa kuendesha vyombo hivyo,” alisema Gekul
Awali
akimkaribisha Naibu Waziri, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Wakala ya Elimu na
Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Dkt. Semvua Mzighani alisema kuwa wameshaingia mkataba
wa maridhiano wa viwango vya mafunzo na utoaji vyeti kwa wafanyakazi wa vyombo
vya uvuvi wa mwaka 1995 na hivyo itasaidia kuweza kutoa vyeti kwa Manahodha wa
Meli, Maafisa wa Meli, Mabaharia na Waangalizi wa Meli zitakazofanyakazi katika
uvuvi wa bahari kuu.
“Huwezi
kuajiriwa kule kama hauna cheti cha kukutambulisha, hivyo kupitia maridhiano
haya sasa Mabahari watapatikana kutoka katika chuo hiki,” alisema Dkt. Mzighani
Dkt.
Mzighani aliongeza kuwa kwa Afrika vyuo vinavyotoa mafunzo kwa Wataalam hao
vipo Afrika ya Kusini na Misri, huku akisema ni wakati mzuri sasa kupitia
mafunzo yatakayotolewa hapa nchini kuongeza ajira kwa vijana na kupata fedha za
kigeni kupitia watu kutoka nchi nyingine watakaokuja kusoma katika chuo hicho.
Aidha,
Dkt. Mzighani alisema pamoja na mipango na mikakati mizuri waliyonayo katika
kuboresha huduma zao bado wanakabiliana na changamoto kubwa ya gharama za
uendeshaji wa vyuo vya uvuvi, hivyo ameiomba serikali iwaongezee nguvu ili
waweze kutoa wataalam wazuri watakaokwenda kulisaidia Taifa kukuza na
kuimarisha uchumi wa bluu.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul akiwapa chakula Samaki alipotembelea Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Kampasi ya Mbegani iliyopo Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani mwishoni mwa wiki. Kulia kwake ni Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Wakala hiyo, Dkt. Semvua Mzighani.
Kaimu
Afisa Mtendaji Mkuu, Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Dkt. Semvua
Mzighani (kushoto) akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline
Gekul (kulia) alipotembelea Wakala hiyo iliyopo Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani
mwishoni mwa wiki.
Nahodha
Mkuu, Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Kampasi ya Mbegani, Nikasi
Mbandi (kulia) akimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul
ramani inayoonesha maeneo ya uvuvi na kina chake katika Bahari ya Hindi
alipotembelea Wakala hiyo iliyopo Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani mwishoni mwa
wiki.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni