Nav bar

Jumamosi, 9 Januari 2021

GEKUL AMPA MKURUGENZI ILALA SIKU 7 KUMLIPA MKANDARASI

Na Mbaraka Kambona,

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kuhakikisha kuwa ndani ya siku 7 anamlipa Mkandarasi anayejenga Machinjio ya Vingunguti shilingi bilioni 5 anazodai ili aweze kukamilisha ujenzi huo.

 

Gekul alitoa agizo hilo alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa machinjio hayo yaliyopo jijini Dar es Salaam Januari 8, 2021.

 

Alisema kuwa hali za machinjio nyingi kwa sasa sio nzuri, Wanyama wanachinjwa katika mazingira machafu na sio salama kwa walaji huku akisema machinjio hayo ya Vingunguti yatakuwa mkombozi kwa wananchi wa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla.

 

“Kwa hiyo Mkurugenzi hakikisha ndani ya siku 7 kuanzia leo tarehe 8 unamlipa Mkandarasi ili kazi hii ikamilike kama ambavyo Mhe. Rais, Dkt. John Magufuli alivyoagiza,” aliagiza Gekul

 

Gekul aliendelea kusisitiza kuwa kukamilika kwa ujenzi huo ni lazima uende sambamba na ununuzi wa magari kwa ajili ya kubebea nyama na kuzisambaza katika mabucha yaliyopo jijini Dar es Salaam kwani haitapendeza kuwepo kwa machinjio hayo mazuri halafu nyama ziwe zinabebwa kwenye pikipiki.

 

Aliongeza kuwa ili kuhakikisha machinjio hayo yanapata Wanyama wazuri na salama kwa ajili ya walaji, wataboresha mnada wa machinjio ya Pugu ili wanyama watakaokuwa wanapelekwa hapo wawe na viwango vya kuchakatwa katika machinjio hayo.

 

Aidha, aliwapongeza Mkurugenzi na Mkandarasi kwa jitihada kubwa wanazozifanya katika kukamilisha ujenzi huo na kuwataka kuongeza kasi ya ujenzi ili ukamilike kama inavyotarajiwa.

 

Naye, Msimamizi wa ujenzi huo kutoka Shirika la Nyumba la Taifa, Mhandisi, Efraim Phanuel alisema kuwa endapo watalipwa kiasi hicho cha pesa wanachodai kama alivyoagiza Naibu Waziri watakamilisha ujenzi huo mapema mwezi wa pili mwaka huu.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul (katikati) akikagua risiti ya mteja aliyemkuta akitoka na mbuzi katika mnada wa Pugu uliopo jijini Dar es Salaam alipotembelea mnada huyo Januari 8, 2021. Kulia ni Kaimu Msajili, Bodi ya Nyama, Imani Sichwale.


Mhandisi Efraim Phanuel akimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul michoro inayoonesha muonekano wa  machinjio ya Vingunguti utakavyokuwa baada ya kukamilika kwake alipotembelea machinjio hayo Januari 8, 2021.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) akimsikiliza Msimamizi wa Ujenzi wa Machinjio ya Vingunguti, Mhandisi EfraimPhanuel (hayupo pichani) alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa machinjio hayo Januari 8, 2021. Kulia ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Jumanne Shauri.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni