Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah
Ulega amewataka wafanyabiashara wanaouza nyama nchini kutopandisha bei ya nyama
kipindi hiki cha sikukuu ya Eid El Fitr ili kuhakikisha kila mwananchi
anapata kitoweo hicho.
Akizungumza (18.05.2020) jijini Dar es
Salaam, Naibu Waziri Mhe.Ulega amemtaka pia Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala,
Bw. Jumanne Shauri ndani ya siku saba kuhakikisha wanawapeleka wafanyabiashara
wanaofanya biashara katika machinjio ya vingunguti kujionea eneo jipya
lililotengewa na Manispaa ya ilala.
Mhe. Ulega amebainisha hayo wakati akikagua
ujenzi wa mradi wa machinjio ya kisasa katika eneo la vingunguti katika
Manispaa ya Ilala, ambapo amesisitiza wafanyabiashara wa nyama wanapaswa kuuza
nyama kwa bei ya kawaida kulingana na hali ilivyo ili kuhakikisha watu wote
wanapata kitoweo hicho.
Aidha amesema imekuwa ni kawaida kwa
wafanyabiashara wa Nyama kupandisha bei kipindi cha sikukuu kinapofika hali
inayosababisha wananchi kutopata nyama kulingana na bei kuwa juu.
"Serikali ya awamu ya tano inatengeneza
uchumi endelevu hivyo katika kuhakikisha hili wafanyabiashara wa nyama
wanatakiwa kuchangamkia fursa ya sikukuu ya Eid El kuuza nyama kwa bei ya
kawaida na sio ya kuwaumiza wananchi," amesema Mhe. Ulega.
Kuhusu mradi wa machinjio ya kisasa ya
vingunguti ambapo hadi sasa umefikia asilimia 85 ya ukamilikaji wake, Mhe.
Ulega amesema mradi huo unaogharimu kiasi cha Sh.Billioni 12.4 ambao unalengo
la kuhakikisha wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam, mikoa mingine na nchi za nje
kupata nyama itakayokuwa bora na yenye kuandaliwa vizuri kutokana na jengo
hilo.
"Wizara yangu ndiyo inashughulikia
masuala ya mifugo natoa pongezi kwa serikali kwa hatua hii ya kufikisha jengo
hili katika kiwango cha juu kwani kiwanda pekee kinachotusaidia kwa sasa kipo
Mwanza, Chobo Investmest hivyo kupitia kiwanda hiki naamini tutaongeza nguvu
katika uuzaji wa nyama." Ameongeza Mhe. Ulega
Hata hivyo Mhe. Ulega amesema uwekezaji wa
mradi huu utailipa serikali katika hatua zote ikiwemo kiuchumi na kijamii pindi
shughuli za mnada zitakapoanza kufanyika katika jengo hilo.
Naibu waziri huyo amesema Tanzania bado ina
fursa nyingi katika mifugo na serikali tayari ina mikakati mizuri ya
kuhakikisha sekta hii inazidi kukua siku hadi siku na kutoagiza nyama nje ya
nchi.
"Bado tuna fursa nyingi katika
kuhakikisha nyama inapatikana kwa wingi na tutaacha ununuaji wa nje ya nchi
pindi mradi huu utakapokamilika na tutahakikisha sisi ndio tunawapelekea watu
wa nchi nyingine" amesema Mhe. Ulega
Amesema eneo hilo litachinja ng'ombe takriban
1,500 na mbuzi 1000 kwa siku moja pindi itakapokamilika hivyo upandishaji
holela wa bei ya nyama kwa vipindi vya sikukuu hautakuwepo tena kutokana na
nyama kupatikana kwa urahisi zaidi.
Pia amesema kwa wafanyabiashara wa machinjio
hayo wanaofanya biashara, tayari wamepatiwa eneo ambalo watajengewa na kufanya
shughuli zao karibu na eneo hilo kama kawaida.
"Najua kuna watu wanajiuliza kuhusu
wakinamama na vijana wanaofanya kazi hapa, Manispaa ya Ilala imeshawatafutia
eneo na ni zuri lipo karibu na machinjio haya ya kisasa litawapa fursa ya
kuendelea kufanya shughuli zenu, ninamuagiza Mkurugenzi wa Manispaa kuwapeleka
wafanyabiashara na kuliona hilo eneo." amesema Ulega
Wakati huo huo Mhe. Ulega amempongeza Rais
Dkt. John Magufuli kwa hotuba yake aliyotoa juzi ambapo wafugaji na wavuvi
wamempongeza kwani bila kutoka kwao hawawezi kupata kipato.
Pia amesema maono ya Rais Magufuli ni ya
kizalendo, Kiutu na kuwainua wananchi wake hivyo watendaji katika nyanja
mbalimbali wanapaswa kutomuangusha ili kuifikisha nchi katika uchumi wa juu.
Kwa Upande wake Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama
nchini, Bw. Imani Sichalwe amesema kupitia mradi huo wafugaji watapata masoko
makubwa na kutoingiliwa na madalali ambao kwa asilimia kubwa walikuwa
wanawapunja.
Amesema ni wakati wa wafugaji kujipanga na
kuanza kufuga kisasa kwa kuongeza ubora na kuwaongezea thamani mifugo yao.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah
Ulega (kushoto) atembelea machinjio mpya inayojengwa Vingunguti Wilaya ya Ilala
Mkoani Dar es salaam.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni