Wizara ya Mifugo na Uvuvi
imeitaka Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO) kubadilika na kufanya shughuli zake
kwa tija ili iweze kunufaika na rasilimali ardhi na mifugo inayomiliki.
Akizungumza wakati
akitembelea na kujionea shughuli zinazofanywa katika ranchi za Ruvu iliyopo Mkoani
Pwani na Mkata iliyopo Mkoani Morogoro jana (01.07.2019), Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amezitaka
ranchi hizo zilizo chini ya NARCO kuhakikisha zinatumia vitu ardhi inazomiliki
ili kufuga mifugo itakayoongeza tija kwa taifa.
Prof. Gariel akiwa katika
Ranchi ya Ruvu amemuelekeza meneja wa ranchi hiyo Bw. Elisa Binamungu kuhakikisha
ranchi hiyo inafuatilia pia madeni yote inayodai ili iweze kupata fedha na
kujiendesha kwa kutumia fursa zilizopo za kuuza kwa tija mazao ya mifugo
ikiwemo nyama na maziwa.
“Lengo la ziara yangu ni
kuhakikisha mnatekeleza agizo alilolitoa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga
Mpina June 15 mwaka huu, alipokutana na viongozi wa NARCO la kuwataka
kubadilika kiutendaji na muweze kunufaika na ardhi na mifugo mnayomiliki hali
kadhalika kuweza kutoa gawio serikalini.” Alisema Prof. Gabriel.
Akiwa katika Ranchi ya Mkata
Prof. Gabriel amejionea ujenzi wa kisima kwa ajili ya kupata maji ya kunyweshea
mifugo na kumuagiza meneja wa ranchi hiyo Bw. Iddy Athuman kuhakikisha kisima
hicho kinakamilika katika mwaka wa fedha 2019/2020 kwa kuwa ranchi hiyo imekuwa
ikikabiliwa na changamoto ya maji kwa mifugo.
“Ni muhimu kisima hiki
kikamilike kwa kuwa maji ni uchumi mtakapokuwa na maji mengi ndivyo mtakavyoweza
kuwa na mifugo kulingana na uwepo wa maji, pia kuhusu wazo lenu la kuanza
kufuga ng’ombe wa maziwa ni wazo zuri hususan kisima hiki kikianza kutumika na
kuwa na maji ya kutosha.” Alifafanua Prof. Gabriel.
Wakiwa katika ranchi
wanazozisimamia mameneja hao wamesema watatekeleza maagizo yote kwa wakati kama
yalivyoelekezwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina ili ranchi hizo za
Ruvu na Mkata ziweze kunufaika kupitia rasilimali ardhi na mifugo zinazomiliki.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo)
Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa
Ranchi ya Mkata mara baada ya kutembelea ranchi za Ruvu na Mkata kujionea
utendaji kazi wa ranchi hizo. (01.07.2019)
|
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa na Meneja wa Ranchi ya Ruvu Bw. Elisa Binamungu (Picha ya kwanza juu) na Meneja wa Ranchi ya Mkata Bw. Iddy Athuman (Picha ya kwanza chini) wakati alipotembelea ranchi hizo na kujionea shughuli mbalimbali wanazofanya. (01.07.2019)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni