Serikali imesema wadaiwa wote
waliowekeza katika ranchi za taifa zinazomilikiwa na Kampuni ya Ranchi ya Taifa
(NARCO) walipe madeni yao kabla haijachukua hatua ya kuwanyang’anya maeneo na kuwafikisha
mahakamani.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema hayo jijini
Dodoma katika ofisi za makao makuu ya NARCO wakati akizungumza na wawekezaji waliopatiwa
vitalu 111 katika ranchi za taifa zilizopo maeneo mbalimbali nchini kwa ajili
ya kulisha mifugo yao ambapo hadi sasa wanadaiwa Tshs Bilioni Saba.
“Lipeni bila shuruti, ahadi
yangu kwenu mkifanya majukumu yenu ofisi yangu itawapatia ushirikiano wa kutosha,
kama mheshimiwa rais akiendelea kuniacha hapa katika wizara hii wale ambao
hawalipi watakuwa wamepoteza sifa za kuwa wawekezaji na siyo kwamba itaishia hapo
tutachukua hatua za kisheria na watalipa deni ili kusudi watanzania wengine
wawekeze ambao wanaweza kulipa hela ya serikali, hulipi nitakuondoa tena
nitakufunga.” amesema Prof. Gabriel
Prof. Gabriel ameitaka NARCO
kuhakikisha makampuni matano ambayo yanadaiwa fedha nyingi zaidi zinazokaribia
tshs Bilioni Moja, yalipe fedha hizo ili kuiwezesha NARCO iweze kufanya
shughuli zake na kuboresha ranchi inazozisimamia.
Katibu mkuu huyo ameitaka pia
NARCO kuwekeza katika ranchi zake ili wawekezaji waweze kupata huduma
mbalimbali muhimu kwa ajili ya mifugo yao yakiwemo maji na malisho pamoja na
kuboreha njia za mawasaliano na wawekezaji, kutengeneza mpango wa uwekezaji na
mikakati ya kiusalama.
Aidha Prof. Gabriel ameutaka
uongozi wa Umoja wa Wawekezaji wa Ranchi za Taifa (UWARATA) kufanya kazi kwa
kufuata misingi ya kisheria ikiwemo kusajili chama chao ili kiwe na nguvu ya
kusimamia wanachama wao katika kuhakikisha wanafanya kazi kwa kufuata taratibu
na sheria za nchi na kuwa daraja la mawasiliano kati ya Wizara ya mifugo na
Uvuvi na NARCO.
Akizungumza kuhusu deni la
tshs Bilioni Saba wanalowadai wawekezaji, kwa niaba ya Kaimu Meneja Mkuu wa Narco
Prof. Philemon Wambura, Meneja Masoko wa NARCO Bw. Emmanuel Mzava amesema deni
hilo limedumu kwa zaidi ya miaka miwili sasa na wamekuwa wakifanya juhudi
mbalimbali za kuwasiliana na wawekezaji ili waweze kulipa na katika kikao hicho
kuweka mkakati wa kulipwa deni hilo.
“Baada ya kufanya kikao na
katibu mkuu sisi watendaji tuliobaki hapa pamoja na wawekezaji katika vitalu
vilivyopo katika ranchi za taifa, miongoni mwa mambo tunayofanya ni kuwekeana
sasa kama makubaliano madogo ambayo yameandaliwa kwamba mwekezaji tunamsomea
deni lake na tunakubaliana lini analipa deni lake.” Amesema Bw. Mzava.
Nao baadhi ya wawekezaji
waliofika katika kikao hicho wamesema kimekuwa na manufaa makubwa kwao ili
waweze kutatua changamoto zinazowakabili na kuwa na misingi mizuri ya kuendelea
kumiliki vitalu walivyopatiwa na kulisha mifugo yao kwa kufuata sheria za nchi.
Kikao cha katibu Mkuu Wizara
ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel, uongozi
wa Kampouni ya Ranchi ya Taifa (NARCO) na wanachama wa Umoja wa Wawekezaji wa
Ranchi za Taifa (UWARATA), kimefanyika ikiwa ni siku chache baada ya Waziri wa
Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina kuutaka uongozi wa NARCO kubadilika na
kutumia maeneo yake kwa ajili ya kuwekeza na kupata faida ili iweze kujiendesha
na kutoa gawio serikalini.
Wanachama hao walioshiriki
kikao hicho wanatoka katika vitalu 111 vilivyopo katika ranchi za Kagoma, Kikulula,
Mabale na Kitengule zilizopo Mkoani Kagera, ranchi zingine ni Uvinza, Usangu na
Kalambo zilizopo Nyanda za juu Kusini na ranchi za Mkata, Mzeri, Dakawa
zilizopo Mashariki na Pwani.
Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa kwenye picha ya
pamoja na wawekezaji katika ranchi za taifa waliohudhuria kikao kwenye makao
makuu ya NARCO jana (15.07.2019) jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na wawekezaji
katika ranchi za taifa kwenye makao makuu ya NARCO jana (15.07.2019) jijini
Dodoma.
Mkurugenzi wa
Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Felix Nandonde
akifuatilia kikao cha Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof.
Elisante Ole Gabriel wakati akizungumza na wawekezaji katika ranchi za taifa
kwenye makao makuu ya NARCO jana (15.07.2019) jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni