Nav bar

Ijumaa, 19 Julai 2019

SHIRIKA LA KIMATAIFA LA AU-IBAR LAFADHILI MAFUNZO YA WAFUGAJI WA TANZANIA NA KENYA.



SHIRIKA la Kimataifa la AU-IBAR linalofadhili Mradi wa Utafiti wa uboreshaji na utunzaji wa Mbari za ng’ombe aina ya Sahiwal limefanikiwa kuwapeleka wafugaji wa Tanzania nchini Kenya kujifunza mbinu bora za uboreshaji mifugo.

Mradi huo unaotelekezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) umewezesha kunufaisha wafugaji wengi wa jamii ya Kimasai katika Wilaya ya Longido Mkoa wa Arusha kuanza uboreshaji mifugo yao kupitia njia ya uhimilishaji.

Akizungumza na wafugaji katika eneo la Kiligoris na Naivasha nchini wakati wa ziara ya mafunzo kwa wafugaji wa Tanzania, Mratibu Mwenza wa mradi huo kutoka TALIRI Makao Makuu Dodoma, Neema Urassa alisema mradi huo umeleta tija wafugaji wengi hasa katika Wilaya ya Longido.

Urassa alisema katika utekelezaji wa mradi huo wafugaji mia moja kutoka wilayani Longido mkoani Arusha wamenufaika kwa kujengewa uwezo kupitia mafunzo ya utunzaji bora wa ng’ombe na ufugaji wa kibiashara wenye tija utakaowezesha wafugaji kukidhi mahitaji ya lishe ya kaya, kutoa fursa za ajira na fursa za kujikwamua kiuchumi.

Aliongeza kuwa mradi huo pia ulitoa fursa kwa wafugaji hao wa Longido kufanya ziara ya mafunzo kwa vitendo katika Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji wa Mifugo Tanzania (NAIC) mkoani Arusha ili kuona madume bora yatakayotumika kutoa mbegu za Sahiwal na jinsi kazi hiyo inavyofanywa na wataalam kituoni hapo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Uhimilishaji NAIC Arusha Dkt. Paul Mollel amesema wafugaji watumie mbinu zilizofanyiwa utafiti na mbegu za Sahiwal ili kuboresha aina ya mifugo wanayofuga na kubadilishana uzoefu juu ya matumizi mbinu bora za ufugaji utakaoharakisha uzalishaji, Wafugaji mje kwa wingi katika kituo cha NAIC Arusha ili muweze kujipatia mbegu nzuri na bora za Sahiwal kwa ajili ya kupata ng”ombe bora na wazuri na mfuge kwa tija. Alisema Dkt. Paul Mollel


Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Masoko Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Abdalla Temba alisema Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa mbegu bora zinapatikana ili kuongeza uzalishaji wa nyama na maziwa.

Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wafugaji wa Sahiwal Longido (UWASALO), Peter Lengooya Ole Kipara amezishukuru Serikali za Tanzania na Kenya na wafugaji wa nchi hizo kwa umoja na ushirikiano mafunzo hayo yameongeza undugu kati yao na kwa umoja huu wameweza kujifunza kufuga kisasa na kuleta tija.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Wafugaji wa Sahiwal upande wa Kenya, David Ole Mosingo amesema mafunzo hayo yamewawezesha kuongeza uelewa na wamekubaliana na njia hiyo ili waweze kufuga kisasa na kwa manufaa zaidi.



Mratibu Mwenza wa Mradi wa Sahiwal kutoka TALIRI Makao Makuu Dodoma, Bi. Neema Urassa pamoja na Mratibu wa Mradi huo Tanzania Dkt. Zabron Nziku wakiangalia mifugo bora iliyoboreshwa kupitia mradi huo kwa wafugaji wa Transmara nchini Kenya

Mratibu Mwenza wa Mradi wa Sahiwal, Bi. Neema Urassa, akichangia hoja katika mafunzo ya wafugaji wa ng'ombe katika ukumbi wa DTI Naivasha Nchini Kenya

Mratibu Mwenza wa Mradi wa Sahiwal kutoka Taasisi ya Utafiti wa mifugo (TALIRI) Makao Makuu Dodoma, Neema Urassa akizungumza na wafugaji wa Transmara nchini Kenya wakati wa ziara ya mafunzo ya wafugaji kutoka Tanzania waliotembelea wenzao wa Kenya kwenye mradi unaofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la AU-IBAR.

Mratibu Mwenza wa Mradi wa Sahiwal kutoka TALIRI Makao Makuu Dodoma, Bi. Neema Urassa akiwa katika picha ya pamoja na wafugaji kutoka Tanzania wakiwa nje ya ukumbi wa TDI Naivasha nchini Kenya .


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni