Serikali kupitia Wizara ya
Mifugo na Uvuvi imedhamiria kupunguza umasikini kwa kuboresha kipato cha wafanyabiashara
na kuongeza ajira kwa wananchi kupitia
zao la ngozi hususan ngozi itokanayo na wanyama wafugwao hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uzalishaji Mifugo na Masoko,
Dkt.Felix Nandonde wakati akifungua mafunzo ya wachunaji wa ngozi wa machinjio
ya Manispaa ya Morogoro mjini humo.
Dkt.Nandonde amesema lengo la
mafunzo hayo ni kuhakikisha kuwa washiriki wanaongeza utaalamu katika
uchinjaji, uchunaji, ukaushaji, uhifadhi,usafirishaji na usindikaji ili
kuzalisha ngozi bora itayokuwa na thamani zaidi.
Akiongelea mchango wa zao la
ngozi kwenye pato la Taifa na la mtu mmoja, mmoja, Dkt.Nandonde alisema kuwa
hadi mwezi Machi mwaka 2018/19 jumla ya sh.bil.5.2 zilikusanywa kutokana na usafirishaji
ngozi na bidhaa zake nje ya nchi.
Akifafanua kuhusu sheria
Na.18 ya Mwaka 2008, inayosimamia biashara ya ngozi nchini, Dkt.Nandonde alisema
kuwa sheria hiyo inawataka wachunaji wote wa Ngozi kupata mafunzo na kupewa
leseni za uchunaji ngozi.
Akihitimisha hotuba yake
mgeni rasmi, Dkt.Nandonde alisema kuwa baada ya mafunzo hayo,Wizara ina mategemeo
makubwa sana kuhusu mabadiliko ya ubora wa ngozi zinazozalishwa hapa nchini.
Naye Kaimu Mkurugenzi
Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe, Wizara ya Mifugo na
Uvuvi, Bw.Gabriel Bura aliwataka washiriki kuzingatia mafunzo hayo ya awali na
kuahidi kuwa mafunzo mengine yataendelea kutolewa nchi nzima ikiwa ni kielelezo
cha serikali kuitambua na kuithamini kada hiyo.
Kwa upande wa washiriki wa
mafunzo hayo wakiongea kwa nyakati tofauti wameishukuru sana serikali ya awamu
ya tano kwa kuitambua na kuonyesha nia ya kuinua sekta hiyo kwa vitendo.
Aidha washiriki hao wameiomba
serikali pia kuangalia uwezekano wa kuwatafutia masoko ya uhakika ili kuinua
vipato vyao na kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye pato la taifa.
Mgeni rasmi,Mkurugenzi
wa Uzalishaji Mifugo na Masoko, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt.Felix
Nandonde (kushoto) akiongea na Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro Bw.John
Mgalula ofisini kwake leo kabla ya kufungua mafunzo ya wachunaji wa ngozi wa
machinjio ya manispaa hiyo.Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Msaidizi wa mazao ya
mifugo, usalama wa chakula na lishe, Bw.Gabriel Bura.
Washiriki wa mafunzo ya wachunaji wa ngozi wa machinjio ya
Manispaa ya Morogoro wakimsikiliza mgeni rasmi Dkt.Felix Nandonde (hayupo
pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku moja yanayofanyika mjini
Morogoro (12.6.2019).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni