Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amemshukuru Rais
Dkt. John Magufuli kufuatia ziara yake ya kikazi ya siku mbili aliyofanya nchini
Namibia kuanzia Mei 27 hadi 28 Mwaka 2019, kuanza kuonesha mafanikio baada ya
kupokea ugeni kutoka Kampuni ya Burmeister and Partners (PTY) Ltd inayomikili
kiwanda cha kuchakata nyama nchini Namibia iliyoonesha nia ya kuwekeza hapa
nchini.
Akizungumza (09.07.2019)
ofisini kwake katika mji wa serikali eneo la Mtumba Jijini Dodoma na mmoja wa
wakurugenzi katika kampuni hiyo Bw. Hendrick Boshoff, Prof. Gabriel amesema
lengo la ziara yake ni kupata taarifa za awali, kutoka kwa wataalam wa Wizara
ya Mifugo na Uvuvi ili waweze kuwa na njia sahihi ya uwekezaji ambao utakuwa na
tija kwa watanzania kupitia Sekta ya Mifugo.
“Mheshimiwa rais alifanya
ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Namibia akiambatana na Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina na viongozi wengine, nichukue fursa hii kwa niaba ya
wizara kumshukuru mheshimiwa rais kutuanzishia suala la soko la mazao ya mifugo
hususan nyama, tumetembelewa na mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni ya Burmeister
and Partners (PTY) Ltd inayomiliki kiwanda cha kuchakata nyama nchini Namibia
ili kukutana na wataalam baada ya rais kuonesha muelekeo na wao wakaitikia.”
Amesema Prof. Gabriel
Katika mazungumzo hayo Katibu
Mkuu huyo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo, amesema
wameuhakikishia ugeni huo kutoka Namibia kuwa wizara iko tayari kupitia Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina kwa kuhakikisha nia ya kampuni hiyo
kuanzisha kiwanda kingine cha kuchakata nyama hapa nchini inafikia katika
utekelezaji kufuatia ziara ya mheshimiwa rais nchini Namibia.
Prof. Gabriel amefafanua kuwa
ujio wa ugeni huo unaratibiwa na wizara nne zikiwemo za Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Viwanda na Biashara, Ofisi ya Waziri Mkuu eneo
la Uwekezaji na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Sekta ya Mifugo ambapo Prof.
Elisante Ole Gabriel ndiye Katibu Mkuu anayeshughulikia sekta hiyo na kwamba
ameupokea ugeni wa mkurugenzi wa kampuni hiyo kutoka Namibia kwa niaba ya
makatibu wakuu kutoka katika wizara nyingine tatu.
Aidha, ametoa wito kwa
watanzania kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali hususan zinazolenga
kuongeza masoko ya kutengeneza na kuuza bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
“Viwanda kama hivi vikija
ajira nyingi zitaongezeka na pia pato la taifa litaongezeka, bado tuko chini katika
ulaji wa nyama takwimu zilizotolewa na Shirika la Chakula Duniani (FAO)
zinaonesha walau mtu wa kawaida anatakiwa kula kilogramu 50 kwa mwaka, bado kwa
watanzania tunakula kilogram 15 kwa mwaka mzima, tunaleta wenzetu waongeze
bidii katika hilo ili wazalishe na soko la ndani liwepo tuuze na nje ya nchi.”
Alifafanua Prof. Gabriel
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Kampuni ya Burmeister and Partners (PTY) Ltd inayomikili kiwanda cha kuchakata
nyama nchini Namibia Bw. Hendrick Boshoff amwemambia Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel kuwa, kampuni hiyo
ilianza kuendesha shughuli zake miaka 40 iliyopita na wamekuja nchini Tanzania
wakilenga zaidi uwekezaji wa kuyaongezea thamani mazao ya mifugo hususan nyama.
Akimwakilisha Katibu Mkuu
Wizara ya Viwanda na Biashara katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Viwanda Vidogo
na Kati (DSME) Dkt. Consolata Ishebabi, amesema ugeni huo utafahamishwa pia
fursa mbalimbali zilizopo hapa nchini kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji
nchini (TIC) ili kufahamu mazingira mbalimbali ya uwekezaji yakiwemo ya sekta
binafsi.
Aidha, Dkt. Ishebabi
amefafanua kuwa ugeni huo utafikishwa pia katika Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO)
ambapo watafikishwa katika Ranchi ya Kongwa ambayo ipo chini ya NARCO kuweza
kuona aina ya mifugo iliyopo nchini na waweze kupata taarifa za jumla ambazo
zitawapatia mwanzo mzuri wa kuwekeza hapa nchini katika Sekta ya Mifugo.
Kikao hicho kiliwahusisha
wataalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda
na Biashara pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki.
Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akiagana na
kupiga picha ya pamoja na mmoja wa wakurugenzi katika Kampuni ya Burmeister na
Partners (PTY) Ltd inayomiliki kiwanda cha kuchakata nyama nchini humo Bw. Hendrick
Boshoff pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda
na Biashara, Ofisi ya Waziri Mkuu eneo la Uwekezaji pamoja na Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo)
Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika mazungumzo ofisini kwake jijini Dodoma
(09.07.2019) na mmoja wa wakurugenzi katika Kampuni ya Burmeister and Partners
(PTY) Ltd ya nchini Naimibia inayolimiki kiwanda cha kuchakata nyama nchini
humo Bw. Hendrick Boshoff (Picha ya kwanza juu kushoto) ambaye yupo nchini kwa
ajili ya nia ya kampuni hiyo kuwekeza kufuatia ziara ya Mhe. Rais Dkt. John
Magufuli nchini Namibia. Bw. Boshoff alisindikizwa na Dkt. Consolata Ishebabi
Mkurugenzi wa Viwanda Vidogo na Kati (DSME) (Picha ya chini kushoto) kutoka
Wizara ya Viwanda na Biashara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni