Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepongezwa kwa jitihada zake za
kuboresha mazingira ya wafugaji nchini, baada ya kuanzisha mchakato wa
uanzishwaji wa chama cha ushirika wa wafugaji wa ng’ombe wa asili.
Akifungua semina iliyowahusisha wafugaji wa ng’ombe wa
asili waliopo Wilayani Tunduru, Mkoani Ruvuma katibu tawala wa wilaya hiyo Bw.
Ghaibu Lingo amesema ushirika huo utakapoanzishwa itakuwa rahisi kwa uongozi wa
wilaya hiyo kutatua na kuwabaini wafugaji waliopo ili waweze kusaidiwa namna ya
kukua kiuchumi na kuboreshewa mazingira ya maeneo ya ufugaji.
Bw. Lingo amesema kupitia ushirikia huo pia itakuwa rahisi
kwa serikali ya wilaya kufahamu idadi halisi ya ng’ombe wa asili waliopo
wilayani hapo na mahitaji yanayotakiwa yakiwemo ya majosho na madawa kwa ajili
ya kuwahudumia mifugo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Ugani kutoka Idara
ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Dkt. Pius Mwambene amesema kuanzishwa kwa chama
cha ushirika wa wafugaji wa ng’ombe wa asili ni kati ya malengo saba ya wizara
hiyo yanayolenga kuboresha sekta ya mifugo nchini.
Dkt. Mwambene amesema ushirika huo utaweza kuwasaidia
wafugaji kujiinua kiuchumi na pia serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi
itaweza kuwatambua rasmi wafugaji hao kupitia chama hicho na kuweza kuwasaidia
kupitia chama chao.
Akitoa mada kuhusu malisho bora ya mifugo mara baada ya
kufunguliwa kwa semina hiyo, Afisa Mifugo kutoka Idara ya Uendelezaji wa
Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo Bw. Deogratius Nholope amewataka
wafugaji kuwa na ufahamu juu ya malisho bora ya mifugo yao ili iweze kuwa na
afya bora na kuweza kutoa mazao bora.
Bw. Nholope amesema kupitia kuanzishwa kwa chama cha
ushirika cha wafugaji wa ng’ombe wa asili katika Wilaya ya Tunduru, wafugaji
watapata fursa ya kufahamu namna ya kupata malisho bora na pia kupatiwa mbegu
kwa ajili ya kupanda malisho.
Naye Afisa Ushirika kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika
Bi. Miriam Mahuwi amewafahamisha wafugaji hao umuhimu wa ushirika kwa kuwa
utawajenga kiuchumi na hatimaye kuwa na ufugaji wenye mafanikio kupitia chama
hicho.
Bi. Mahuwi amesema ili kuanzishwa kwa ushirika huo ni
vyema wafugaji hao wakawa katika kikundi wanachoelewana na ambao wanafanya shughuli
inayofanana na kujiwekea malengo na hatimaye chama hicho mara baada ya
kuanzishwa kiweze kuwapatia mafanikio kiuchumi.
Semina hiyo imewahusisha wafugaji kutoka Wilaya ya
Tunduru, Mkoani Ruvuma ambao wamepatiwa vitalu na Halmashauri ya Wilaya ya
Tunduru ili waweze kulisha mifugo yao na kuondokana na tabia ya kuhamahama
kutafuta malisho.
Mkurugenzi Msaidizi wa Ugani, kutoka Idara ya Utafiti,
Mafunzo na Ugani Dkt. Pius Mwambene akitoa mada kwa wafugaji juu ya umuhimu wa
kuanzishwa kwa chama cha wafugaji wa ng’ombe wa asili katika Wilaya ya Tunduru,
Mkoani Ruvuma. (12.06.2019)
Afisa Mifugo kutoka Idara ya Uendelezaji wa Malisho na
Rasilimali za Vyakula vya Mifugo Bw. Deogratius Nholope akitoa mada kwa
wafugaji juu ya umuhimu wa malisho bora ya mifugo kwa wafugaji waliohudhuria
semina ya uanzishwaji wa chama cha ushirika wa wafugaji wa ng’ombe wa asili
katika Wilaya ya Tunduru, Mkoani Ruvuma. (12.06.2019)
Afisa Ushirika kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Bi.
Miriam Mahuwi akizungumzia faida na namna ya kuanzishwa kwa ushirika kwa
wafugaji waliohudhuria semina yenye lengo la kuanzishwa kwa chama cha ushirika
wa wafugaji wa ng’ombe wa asili katika Wilaya ya Tunduru, Mkoani Ruvuma.
(12.06.2019)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni