Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante
Ole Gabriel amesema anataka wizara hiyo
iwe ya mfano katika kumsaidia Rais Dkt. John Magufuli katika kutimiza majukumu
na malengo ya nchi kwa kufanya kazi kwa bidii na ufanisi zaidi.
Prof. Gabriel amesema hayo leo (08.05.2019) ofisini kwake
jijini Dodoma wakati akipokea taarifa ya ukaguzi wa utendaji kazi wa wizara
hiyo katika idara ya utawala na rasilimali watu, na kupongeza utendaji kazi wa
idara hiyo katika kusimamia matakwa ya mtumishi wa umma.
"Nina dhamira ya
dhati ya kuboresha wizara na mambo yote yaliyofanyiwa ukaguzi yatafanyiwa kazi
na yanaendelea kufanyiwa kazi pamoja na kusaini fomu zote za likizo kwa wakati,
kupandisha watumishi vyeo pamoja na kutoa elimu ya majukumu kwa waajiriwa
wote." Alisema Prof. Gabriel.
Aidha Katibu Mkuu huyo akizungumza mbele ya wakaguzi kutoka
katika tume hiyo wakiongozwa na bibi Kombe Shayo, ameshauri wakaguzi kutembelea
taasisi zilizo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi zikiwemo TALIRI, TAFIRI,
TVLA, FETA, Bodi ya Maziwa na Bozi ya Nyama kuona wanavyofanya shughuli zao,
kuonyesha kiwango au hatua walizofikia tangu kuanza kwa ukaguzi.
Hali kadhalika Prof. Gabriel ameomba wakaguzi kutoa elimu ya
‘opras’ kwa watumishi wa wizara mwishoni mwa mwezi Mei au mwanzoni mwa mwezi
Juni ili watumishi waelewe vizuri na
kupewa zaidi elimu ya nidhamu ya kazi pamoja na ufanyaji kazi mzuri,
ulio bora na wenye tija.
Awali akiwasilisha taarifa kwa katibu mkuu huyo, Mkaguzi
kutoka Tume ya Utumishi wa Umma Bibi Kombe Shayo amesema watumishi wanapaswa
kupewa elimu juu ya kujaza fomu ya ‘opras’ na watu wa masijala wapate maelekezo
ya jinsi ya kutunza fomu hizo pamoja na menejimenti ya wizara kuhakikisha
inapandisha watumishi madaraja na kuwathibitisha kazini kwa wakati pamoja na
watumishi kupata mgawanyo wa kazi.
"Watumishi wanaenda kwenye mafunzo na wanatoa taarifa
pindi wakiwa masomoni na pindi wamalizapo ambalo ni jambo zuri na pia ufadhili upo na watumishi wakasome
mapema na wasisubiri umri usogee" alifafanua Bibi Shayo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Bw.
Zakariyya Kera alipatiwa sifa za kipekee na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na
Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel pamoja na Mkaguzi wa Tume ya Utumishi
wa Umma Bibi Kombe Shayo kwa kufanya kazi kwa umahiri mkubwa katika idara hiyo
kutokana na kusimamia kwa ufanisi mkubwa mambo mbalimbali yahusuyo watumishi wa
wizara hiyo.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Zakariyya Kera akimwagiwa sifa za utendaji na mkaguzi Bi. Kombe Shayo. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni