SERIKALI ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Denmark
kupitia Shirika la Misaada la Kimaendeleo (DANIDA) imesema kuna haja ya
kuendeleza mapinduzi makubwa katika sekta ya uvuvi nchini ili kulinda
rasilimali zipatikanazo katika maziwa, bahari na mito nchini.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa kupokea taarifa ya
utafiti uliofanywa katika Ziwa Tanganyika lililopo Mkoani Kigoma, kutazama
mabadiliko ya tabia nchi katika eneo la ziwa hilo, Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema utafiti huo umeonyesha wazi kuwa zipo athari
zinazotokana na tabia nchi na sababu zingine kama idadi ya wavuvi kuongezeka na
baadhi yao kutumia zana haramu za uvuvi na kuathiri mazingira ya ziwa na
rasilimali zilizopo.
Mhe. Ulega amesema mambo yote ambayo yamefanyiwa utafiti
yakijadiliwa vyema litatolewa tamko la Sera ambayo itakuwa ni ushauri wa
kitaalam ambao utaiongoza serikali ikiwa inaendelea kufanya maboresho ya kanuni
na sheria za uvuvi.
"Kitu hiki ni muhimu sana kwa sababu eneo la Ziwa
Tanganyika watu wanatengemea sana kwa shughuli za kujipatia samaki na kuendesha
maisha yao, ile rasilimali tusipoweza kuweka mkakati mzuri wa kuitunza na
kuhakikisha kuwa inakuwa endelevu basi maana yake jamii ile kuna wakati ile
rasilimali kama sasa hivi kiasi cha samaki kimepungua sio kama ilivyokuwa huko
kipindi cha nyuma”. Alisema Mhe. Ulega
Amefafanua kuwa ni muhimu kuchukua hatua mbalimbali za
kielimu kwa kuwaelimisha wavuvi, hatua za kusimamia kwa kutumia njia zilizo
bora zaidi ili kupatikana kwa uendelevu wa rasilimali zilizopo katika Ziwa
Tanganyika.
“Kinyume na hapo watu watakosa zile fursa na umasikini
utajikita zaidi kwa hivyo ni muhimu kudhibiti na kuweza kuwa na mpangilio mzuri
ili mradi ile rasilimali iweze kuwa endelevu”. Alifafanua Mhe. Ulega
Aidha Naibu Waziri Ulega amebainisha kuwa serikali na
wananchi kwa ujumla ina jukumu la kudhibiti shughuli za kibinadamu ziendane na utaratibu wa ulinzi
wa mazingira ili kudhibiti athari za mazingira.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt.
Rashid Tamatamah amesema matokeo hayo ya utafiti yamekuja wakati muafaka kwa
sababu baadhi ya majukumu ya kisera ambayo wameyaleta yanahusiana na zoezi
ambalo linaendeshwa na wizara la kuboresha Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2003 ili
iendane na hali halisi ya sasa.
“Tumekusanya maoni kwa wadau nchi nzima na sasa tunachambua
yale maoni tuangalie maendeleo yanayotakiwa, kwa hiyo na hawa katika ushauri
wanaokuja nao na matamko ya kisera kuna maeneo vilevile kutokana na uchunguzi
waliofanya wanaona ili tuendelee vizuri katika kujenga rasilimali za uvuvi
katika Ziwa Tanganyika kuna vitu tunatakiwa tubadilishe kwenye sheria hivyo
wamekuja muda muafaka na tumefurahi sana”. Alisema Dkt. Tamatamah
Hali kadhalika, Bw. Ismail Aron Kimbilei ambaye ni
Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Mkoa wa Kigoma
amesema wamependekeza Ziwa Tanganyika kupumzishwa kwa shughuli za uvuvi kila
baada ya muda fulani ili kuongeza mazalia ya samaki.
“Naamini kwamba yatafanyiwa kazi na naamini utafiti wetu
utakuwa na faida kama watawahusisha
wadau kwamba wavuvi wawekwe chini na waelezwe faida za kutunza ziwa na waelezwe
hasara za kufanya kinyume na matarajio halafu waangalie na waamue kwa pamoja na wanaweza kufanya kwa mfano tuu
tuanze kwa kufunga miezi mitatu tuone matokeo yake kama dagaa na migebuka
itakuwa imeongezeka na baada ya hapo wataamua cha msingi ni kushirikisha
wadau.” Alisema Bw. Kimbilei
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni