SERIKALI imewataka wafugaji nchini kubadili fikra zao na
kutambua umuhimu wa kufuata sheria, taratibu na kanuni za nchi ili kujiepusha
na mkono wa sheria pindi wanapoingiza mifugo yao katika hifadhi na mapori ya
akiba.
Akizungumza na baadhi ya wafugaji jana (20.04.2019) katika
Wilaya ya Meatu, Mkoani Simiyu, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo)
Prof. Elisante Ole Gabriel amesema baadhi ya wafugaji wamekuwa wakiingiza
mifugo yao katika hifadhi na mapori ya akiba, hivyo kusababisha kutokuwepo kwa
mahusiano mazuri kati yao na wahifadhi kwa madai ya kuonewa ilhali wahifadhi
hao wanatakeleza sheria za nchi.
“Tunatamani fikra za wafugaji wote nchini zibadilike na
zianze kutambua umuhimu wa kufuata sheria, taratibu na kanuni, ndiyo msingi wa
mafaniko. Niwaombe wafugaji wote nchini watambue kwamba Wizara ya Mifugo na
Uvuvi itapenda wafugaji wafuate sheria, taratibu na kanuni, tukifanya hivyo
tutakuwa marafiki wa wizara unapokuwa mhalifu unakuwa tena siyo mfugaji bali
unakuwa mhalifu.” Alisema Prof. Gabriel.
Katibu mkuu huyo amelazimika kukutana na wafugaji hao
kutokana na hivi karibuni ng’ombe kukamatwa katika Pori la Akiba la Maswa
ambapo wamiliki wa ng’ombe hao wamekiri kufanya kosa na kulipa faini
waliyotozwa na mahakama mara baada ya kukiri kosa na kutiwa hatiani.
“Hivi karibuni ng’ombe walikamatwa katika Pori la Akiba la
Maswa, ndipo busara ikatumika kuona jambo hilo linafikia tamati ambapo wahusika
wamekabidhiwa ng’ombe zao kwa kuwa busara imetumika na siyo kwamba wao
wameshinda, kwa mujibu wa sheria wenzetu wa hifadhi wanachofanya ni kusimamia
Sheria Namba Tano ya Mwaka 2009 ya Hifadhi ya Wanyamapori kwamba mifugo
ikikamatwa inaweza kutaifishwa.” Alifafanua Prof. Gabriel.
Awali akizungumza na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Meatu kabla ya kuzungumza na wafugaji hao, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na
Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel amewashukuru madiwani wa halmshauri
hiyo wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Mhe.
Juma Issack Mpina kwa uelewa wa hali ya juu baada ya Meneja wa Pori la Akiba la
Maswa Bw. Lusato Masinde kutoa elimu na sheria iliyotumika na maamuzi
yaliyotolewa na mahakama kwa wafugaji waliyoingiza mifugo katika Pori la Akiba
la Maswa.
Aidha amebainisha kuwa kunapaswa kuwepo kwa mawasiliano
mazuri kati ya viongozi na jamii ya wafugaji katika maeneo yote nchini ili
kujenga mahusiano mazuri na kuelewa majukumu ya wasimamizi wa hifadhi na mapori
ya akiba ambao wamekuwa wakisimamia sheria na kwamba hawapo kwa ajili ya
kumuonea mtu yeyote.
Katika kikao na wafugaji Prof. Gabriel amewataka pia
wasijichukulie sheria mkononi hata wanapokuwa wamepishana kauli na wasimamizi
wa sheria kama ambavyo imekuwa ikijitokeza katika maeneo mbalimbali nchini ambapo
amebainisha kuwa kwa kufanya hivyo ni kosa kubwa kisheria, huku akiwapongeza
wafugaji wa Wilaya ya Meatu kwa kuwa watulivu na kuonesha ushirikiano kwa
maafisa wa Pori la Akiba la Maswa baada ya kuingiza mifugo yao katika pori hilo
kinyume na sheria na kutii hatua za kisheria zilizochukuliwa dhidi yao.
Akizungumza na wafugaji Katika kuhakikisha sekta ya ufugaji
inaboreka katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Wilaya ya Meatu, Mkoani
Simiyu, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole
Gabriel amesema wizara inahakikisha kwa juhudi zote inaboresha sekta ya ufugaji
nchini yakiwemo malisho bora kwa kuwepo kwa shamba darasa katika wilaya hiyo na
maeneo mengine.
Pia Prof. Gabriel amewataka wafugaji kufuga kisasa kwa kuwa
na ng’ombe wanaopatikana kwa njia ya uhimilishaji ambao wamekuwa na matokeo
mazuri kwa kuwa na nyama nyingi na maziwa mengi yenye ubora.
“Ukifuga wa kisasa wa ng’ombe wanaopatikana kwa njia ya
uhimilishaji hautajivunia idadi ya ng’ombe ulionao bali kwa kilo na wingi wa maziwa
ambao ng’ombe hao wanatoa, ambapo ng’ombe mmoja anafikia hadi kilogram 800 na
tumehakikisha kama wizara wafugaji wanapata mbegu za ng’ombe bora kwa bei
isiyozidi Shilingi Elfu Tano.” Alisema Prof. Gabriel
Kwa upande wake Meneja wa Pori la Akiba la Maswa Bw. Lusato
Masinde amesema wapo kwa ajili ya kuwasaidia wananchi na kwamba wataendelea
kusimamia sheria.
“Sisi tutaendelea kutoa elimu ili wananchi wafahamu umuhimu
wa sheria zilizopo nchini ikiwemo inayohusu maeneo ya hifadhi na mapori ya
akiba ili wananchi wasifanye shughuli zinazokatazwa katika maeneo hayo.”
Alisema Bw. Masinde.
Amefafanua wao kama maafisa wanaolinda Pori la Akiba la
Maswa wanahitaji ushirikiano kutoka kwa wananchi hususan wafugaji wa Wilaya ya
Meatu ili kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuwatia hatiani kwa kukiuka sheria
za nchi ambazo wamepewa kuzisimamia.
Nao baadhi ya wafugaji walioshiriki kikao cha Katibu Mkuu
Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel wameomba kupata
elimu zaidi juu ya uhimilishaji ili waweze kufuga ng’ombe kisasa na wenye tija
kiuchumi.
Pamoja na hilo wamewaomba pia wafugaji wenzao kufuata
sheria, taratibu na kanuni za nchi na kuwa karibu na viongozi wa wilaya hiyo
ili waweze kufanya shughuli zao kwa kufuata maelekezo yao na kuwa na mawasiliano
mazuri ambayo yatawaepusha kutojiingiza na ukiukwaji wa sheria kwa kuingiza
mifugo kwenye maeneo wasiyoruhusiwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni