Nav bar

Jumamosi, 30 Septemba 2023

WAZALISHAJI WA VYAKULA VYA MIFUGO WATAKIWA KUHAKIKI UBORA WA SAMPULI ZAO

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega ametoa rai na kuwasisitiza wazalishaji wa vyakula vya mifugo wote nchini kuhakikisha wanapeleka sampuli za vyakula wanavyozalisha kwenye maabara ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) ili kuhakiki ubora na viwango kwa kuzingatia matakwa ya sheria hiyo kabla ya kuanza kuwauzia wafugaji ndani ya nchi au kuvisafirisha nje ya nchi. 


Waziri Ulega alitoa rai hiyo wakati akifungua warsha kuhusu uzalishaji wa protini kwa ajili ya vyakula vya Mifugo na kupunguza ushindani iliyofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 29, 2023.


Alisema kuwa tasnia hiyo imepewa kipaumbele na umuhimu wa pekee kwa kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetunga sheria mahususi inayojulikana kwa jina la Sheria ya Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Wanyama (Sura Na.180) pamoja na Kanuni na Miongozo mbalimbali. Lengo la sheria hiyo ni kuhakikisha vyakula vinavyozalishwa vinakidhi ubora na viwango stahiki ili kuwezesha uzalishaji bora wa mifugo, samaki na mazao yatokanayo na mifugo na samaki. 


Aliendelea kufafanua kuwa pamoja na  Sheria hiyo, Wizara inayo Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) iliyopewa jukumu la kuhakiki na kupima ubora na viwango stahiki vya malighafi zinazotumika kwenye uzalishaji wa vyakula vya mifugo. 


"Hivyo, ninapenda kupitia warsha hii kutoa rai na msisitizo mkubwa kwa wazalishaji wa vyakula vya mifugo wote nchini kuhakikisha wanapeleka sampuli za vyakula wanavyozalisha kwenye maabara ya TVLA ili kuhakiki ubora na viwango kwa kuzingatia matakwa ya sheria hiyo kabla ya kuanza kuwauzia wafugaji wetu au kuvisafirisha nje ya nchi," alisema Waziri Ulega 


Aidha, aliitaka TVLA kuhakikisha inatembelea katika maeneo ya wazalishaji wa malighafi za kutengeneza vyakula vya Mifugo ili wakakague ubora wa malighafi hizo ili kuongeza tija na ufanisi wa kazi katika kulinda usalama wa chakula cha mifugo.


Sambamba na hilo, Waziri Ulega amewahimiza wafugaji wote wa mifugo na samaki na watumiaji wa rasilimali za vyakula vya mifugo, kuhakikisha wanatumia vyakula vinavyozalishwa kwenye viwanda vilivyosajiliwa na kutambuliwa rasmi na Wizara ya Mifugo na Uvuvi. 


 Aliongeza kwa kusema kuwa wafugaji wakitumia vyakula vinavyozalishwa kwenye Viwanda itasaidia kupunguza malalamiko ya udumavu wa mifugo kwa kulishwa vyakula visivyo na ubora na viwango stahiki na hivyo kumwongezea hasara na mara nyingine kusababisha hata vifo kwa mifugo na samaki.



"Kwa kufuata utaratibu huo, Wizara itaweza kufuatilia malalamiko yanayoweza kutokea kwa vile mfugaji atakuwa ana uhakika wa chanzo cha chakula alichotumia kimetoka kwa mzalishaji gani", alibainisha Waziri Ulega


Kwa upande wake, Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Mhe. Wieber de Boer alisema gharama za uzalishaji wa protini kwa ajili ya chakula cha mifugo ni kubwa hapa nchini hivyo wapo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutafuta njia mbadala ya kutatua changamoto hiyo ili sekta ya mifugo iweze kukua vizuri.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiongea na wadau wa sekta ya mifugo wakati akifungua warsha kuhusu uzalishaji wa protini kwa ajili ya vyakula vya Mifugo na kupunguza ushindani iliyofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 29, 2023.

Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Mhe. Wieber de Boer akitoa neno la utangulizi katika warsha kuhusu uzalishaji wa protini kwa ajili ya vyakula vya Mifugo na kupunguza ushindani iliyofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 29, 2023.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akiteta jambo na Mkurugenzi wa Viumbe Maji, Dkt. Nazael Madalla katika warsha kuhusu uzalishaji wa protini kwa ajili ya vyakula vya Mifugo na kupunguza ushindani iliyofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 29, 2023.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akimueleza jambo Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Mhe. Wieber de Boer (kushoto) walipokutana mapema leo kando ya   warsha kuhusu uzalishaji wa protini kwa ajili ya vyakula vya Mifugo na kupunguza ushindani iliyofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 29, 2023. Kulia ni Mtendaji Mkuu wa Kituo cha SAGCOT, Bw. Geoffrey Kirenga.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Bw. Rogers Shengoto akiwa katika warsha kuhusu uzalishaji wa protini kwa ajili ya vyakula vya Mifugo na kupunguza ushindani iliyofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 29, 2023.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni