Nav bar

Jumamosi, 30 Septemba 2023

PROF. SHEMDOE AWAAGA WAWAKILISHI MICHUANO YA SHIMIWI

◾Waahidi Makubwa, Kuelekea Iringa kesho 


Katibu Mkuu Wizara ya Mfugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amewaaga wawakilishi wa wizara hiyo kwenye  michuano ya SHIMIWI ambapo amewataka wawakilishi hao kurejea na ushindi wa nafasi ya kwanza kwenye kila mchezo watakaoshiriki.


Katika tukio hilo lililofanyika Septemba 27, 2023 kwenye Ofisi ndogo za Wizara hiyo zilizopo jengo la NBC jijini Dodoma, Prof. Shemdoe amewataka wachezaji wote waliochaguliwa kushiriki kwenye michuano hiyo kujituma na kucheza kwa ushindani wakati wote wa michuano hiyo.


“Mimi mara zote nipo kwenye timu ya ushindi kwa hiyo hata huku naamini nimekuja kwenye timu ya ushindi na nina Imani sana na nyinyi kwa sababu ninafahamu kuwa kwenye mashindano ya mwaka huu tutakuwa na vikombe vingi zaidi ya vile tulivyoshinda mwaka jana” Ameongeza Prof. Shemdoe.


Akisisitiza suala la kudumisha  nidhamu , Prof Shemdoe amewataka wachezaji hao kutambua kuwa wao ni watumishi wa umma hivyo wanapaswa kufuata taratibu zote zinazowaongoza kulingana na nafasi zao wakati wote wakiwa kwenye mashindano hayo.


“Wale dada zangu ambao mmefanya vizuri msimu uliopita niwaombe mkafanye vizuri zaidi mwaka huu na ninajua tuna washiriki wengi wa mchezo wa Kamba,nina Imani safari hii tutashika nafasi ya kwanza inshaallah” Amebainisha Prof. Shemdoe.


Awali akitoa taarifa fupi ya maandalizi ya timu hizo yalivyokuwa Mwenyekiti wa SHIMIWI kutoka Wizarani hapo Bw. Ally Suru aliuhakikishia uongozi wa Wizara kufanya vizuri kwenye mashindano hayo kutokana na maandalizi mazuri waliyoyafanya.


"Naomba nitumie fursa hii kwa niaba ya viongozi wenzangu, makocha na wachezaji kuwashukuru Viongozi wa Wizara kwa ushirikiano mkubwa ambao wametupatia tangu tulipoanza maandalizi yetu na tunaomba muendelee kutuonesha ushirikiano huo ili tufanye vizuri zaidi kwenye mashindano huko Iringa" Aliongeza Bw. Suru.


Aidha Bw. Suru amewapongeza viongozi hao kwa uamuzi  wa kupeleka washiriki wa michezo yote inayoshindaniwa kwenye michuano hiyo jambo ambalo limekuwa ni kinyume kwa Taasisi nyingi kutokana na changamoto ya ufinyu wa bajeti.


Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wanamichezo wenzake, mwakilishi wa wachezaji hao Dkt. Aurelia Bundala amemuahidi Prof. Shemdoe kutekeleza yote aliyowaasa ambapo amemhakikishia kuwa wataibuka vinara kwenye kila mchezo watakaoshiriki.


Jumla ya wanamichezo 93 kutoka wanaoshiriki michezo ya Mpira wa miguu, mpira wa pete, kuvuta Kamba, mbio za baiskeli, riadha na kurusha vishale kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wataondoka Septemba 28, 2023 kuelekea  mkoani Iringa inakotarajiwa kufanyika Michuano ya SHIMIWI kuanzia Septemba 29, 2023.Hakuna maoni:

Chapisha Maoni