◾ Yatoa suluhu na Ofisi ya waziri Mkuu (Sera) upande wa mpira wa miguu.
Timu ya mpira wa pete kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza vema mbio za kutwaa taji la mchezo huo kwenye michuano ya SHIMIWI inayoendelea mkoani Iringa mara baada ya kufanikiwa kuifunga timu ya Tume ya Utumishi kwa magoli 11-6 kwenye mchezo uliochezwa chuo kikuu cha Ruaha leo Septemba 29, 2023.
Timu hiyo ilianza kwa kasi ya chini kipindi cha kwanza ambapo hadi timu zinaenda mapumziko ilikuwa imeshakubali kichapo cha magoli 4-3 hali iliyomlazimu kocha wa timu hiyo Bi. Masele Shabani kufanya mabadiliko na kuiongezea kasi timu hiyo hali iliyowafanya waibuke na ushindi huo mpaka mwisho wa mchezo.
Kwa upande mwingine katika mchezo uliochezwa mapema kabisa leo asubuhi, timu ya Wizara hiyo kwa upande wa mpira wa miguu imetoka suluhu na timu ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera) mara baada ya kuhitimishwa kwa mchezo uliokuwa na upinzani mkali kutoka pande zote mbili.
Timu hiyo inatarajia kutupa karata yake ya pili kesho (Septemba 30, 2029) kwenye mchezo baina yake na timu ya Mawasiliano utakaochezwa kwenye uwanja wa Mkwawa 2 kuanzia saa 08 kamili mchana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni