Nav bar

Jumatatu, 25 Aprili 2022

NZUNDA AHIMIZA WELEDI, UWAJIBIKAJI*

 

Na Mbaraka Kambona, Morogoro

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda amewataka Watumishi wa Wizara hiyo, Sekta ya Mifugo kufanya kazi kwa weledi, uadilifu, uwajibikaji na usikivu kwa umma ili waweze kutoka huduma bora kwa jamii.

Nzunda alitoa wito huo alipokuwa akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi, Sekta ya Mifugo kilichofanyika Mkoani Morogoro Machi 18, 2022.

Wakati akizungumza na Watendaji na Watumishi wa Wizara hiyo aliwataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake waimarishe uwajibikaji ili waweze kuwaletea  maendeleo wananchi.

"Jukumu letu la kwanza ni kuhakikisha tunatoa huduma bora kwa umma kwa kiwango cha juu na zinazokidhi matarajio na matakwa ya wananchi", alisema Nzunda

Pia, aliwataka wajiandae kufanya mabadiliko makubwa katika Sekta hiyo huku akiwahimiza kuja na mikakati ya kupata rasilimali fedha nje ya bajeti ya Serikali.

"Ili tuweze kuleta mabadiliko hayo ni wajibu wetu kuwa wabunifu na kuwashirikisha Wadau kupata rasilimali na kuvutia wawekezaji kuwekeza katika sekta hii", aliongeza

Aliendelea kusema kuwa serikali itaendelea kuwawekea mazingira bora ya utendaji wa kazi ikiwemo kuwapatia rasilimali fedha na vifaa ili waweze kutoa huduma ambayo wananchi wanaitaka.

Aidha, aliwataka Watumishi hao kufanya kazi kwa kuzingatia matokeo chanya na kuachana na michakato isiyo na tija

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda akiongea na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Sekta ya Mifugo (hawapo pichani) wakati akifungua kikao cha baraza hilo kilichofanyika Mkoani Morogoro Machi 18, 2022. wakati akifungua kikao hicho, Bw. Nzunda aliwahimiza Watumishi kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi ili kuongeza tija na ufanisi wa kazi. 

 

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi, Sekta ya Mifugo muda mfupi baada kufungua kikao cha baraza hilo kilichofanyika Mkoani Morogoro Machi 18, 2022. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni