Nav bar

Jumatano, 31 Mei 2023

​VIJANA WANUFAIKA MAFUNZO YA UVUVI KUPEWA KIPAUMBELE KATIKA MIKOPO

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewahakikishia vijana walionufaika na mafunzo atamizi ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji na ambao wameshaandaa maandiko ya miradi kuwa watapewa kipaumbele katika kupata mikopo ili waweze kuendeleza miradi yao.

Waziri Ulega alitoa kauli hiyo wakati akifunga mafunzo atamizi ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji katika hafla fupi iliyofanyika mkoani Mwanza Mei 29, 2023.

Alisema kuwa Wizara yake inatambua changamoto ya upatikanaji wa mitaji kwa wawekezaji katika sekta ya uvuvi hivyo kupitia programu hiyo wizara imejipanga kuwasaidia wanufaika wa mafunzo hayo kupata mitaji ya kuanzisha miradi iliyobuniwa kutokana na maandiko waliyowasilisha wizarani.

"Juhudi hizi za kutafuta mitaji ni pamoja na ruzuku na mikopo kutoka serikalini, taasisi za kifedha na washirika wa maendeleo. Nipende kusisitiza kuwa uanzishwaji wa vikundi, ushirika au kampuni ni fursa ya kuweza kufikiwa kirahisi na serikali sambamba na kupata fursa za mikopo yenye masharti nafuu kutoka serikalini na taasisi mbalimbali za kifedha,"alisema

Aliongeza kuwa programu hiyo ya atamizi inaendana na azma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yenye nia ya kuwajengea uwezo vijana katika fani ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji ili waweze kujiajiri, kuongeza tija na kuongeza kipato kwa mtu na Taifa kwa ujumla.

Aidha, aliwaeleza vijana hao kuwa hatua walizoanza kuchukua za mchakato wa kuunda vikundi au kampuni kwa nia ya kuanzisha miradi ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji zitasaidia kwa kiasi kikubwa juhudi ya serikali ya kuongeza fursa za ajira kupitia sekta ya uvuvi; na kuchangia ukuaji wa sekta kutoka asilimia 2.5 ya sasa hadi kufikia asilimia 8.4 ifikapo mwaka 2025/2026.

Kwa upande wao vijana 197 walionufaika na mafunzo hayo walimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa fursa ya kujifunza kwa vitendo ufugaji wa samaki wakisema kuwa fursa hiyo itawawezesha kujiajiri, kukuza kipato chao na Taifa kwa ujumla.




#MifugoNaUvuviNiUtajiri

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni