Nav bar

Jumatano, 31 Mei 2023

HEKARI 5,520 ZA NARCO ZAKABIDHIWA KWA WANANCHI

Na. Edward Kondela

 

Serikali imekabidhi hekari 5,520 za Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kwa wananchi wa wilaya za Bagamoyo, Chalinze na Kibaha Mkoani Pwani ili ziendelezwe kwa shughuli mbalimbali za kijamii zikiwemo za mifugo na kilimo.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (Mb), amebainisha hayo (26.05.2023) katika Ranchi ya Ruvu iliyopo Wilaya ya Kibaha, ambapo amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeridhia kukabidhi hekari 5,520 kwa vijiji 19 vilivyokuwa vimevamia sehemu ya eneo la ranchi na kuwataka wananchi ambao wapo ndani ya mipaka mipya ya Ranchi ya Ruvu kuondoka mara moja.


Mhe. Silinde amesema serikali imeridhia kukabidhi hekari hizo baada ya timu iliyoundwa mwaka wa fedha 2019/20 kutoa mapendekezo juu ya vijiji vilivyozunguka Ranchi ya Ruvu ambavyo vilivamia eneo la ranchi hiyo.


Ameongeza kuwa kufuatia uamuzi huo wa serikali, amewataka viongozi wa maeneo hayo kupanga mipango bora ya ardhi ili kuondokana na migogoro ya ardhi baina ya wafugaji na wakulima na kuwataka wananchi kutovamia tena mipaka mipya iliyopo kati ya Ranchi ya Ruvu na vijiji vinavyozunguka ranchi hiyo.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Aboubakar Kunenge amesema kufuatia makabidhiano ya ardhi hiyo kwa wananchi kutoka NARCO, ni dhahiri serikali imeamua kutafuta suluhu kwa wananchi wake kwa kuwapatia eneo ambalo wataweza kufanya shughuli zao baada ya kukaa kwa muda mrefu katika eneo hilo ambalo walikuwa hawalimiliki.


Mhe. Kunenge amewataka wananchi kuendelea kuiamini serikali na kuwataka kutoa ushirikiano kwa viongozi wao badala ya kujichukulia maamuzi ambayo baadae yanasababisha kutoa hisia tofauti kuwa serikali haiwajali wananchi wake na kukemea vitendo vya uvamizi wa maeneo ya serikali.


Nao baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo fupi wamepongeza maamuzi ya serikali ya kuwakabidhi ardhi ambayo wamekuwa wakiitumia na kuahidi kuzidi kutoa ushirikiano kwa serikali na kuipongeza kwa kuwapatia ardhi hiyo ambayo wataiendeleza kwa shughuli zao na kuwa walinzi wa mipaka ya Ranchi ya Ruvu ambayo wanaiuzunguka.


Serikali imekabidhi hekari 3,720 kwa Wilaya ya Chalinze, hekari 300 Wilaya ya Bagamoyo na hekari 1,500 Wilaya ya Kibaha ambazo zilikuwa zikimilikiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) katika Ranchi ya Ruvu ambayo wananchi walikuwa wamevamia sehemu ya ranchi hiyo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (Mb) akizungumza juu ya maamuzi ya serikali kutoa hekari 5,520 za Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kutoka katika Ranchi ya Ruvu kwa ajili ya wilaya za Bagamoyo, Chalinze na Kibaha Mkoani Pwani kwa vijiji 19 vinavyozunguka ranchi hiyo ambavyo vilikuwa vimevamia eneo la ranchi na kuwataka wananchi waliovamia mipaka mipya ya ranchi kuondoka mara moja. Naibu Waziri Silinde amezungumza hayo katika hafla fupi iliyofanyika katika Ranchi ya Ruvu iliyopo Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani. (26.05.2023)


Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Aboubakar Kunenge akibainisha namna serikali ilivyoamua kutafuta suluhu kwa wananchi wake kwa kuwapatia maeneo ambayo wataweza kufanya shughuli zao baada ya kukaa kwa muda mrefu kwenye maeneo hayo ambayo walikuwa hawamiliki. Mhe. Kunenge amebainisha hayo katika hafla fupi iliyofanyika katika Ranchi ya Ruvu iliyopo Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani, ambapo serikali imekabidhi hekari 5,520 za Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kutoka katika Ranchi ya Ruvu kwa ajili ya wilaya za Bagamoyo, Chalinze na Kibaha Mkoani Pwani kwa vijiji 19 vinavyozunguka ranchi hiyo. (26.05.2023)

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Prof. Peter Msoffe (aliyekaa kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Chalinze Bw. Ramadhan Possi wakitia saini makabidhiano ya eneo la hekari 3,720 lililokuwa linalomilikiwa na NARCO kutoka katika Ranchi ya Ruvu baada ya serikali kuamua kukabidhi eneo hilo kwa wananchi waliokuwa wamevamia eneo hilo. Wanaoshuhudia utiaji saini huo ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Aboubakar Kunenge, katika hafla fupi iliyofika kwenye Ranchi ya Ruvu. (26.05.2023)

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Prof. Peter Msoffe akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kibaha Bi. Butamo Ndalahwa hati ya makabidhiano ya eneo la hekari 1,500 lililokuwa linamilikiwa na NARCO kutoka katika Ranchi ya Ruvu baada ya serikali kuamua kukabidhi eneo hilo lililokuwa limevamiwa na wananchi. Hafla hiyo fupi imefanyika kwenye Ranchi ya Ruvu iliyopo Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani. (26.05.2023)

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Prof. Peter Msoffe akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Bagamoyo Bw. Shauri Selenda hati ya makabidhiano ya eneo la hekari 300 lililokuwa linamilikiwa na NARCO kutoka katika Ranchi ya Ruvu baada ya serikali kuamua kukabidhi eneo hilo kwa wananchi waliokuwa wamelivamia. Hafla hiyo fupi imefanyika kwenye Ranchi ya Ruvu iliyopo Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani na kushuhudiwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Aboubakar Kunenge. (26.05.2023)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni