Nav bar

Jumatano, 31 Mei 2023

VITUO ATAMIZI VYA MIFUGO VITATUE CHANGAMOTO YA AJIRA KWA VIJANA

Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) imetakiwa  kuwasimamia vizuri vijana 240 wanaoendelea kupatiwa mafunzo ya unenepeshaji mifugo  katika vituo atamizi 8 chini ya LITA ikiwa ni mpango wa Serikali kusaidia vijana hao kujiajiri na  kujikwamua kiuchumi.


Wito huo umetolewa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu ambaye ni  Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina wakati wa kikao cha baraza la wafanyakazi wa LITA kilichofanyika mkoani Arusha Mei 26, 2023.


Dkt. Mhina alisema Serikali imeanza kutekeleza mradi huo katika mwaka huu wa fedha baada ya kubaini wataalamu wanaotoka katika vyuo hivyo wanayo nafasi ya kupatiwa ujuzi zaidi ya kuzalisha kupitia vituo atamizi ili watakaporejea mitaani waweze kuwa na uwezo wa kuwekeza zaidi.


“Tunatengeneza wataalam ambao ni wawekezaji wao wenyewe watakapoweza kuzalisha ndivyo ambavyo tutaweza kuzalisha malighafi zaidi kwenye viwanda vyetu, kwahiyo hatutarajii wakitoka hapa wakategemee kuajiriwa ndio maana tunawaweka kwenye vituo atamizi ili wafanye kwa vitendo na kufanya kibiashara zaidi” amesema


Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene alifafanua kuwa mradi huo kwa kuanzia utatekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja ambapo utagawanywa kwa awamu 4 ambapo vijana hao watahudumia mifugo kwa kunenepesha ndani ya miezi 3.


Alisema katika kila kituo kuna  vijana wasiopungua 30 ambapo kila mmoja anahudumia ng’ombe 10 kwa kuwanenepesha kwa kipindi cha miezi mitatu na kufanya wahudumia ngombe 40 kwa mwaka mzima


“ kila kijana kwa mzunguko moja amepewa ng’ombe 10 wa kunenepesha kwa hiyo kwa mwaka mzima atanenepesha ngombe 40  na tunategemea faida itakayotokana na hao Ng’ombe watakao uzwa mnadani ni mtaji kwa kijana kwa ajili ya kwenda kuanzisha mradi wake baada ya kumaliza mwaka mmoja” amesema


Aliongeza kuwa mradi huo utakuwa fursa nzuri kwa vijana kufuga kibiashara kwa sababu licha ya kuanza kutekeleza mradi huo mwezi Aprili mwaka huu tayari wameanza kupokea oda ya kuhitaji ng’ombe hao.


Mwakilishi wa katibu Mkuu, ambae ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi,  Dkt. Charles Mhina akiongea wakati wa kufungua kikao cha baraza la wafanyakazi wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kilichofanyika Tengeru LITA mkoani Arusha, Mei 26,2023


Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Plus Mwambene (kulia) akieleza namna wakala hiyo inavyotekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa vitendo ili kuwaandaa vijana kujiajiri, kwa Mwakilishi wa Katibu Mkuu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina  wakati alipoenda kufungua kikao cha baraza la wafanyakazi LITA kilichofanyika Tengeru mkoani Arusha Mei 26,2023.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Mhina (kulia) akimsikiliza kwa makini mkuu wa chuo cha Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) Tengeru, Dkt.  Flora Kajuna (kushoto) wakati alipotembelea maabara chuoni hapo alipoenda kufungua kikao cha baraza la wafanyakazi LITA Mei 26, 2023 Mkoani Arusha.

Mwanafunzi anayejikita kwenye eneo la Afya ya Mnyama na Uzalishaji Bw. Julius Mmbando akionyesha namna taarifa /majibu ya vipimo vya magonjwa mbalimbali ya mnyama yanavyotoka kwenye mashine ya kupimia magonjwa hayo ya mifugo kwa Mwakilishi wa Katibu Mkuu Dkt. Charles Mhina alifika chuoni hapo Tengeru Mkoani Arusha Mei 26,2023.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu ambae pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa baraza hilo mara baada ya kikao kifupi kilichofanyika kwenye ukumbi wa chuo cha Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) Tengeru mkoani Arusha,  Mei 26, 2023 wa pili kutoka kulia ni Mtendaji mkuu wa Wakala hiyo Dkt. Pius Mwambene.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni