Nav bar

Jumatano, 31 Mei 2023

ASILIMIA 90 YA MAZIWA YANAYOZALISHWA NCHINI YAPO NJE YA MFUMO-DKT. MUSHI

◼️ AWAMWAGIA SIFA ASAS KWA MCHANGO WAO KWENYE JAMII INAYOWAZUNGUKA 


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Daniel Mushi ameitaka Bodi ya Maziwa nchini kwa kushirikiana na wadau wote waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa bidhaa hiyo kufanya tathmini ya kina juu ya kiwango cha maziwa yanayozalishwa na kupotea kabla hayajaingia kwenye mfumo rasmi wa uchakataji.


Dkt. Mushi amesema hayo Mei 31,2023 wakati akifungua kongamano la wadau wa tasnia ya maziwa lililofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambapo amebainisha kuwa ni asilimia 10 pekee ya maziwa yanayozalishwa ndio yanayoingia kwenye mfumo rasmi huku asilimia 90 ikiwa haijulikani ilipo.


“Kwanza ni lazima tukubali kuwa kiwango cha maziwa cha lita Bil.3.6 kwa mwaka ni kidogo sana ukilinganisha na idadi ya mifugo tuliyonayo lakini pia tungetamani tufike mahali tujitosheleze kwenye matumizi ya maziwa yanayozalishwa hapa nchini kwa sababu kwa  sasa tunatumia maziwa mengi yanayoagizwa kutoka nje” Ameongeza Dkt. Mushi.


Dkt. Mushi amesema kuwa viwanda vilivyopo hapa nchini vina uwezo wa kuchakata lita 865,000 lakini mpaka sasa viwanda hivyo vinachakata asilimia 25 tu ya uwezo wake jambo ambalo amebainisha kuwa linarudisha nyuma jitihada za wasindikaji hao katika kukuza uchumi wa taifa kwa ujumla.


Katika hatua nyingine Dkt. Mushi ameipongeza kampuni ya ASAS kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kukuza tasnia ya maziwa na ustawi wa jamii inayoizunguka kupitia shughuli zake za usindikaji wa maziwa.


“Kwa kweli ASAS wamefanya kazi kubwa sana kiukweli ningetamani tuwe na kina ASAS wengi zaidi hapa nchini kwa sababu naamini hilo lingepeleka mbali sana maendeleo ya tasnia ya maziwa hivyo nitoe wito kwa wasindikaji na wadau wengine wa maziwa tuachane na mashindano na badala yake tushirikiane kutumia fursa nyingi sana zilizopo kwenye tasnia kwa sababu hata wakiwepo kina ASAS 20 bado hawatatosha” Amesisitiza Dkt. Mushi.


Kongamano la wadau wa Tasnia ya maziwa hufanyika kila mwaka kwa lengo la kujadili na kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili wadau wote waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa maziwa.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni