Nav bar

Jumatano, 31 Mei 2023

SERIKALI YAJA NA MPANGO MAALUM WA MAFUNZO YA UFUGAJI SAMAKI

Na. Edward Kondela


Serikali kuanza kutoa mafunzo maalum ya muda mfupi kwa wafugaji wa samaki kote nchini ili kukuza tasnia hiyo na kuleta tija kwa nchi na wananchi kwa ujumla.


Hayo yamebainishwa (19.05.2023) jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Sekta ya Uvuvi) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh, mara baada ya wizara hiyo kuingia hati ya makubaliano kupitia Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA) na Chama Kikuu cha Wakuza Viumbe Maji Tanzania (AAT) ili wakala hiyo kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wafuga samaki na watu wanaotaka kuingia katika tasnia hiyo kupitia Mradi wa Kikanda wa Ukuzaji Viumbe Maji (EAC TRUEFISH PROJECT).


Prof. Sheikh amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo kwenye sekta za uzalishaji ikiwemo uvuvi kwa kuweka fedha nyingi kwenye ukuzaji viumbe maji hususan ufugaji wa samaki, hivyo kuna haja ya kuweka mafunzo maalum katika ufugaji wa viumbe maji.


“Huu ni ushirikiano kati ya wizara kupitia chuo cha FETA, kwa kuwa serikali imeweka fedha nyingi katika ufugaji viumbe maji, kuwa na mafunzo ya namna hii ya ufugaji wa samaki na kutengenza mitaala inayokubalika kwa Afrika Mashariki ni suala la msingi ili kufuga kwa tija.” Amesema Prof. Sheikh


Ameongeza kuwa lengo la makubaliano hayo ni kuwa na wanufaika wengi ambapo kwa sasa wataanza na wachache ambao wanategemewa kwenda kufundisha wengine baada ya kuhitimu mafunzo hayo ili kuwa na ufugaji wa tija.


Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA) Dkt. Semvua Mzighani amesema mafunzo ya ufugaji samaki yatatolewa kwa muda wa wiki moja hadi mbili kwa kuanzia katika Kampasi ya FETA iliyopo Nyegezi jijini Mwanza, ambapo kwa sasa walengwa wakubwa ni katika Bonde la Ziwa Victoria ambao tayari wameanza kufuga samaki ili kuwapatia maarifa ya ufugaji bora.


Dkt. Mzighani amefafanua kuwa masomo yatakayofundishwa katika kozi hizo ni namna ya kupata vifaranga bora vya samaki, vyakula bora vya samaki na namna ya kuwafuga samaki ili wakue wakiwa salama na wenye afya njema kabla ya kuwafikisha sokoni.


Aidha, amesema mafunzo hayo yatakuwa na mbinu mpya na aina nzuri ya ufugaji ambayo itampa faida mfugaji kwa sababu ufugaji ni biashara na kwamba wananchi ambao pia bado hawajaanza ufugaji samaki wanaruhusiwa pia kufika katika Kampasi ya FETA Nyegezi jijini Mwanza ili kupatiwa utaratibu wa kupata mafunzo hayo.  


Naye Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Wakuzaji Viumbe Maji Tanzania (AAT) Dkt. Charles Mahika amesema mafunzo hayo ni muhimu kwao hususan katika kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa chakula bora cha samaki, mafunzo ya kuzalisha vifaranga bora vya samaki pamoja na upatikanaji wa masoko ya samaki.


Dkt. Mahika ameongeza kuwa wao kama chama kazi yao kubwa ni kuwaunganisha wafugaji wa samaki kote nchini kupata mafunzo hayo kutoka FETA ambapo wanaamini ufugaji wa samaki utakuwa na tija zaidi kwa kuzingatia kumekuwa na ongezeko la ufugaji kwa kutumia vizimba.


Hati ya makubaliano hayo iliyotiwa saini kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA) na Chama Kikuu cha Wakuzaji Viumbe Maji Tanzania (AAT) kwa ajili ya kutoa mafunzo ya muda mfupi ya ufugaji samaki yanafadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kupitia Mradi wa Kikanda wa Ukuzaji Viumbe Maji (EAC TRUEFISH PROJECT).

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA) Dkt. Semvua Mzighani (kushoto) na Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Wakuza Viumbe Maji Tanzania (AAT) Dkt. Charles Mahika (kulia), wakitia saini hati ya makubaliano kati ya FETA na AAT ili wafuga samaki kupatiwa mafunzo ya muda mfupi na FETA kupitia Mradi wa Kikanda wa Ukuzaji Viumbe Maji (EAC TRUEFISH PROJECT) unaofadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO). Wanaoshuhudia utiaji saini huo ni baadhi ya maafisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na FAO. (19.05.2023)

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA) Dkt. Semvua Mzighani (kushoto) na Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Wakuza Viumbe Maji Tanzania (AAT) Dkt. Charles Mahika (kulia), wakibadilishana hati ya makubaliano kati ya FETA na AAT ili wafuga samaki kupatiwa mafunzo ya muda mfupi na FETA kupitia Mradi wa Kikanda wa Ukuzaji Viumbe Maji (EAC TRUEFISH PROJECT) unaofadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO). Wanaoshuhudia utiaji saini huo ni baadhi ya maafisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na FAO. (19.05.2023)

Kabla ya utiaji saini wa hati ya makubaliano ya mafunzo ya muda mfupi ya ufugaji samaki kati ya Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA) na Chama Kikuu cha Wakuza Viumbe Maji Tanzania (AAT) ili wafuga samaki kupatiwa mafunzo ya muda mfupi na FETA kupitia Mradi wa Kikanda wa Ukuzaji Viumbe Maji (EAC TRUEFISH PROJECT) unaofadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO). Washirki walipata fursa ya kupitia makubaliano hayo kabla ya kusainiwa rasmi kwa ajili ya kuanza utekelezaji. (19.05.2023)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni