Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema Serikali inaendelea na juhudi za Kuimarisha uvuvi wa bahari kuu kwa kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) ili kuiwezesha nchi kunufaika na rasilimali za uvuvi hususan zile zilizopo katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari na Bahari Kuu.
Mhe. Ulega aliyasema hayo Juni 07, 2021 wakati akijbu swali la Mbunge wa Kawe, Mhe. Askofu Josephat Gwajima ambaye alitaka kufahamu mpango madhubuti wa kutumia Bahari kwa programu za uvuvi wa Bahari Kuu na michezo ya bahari ili kutengeneza ajira kwa vijana wa Jimbo la Kawe hasa ikizingatiwa nusu ya Jimbo hilo lipo mwambao wa Bahari ya Hindi.
Alisema hadi sasa Serikali ina mpango wa kununua meli tano (5) za uvuvi ambazo zitavua katika maji ya kitaifa, bahari kuu, pamoja na kutoa leseni kwa meli kubwa zinazomilikiwa na Sekta Binafsi.
Aliongeza kuwa Serikali ina mpango wa Kujenga Bandari ya Uvuvi katika Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi ambapo uwepo wa Bandari hiyo utawezesha meli za uvuvi zinazovua katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari ya Tanzania na Bahari kuu, kutia nanga, kushusha Mazao ya Uvuvi na kupata huduma mbalimbali zikiwemo mafuta na chakula ambapo meli hizo zitachangia kutoa ajira kwa wananchi, wakiwemo wa Jimbo la Kawe.
“Serikali inaendelea kuboresha mazingira na usalama wa fukwe ya Bahari ya Hindi ili kuwavutia wawekezaji kuwekeza katika shughuli mbalimbali za michezo katika fukwe hizo," Alisema Mhe. Ulega.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kawe aliyetaka kufahamu siku ambayo Serikali italeta boti kwa ajili ya kuokoa inapotokea madhara na kujua siku serikali itatoa mikopo kwa wavuvi wadogo wadogo wanaotumia mitumbwi ili kuboresha uvuvi wao, Mhe. Ulega alisema Serikali kwa pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi , Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi kupitia polisi marine na ofisi ya Waziri Mkuu zote zinafanya kazi kwa pamoja.
Alisema kwa sasa wana mkakati wa kuhakikisha kwamba panapatikana chombo au vyombo ambavyo vitakuwa vikifanya kazi hiyo ya doria na kazi hiyo itaratibiwa na ofisi ya Waziri Mkuu kwa hivyo na wananchi wa kawe wapo katika mpango wa namna hiyo.
Aliongeza kuwa tumejipanga vyema katika bajeti yetu ya 2021/2022, Serikali ya awamu ya sita ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga vyema huku alitumia fursa hiyo kumkaribisha kwa ajili ya kuhakikisha vikundi na vijana wa pale kawe waweze kupata mashine za boti na waweze kujiunga kwenye vikundi vitakavyo wasaidia kutengeneza vichanja vya ukaushaji wa samaki na hata kutengeneza mashine za kuzalisha barafu wauziane wenyewe ili kukomesha tatizo la upotevu wa mazao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni