Nav bar

Jumapili, 20 Juni 2021

KAMATI YARIDHISHWA NA ELIMU YA UVUVI HARAMU BWAWA LA MTERA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imeridhishwa na elimu iliyotolewa kuhusu uvuvi haramu kwa wavuvi wa bwawa la Mtera.

 

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dkt. Christine Ishengoma ameyasema hayo leo (19.06.2021) baada ya kamati kumaliza ziara yake kwenye kijiji cha Misisiri wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma na kijiji cha Mnadani wilaya ya Iringa ambapo walizungumza na wavuvi na wananchi wa maeneo hayo.

 

Dkt. Ishengoma amesema katika vijiji vyote walivyopita wamekuta wavuvi na wananchi kwa ujumla wanayo elimu kuhusu uvuvi haramu na wanashiriki katika kudhibiti kwa kukamata nyavu haramu na kuziteketeza.

 

Wavuvi wametakiwa kuendelea kudhibiti uvuvi haramu katika bwawa hilo ambalo kwa sasa samaki wamepungua katika baadhi ya maeneo kutokana na Uvuvi haramu.

 

Dkt. Ishengoma amewaahidi wananchi wa kijiji cha Mnadani kuwa atalifikisha tatizo la wingi wa viboko katika bwawa hilo kwa Waziri wa Maliasili na Utalii ili aweze kulishighulikia.

 

Naye Katibu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah amesema kuwa wizara imekuwa ikitoa elimu kuhusu uvuvi haramu na madhara yake kwa wavuvi na wananchi wanaolizunguka bwawa la Mtera ambapo kwa sasa wananchi hao wamekuwa wakishirikiana na serikali kudhibiti na kuteketeza nyavu zisizofaa zilizokamtwa.

 

Dkt. Tamatamah amewaahidi wavuvi wa kijiji cha Miseseri kuwaletea injini moja ya boti mwezi Julai, 2021 ambayo pamoja na shughuli za uvuvi itawasaidia katika kufanya doria za kudhibiti uvuvi haramu.

 

Pia amewaahidi wananchi hao kuwa atawatuma wataalam wa  utafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) kuja kuangalia kutafiti Kama upo uwezekano wa kuweka mbegu ya samaki ili kusaidia kuongeza wingi wa samaki katika bwawa.

 

Dkt. Tamatamah amewasisitiza wavuvi kujiunga kwenye vyama vya ushirika ili waweze kukopesheka na kuweza kupata zana sahihi za uvuvi ambazo mara nyingine hutolewa na wizara.

 

Mkazi wa kijiji cha Mnadani kata ya Izazi wilayani Iringa, Bw. Amiri ameieleza kamagi hiyo kuwa viboko katika bwawa hilo wameongezeka na wamekuwa wakijeruhi na hata kuwauwa wavuvi na hivyo kusababisha wavuvi kutokwenda kuvua. Tatizo hili limefanya samaki kuwa wachache katika masoko na kuwafanya wavuvi kutafuta shughuli nyingine za kuwaingizia kipato na hivyo ameiomba kamati kuwasaidia kulitatua tatizo hilo.

 

Wananchi katika vijiji vyote viwili wameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge na wizara kwa kuwatembele na kusikiliza matatizo waliyonayo na wanaomani kuwa matatizo yao yatatafutiwa ufumbuzi.


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Dkt. Christina Ishengoma akizungumza na wananchi wa kijiji cha Msisiri Kata ya Chipogolo wilayani Mpwapwa wakati kamati hiyo ilipotembelea kijijini hicho kusikiliza changamoto za wavuvi na wananchi kuhusu maendeleo ya Bwawa la Mtera. (19.06.2021)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akijibu maswali ya wananchi wa kijiji cha Msisiri (hawapo pichani) kilichopo Kata ya Chipogolo wilayani Mpwapwa wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ilipotembelea kijiji hicho na kusikiliza kero za wavuvi pamoja na wananchi kuhusu maendeleo ya Bwawa la Mtera. (19.06.2021)

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ambaye pia ni Mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde akitoa mapendekezo yake kwa wananchi wa kijiji cha Msisiri kilichopo wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma mara baada kamati hiyo kutembelea kijiji hicho kuhusu Maendeleo ya Bwawa la Mtera. (19.06.2021)


Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Msisiri wakifatilia majibu na maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na viongozi wakati wa mkutano wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji walipofika kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho kilichopo Kata ya Chipogolo wilayani Mpwapwa  kuhusu za maendeleo ya Bwawa la Mtera. (19.06.2021)


Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Dkt. Christina Ishengoma akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mnadani Kata ya Izazi wilayani Iringa, Mkoani Iringa baada ya kamati hiyo kufanya ziara na kuzungumza na kuwasikiliza wananchi hao kuhusu maendeleo ya Bwawa la Mtera. (19.06.2021)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akitoa ufafanuzi kwa wananchi wa kijiji cha Mnadani Kata ya Izazi wilayani Iringa Mkoani Iringa wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji iliyosikiliza maoni na kero za wananchi kuhusu maendeleo ya Bwawa la Mtera. (19.06.2021)

Mvuvi wa Samaki, Amir Kiselo akitoa maoni yake kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ilipotembelea kijiji cha Mnadani Kata ya Izazi wilayani Iringa Mkoani Iringa kuhusu Maendeleo ya Bwawa la Mtera. (19.06.2021)


Afisa Uvuvi Kata ya Izazi, Onesmo Peter akielezea changamoto wanazozipata wavuvi katika Bwawa la Mtera wakati ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ilipotembelea kijiji hapo wilayani Iringa kwa lengo la kujua Maendeleo ya Bwawa la Mtera. (19.06.2021)


Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mnadani wakifatilia majibu na maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na viongozi (hawapo pichani) wakati wa mkutano wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji walipofika kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho kilichopo Kata ya Izazi wilayani Iringa kuhusu za maendeleo ya Bwawa la Mtera. (19.06.2021)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni