Na Mbaraka Kambona, Dodoma
Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ametoa miezi mitatu (3) kwa Meneja wa
Machinjio ya Dodoma, Victor Mwita kufanya maboresho ya miundombinu iliyopo
katika machinjio hayo ili iweze kutoa huduma inayostahiki na kuchangia ipasavyo
katika pato la taifa.
Waziri
Ulega alitoa maelekezo hayo wakati alipofanya ziara ya kukagua machinjio hayo
yaliyopo jijini Dodoma Juni 8, 2021 ambapo pamoja na mambo mengine alimtaka
meneja huyo kutumia vyema mapato wanayokusanya ili kuboresha miundombinu ya
machinjio hiyo.
“Natoa
miezi mitatu (3) ya kuboresha miundombinu ya machinjio hii, na mimi nitakuwa
nakuja hapa kila mwezi kuangalia ni maboresho gani mmeyafanya, madhumuni yetu
machinjio hii iweze kutoa mchango unaohitajika kwa taifa,” alisema Ulega
Alisema
kuwa lengo la Serikali ya awamu ya sita ni kuona machinjio hiyo inafanya kazi katika
uwezo wake uliosimikwa ili mchango wa sekta ya mifugo katika pato la taifa
uweze kuonekana.
Aidha,
alitumia nafasi hiyo pia kuwakumbusha maafisa wanaohusika katika kukusanya mapato
katika machinjio na maeneo mengine kuwa hawatamvumilia mtu yeyote asiyekusanya
mapato ya Serikali.
“Tuko
imara sana katika ukusanyaji wa mapato, afisa yeyote asiyekusanya mapato ya
serikali tutamtoa mara moja, tunataka tuhakikishe watu wanakusanya kwa haki na
huduma inayotolewa pia itolewe kwa haki, hili jambo tunataka kulisimamia bila
muhali,” aliongeza Ulega
Aliendelea
kusema kuwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali yaende sambamba na uboreshaji wa
mazingira mazuri ya biashara ili kumfanya anayelipa ushuru aone ni haki na ni
halali kulipa, kwani kwa kufanya hivyo biashara ya mifugo itashamiri zaidi.
Naye,
Meneja wa Machinjio hiyo, Victor Mwita alisema kuwa wamepokea maelekezo yote ya
Naibu Waziri huyo na aliahidi kuyatekeleza yote ili kufikia malengo
yaliyokusudiwa.
Alisema mkakati watakaoanza nao ni kuhakikisha wanabana matumizi ili waweze kutumia vizuri mapato watakayoyapata kuboresha miundo mbinu ya machinjio hayo ili iweze kuleta tija zaidi.
Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiangalia Ng'ombe waliopelekwa
katika Machinjio ya Dodoma kwa ajili ya kuchinjwa. Waziri Ulega alifanya ziara
ya kukagua Machinjio hiyo Juni 8, 2021.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (wa pili kutoka kushoto) akishuhudia shehena ya nyama za Mbuzi zinazopakizwa katika gari maalum la kubebea nyama hizo kwa ajili ya kusafirishwa na kuuzwa nje ya nchi alipotembelea machinjio ya Dodoma yaliyopo jijini Dodoma Juni 8, 2021. Kulia ni Mmiliki wa shehena hiyo, Muhamad Azim.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (kulia) akiongea na Mfanyabiashara wa nyama za Mbuzi, Muhamad Azim alipokutana nae katika Machinjio ya Dodoma yaliyopo jijini Dodoma Juni 8, 2021. Waziri Ulega alifanya ziara ya kukagua Machinjio hayo na amemtaka Meneja wa machinjio hayo kufanya uboreshaji wa miundombinu ili iweze kutoa huduma stahiki.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni