Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imepewa semina kuhusu Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kwa malengo ya kujua majukumu yake, muundo wake, utekelezaji wa bajeti, mafanikio, changamoto na mikakati ya kutatua changamoto hizo.
Kamati imepatiwa semina
hiyo leo (11.06.2021) katika ukumbi wa Msekwa D uliopo ndani ya Viwanja vya
Bunge Jijini Dodoma ambapo viongozi wa Wizara waliongozwa na Naibu Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega.
Akizungumza kuhusu semina
hiyo Mhe. Ulega amesema kuwa wizara imeona ni wakati muafaka kufanya semina
kuhusu NARCO ili wajumbe wa kamati hiyo waweze kuielewa na kutoa maoni yao
ambayo yatasaidia sana katika kuhakikisha kampuni hiyo inaendelea kuimarika kwa
kuongeza uzalishaji wa mitamba, nyama na kuzidi kuchangia kwenye pato la taifa.
Mhe. Ulega amesema kuwa
Kampuni hiyo ya Ranchi za Taifa ilipita katika kipindi kigumu na hivyo
kushindwa kujiendesha lakini kutokana na jitihada mbalimbali zilizofanywa na
wizara kwa sasa Kampuni hiyo inajiendesha yenyewe.
Katika
taarifa iliyowasilishwa kwenye Kamati hiyo, imeainisha mafanikio
yaliyopatikana, mipango iliyopo ya kuongeza uzalishaji na maeneo ya vipaumbele yaliyopo
katika bajeti ya mwaka 2020/2021. Maeneo hayo ni Kuboresha Ranchi tano (5) za Kongwa, Ruvu, Kalambo,
Missenyi na West Kilimanjaro ili kuongeza tija katika mnyororo wa thamani wa
mazao ya Mifugo, Kuongeza uzalishaji wa ng’ombe kwa njia ya Uhimilishaji (AI) -
kwa kutumia mbegu bora za ng’ombe wa nyama kama vile Boran na Simental.
Maeneo mengine ni Kudhibiti vifo vya mifugo kwa
kiwango kisichozidi 2% ya wastani wa mifugo, Kuongeza na kuboresha nyanda za
malisho kwa kudhibiti na kuondoa vichaka na
kuimarisha vyanzo vya maji na Kuweka alama za kuonekana katika mipaka ya
ranchi, kuondoa wavamizi na kuimarisha
ulinzi wa mipaka.
Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Dkt. Christina
Ishengoma amesema sasa ni wakati muafaka kwa Ranchi za Taifa kuanza kuzalisha
malisho kwa ajili ya mifugo ambayo yataweza kuwasaidia hata wafugaji
wanaozizunguka ranchi hizo. Vilevile ameshauri ranchi hizo ziweze kutumika kama
mashamba darasa ambapo wafugaji hasa wa maeneo ya jirani wataweza kupata elimu
juu ya ufugaji bora.
Akichangia baada ya taarifa kuwasilishwa mjumbe wa
kamati hiyo, Mhe. Prof. Patrick Ndakidemi amesema kuwa ni wakati muafaka kwa
kamati kuisaidia NARCO. Prof. Ndakidemi amesema kwa kuwa tayari kampuni hiyo
imeshaandaa andiko mradi, ni vema wajumbe hao wakalisoma hilo andiko na kuona
ni maeneo yapi kamati inaweza kuisaidia kampuni hiyo. Vilevile amewasihi NARCO
kuendelea kuyatunza na kuyalinda maeneo yao kwani yanawasaidia wafugaji wenye
changamoto ya maeneo ya malisho kwa kuwakodishia.
Wajumbe
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakitoa maoni na kuuliza
maswali mara baada ya kumalizika kwa uwasilishaji wa taarifa kuhusu Kampuni ya
Ranchi za Taifa (NARCO) wakati wa semina iliyofanyika kwenye ukumbi wa Msekwa D
uliopo katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma. (11.06.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni